Upepo huu wa mafua unaoendelea, unatukumbusha chanjo ni muhimu

24Dec 2021
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Upepo huu wa mafua unaoendelea, unatukumbusha chanjo ni muhimu

UNAPOSALIMIANA na watu hivi sasa, wanne kati ya kumi watakwambia anaumwa. Inawezekana hata anayewasalimia, pia naye ana tatizo hilo hilo.

Kwa sasa, kwenye nchi yetu na dunia nzima kumezuka na tatizo la homa kali, kifua na mafua, kichwa na viungo kunyong'onyea. Ni tatizo lilionekana kuanza kukumba wengi nchini mwanzoni mwa Novemba.

Tumesikia hata wachezaji wa timu kubwa za soka nchini Simba, Yanga, Azam, Mtibwa Sugar, JKT na zingine wakipata tatizo hilo.

Mitaani ndiyo kabisa! Kumekuwa na watu wengi waliopatwa na maambukizi ya ugonjwa huo wa homa na kukohoa na mafua makali.

Ni ugonjwa ambao unasababisha kichwa kuuma, kwenye maungio kama vile kwenye magoti na katikati ya mikono kuuma kama mtu aliyepigwa.

Yupo rafiki yangu mmoja alinipigia simu na kuniambia anaumwa yeye, mkewe, watoto watatu na mfanyakazi wake wa ndani.

Mama mmoja nilimuona anakwenda hospitali akiwa na watoto wake wawili wadogo, wote wakiwa wamekumbwa na tatizo hilo.

Kila mtu anaonekana kushangaa ni upepo gani mbaya ambayo umepita. Wengine wakidai ni mvua za ghafla zilizonyesha na baadaye kuacha, ndizo zilizobadili hali ya hewa na watu wanaanza kuumwa.

Nakumbuka wakati chanjo za ugonjwa wa Covid -19 zilipoanza, wengi walionekana kuzipinga kwa sababu mbalimbali ambazo walikuwa wanazitoa.

Wapo waliosema kuwa huenda baadaye wakawa na matatizo ya kuzaa. Wengine wakadai kuwa zinaweza kusababisha kuua nguvu za kiume. Kuna walioenda mbali sana na kudai kuwa huenda wangegeuka 'mazombi'.

Wale wanaopenda kuangalia filamu za watu wa kutisha wanaweza kuelewa zaidi, inawezekana hawa zamani ndiyo walikuwa wanaitwa mazimwi.

Hadi leo hatujawahi kuona hata mtu mmoja tunayemfahamu aliyechanjwa amegeuka zombi.
Wataalamu wakabainisha kuwa siyo kama mtu ukichanja basi huwezi kupata kabisa maambukizi, la hasha.

Ila kinachosaidia ni kwamba ukichanja, bali unakuwa na kinga hata kama ikija, basi mwili unaweza kukabiliana na misukosuko ya nguvu ya ugonjwa wenyewe.

Hii imeanza kuonekana kwani wengi ambao walikuwa hawataki kuchanja, au kukimbia kwa sababu mbalimbali ndiyo wanaoonekana kupigwa sana na homa hii, kuliko ambao wameshachanjwa.

Ndiyo maana unaweza kumuona mtu anaumwa, lakini bado anakwenda kazini, anafanya shughuli zake kama kawaida.

Anachofanya ni kufuata maagizo tu ya wataalamu ili asiambukize wengine, kuambukizwa na kufuata matibabu mengine, ili apone haraka.

Mfululizo wa homa hizi hizi, zimewapata wengine ambao wamekimbilia hospitalini na kuwalaza, wengine wamelala majumbani hawajiwezi kutokana na kuumwa sana kichwa, kifua, kukohoa na kukosa nguvu.

Ukifuatilia kidogo, utakuta hawa ni wale ambao walikuwa wakipuuzia chanjo. Mbali na hilo, hata kupona kwao wamekuwa wakichukua muda mrefu tofauti na wengine.

Kuna ambao hawajapata kabisa matatizo haya, hawa wengine wao ni wale ambao wameshapata chanjo ya Covid -19.

Hata kama wapo ambao wameshachanja, nimeeleza hapo juu kuwa hawakuteseka sana na maumivu ya ugonjwa, kukaa nyumbani siku kadhaa bila kwenda kutafuta riziki, pia kuchua muda mrefu kupona.

Kwa maana hiyo, ni kwamba wakati kumeonekana kuna mlipuko wa changamoto ya mafua na homa kali, huu ndiyo wakati wa kukimbilia kwenye vituo mbalimbali vilivyowekwa ili kupata chanjo ya Covid - 19.

Wachezaji soka wengi kabla ya ligi kuu kuanza wakiwamo wa Simba wamechanja, lakini hata baadhi yao ambao wamepata maambulizo na kutocheza mechi dhidi ya Kagera Sugar Jumamosi iliyopita, waliendelea na mazoezi kama kawaida, na kuna timu zingine, zikiwamo Azam, Yanga, Mtibwa Sugar zilikuwa na wachezaji wenye matatizo hayo, lakini waliendelea kucheza.

Ni kwa sababu miili yao ina kinga zaidi. Kama isingekuwa hivyo, sidhani kama wangeweza. Wangekuwa wamelala vitandani kama wengine ambao hawajapata chanjo tunavyowaona. 

Kwa maana hiyo sasa Watanzania tujifunze kutokana na hili lililotokea. Chanjo ni muhimu kwa Watanzania wote. Inawezekana kabisa kuwa asilimia 90 ya Watanzania wote wangekuwa wamepata chanjo, changamoto hii isingejitokeza kwa ukubwa huu unaoonekana.

Binadamu siku zote hujifunza kutokana na makosa, lakini inatakiwa Watanzania wanasikosee tena, wahimizane kwenda kuchanja, ili kama kuna tatizo lingine mbele ya safari likute karibuni wote wako vizuri, wameshachanja na wana kinga thabiti mwilini.