Wamachinga kubali kuhama bila shuruti

20Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Wamachinga kubali kuhama bila shuruti

KWA muda mrefu, wafanyabiashara wadogo maarufu kama ‘machinga’ wamekuwa wakifanya biashara zao katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwamo yasiyo rasmi kama kandokando ya barabara, na kusababisha kero kwa watumiaji wa barabara na uchafuzi wa mazingira.

Hali hiyo imeifanya serikali kuchukua hatua za kutaka kuhakikisha wanafanya biashara zao katika mazingira rafiki ambayo watakuwa salama na pia kutochafua mazingira na kuhatarisha afya zao.

Kinachoendelea mkoani Dar es Salaam sasa ni kuwaondoa katika maeneo waliopo na kwenda katika maeneo yakiwamo masoko waliotengewa ili barabara ziwe wazi, lakini wasichafue mitaro ya kupitisha maji ya mvua.

Kwa kuwa hatua hizo za serikali zina nia nzuri kwa ajili yao, wito wetu kwa wamachinga ni kwamba, wazingetia maelekezo ambayo wamepewa ya kuhama ili yafanyike bila shuruti wala mvutano.

Tunashauri hivyo, kwa sababu uzoefu unaonyesha kuwa kila wamachinga wanapohamishwa, huwa kunatokea mvutano kati yao na vyombo vya dola, jambo ambalo kwa upande wetu tunaona si jema.

Tumeshaanza kuona baadhi yao wakifanya ukaidi wakutekeleza maelekezo ya kuondoka katika maeneo yasiyoruhusiwa.

Baadhi wanavunjiwa vibanda, lakini kesho yake wanarejea kwa kupanga bidhaa zao. Serikali ina nia njema ya kutaka wamachinga waendeshe shughuli zao katika maeneo ambayo ni rasmi.

Limekuwa ni jambo la kawaida katika miji kukuta wamepanga bidhaa zao kando ya barabara na kusababisha kero kwa wapita njia, lakini kuhatarisha usalama wao.

Kwa machinga wa Dar es Salaam, Oktoba 18, mwaka huu, ilikuwa mwisho wao kufanya biashara kwenye maeneo yasiyo rasmi, lakini Mkuu wa Mkoa huo, Amos Makalla, juzi alitangaza kuwaongezea siku nyingine 14 za kujiandaa kuhama.

Wiki hii, akihutubia wakazi wa Jiji la Arusha, Rais Samia Suluhu Hassan, aliipongeza Dar es Salaam kwa kuwapanga machinga na kuwezesha maeneo mengi kuonekana vizuri na kurahisisha usafi.

Rais anataka miji na majiji mengine kuiga mfano huo ulioonyeshwa na wenzao wa Dar es Salaam. Na hili tunaona ni muhimu wadau wote kuhusika, kuanzia viongozi hadi machinga wenyewe kushirikiana katika hili.

Tunatambua na kuthamini shughuli za machinga, kutokana na ukweli kwamba wamekuwa na mchango mkubwa kwa watu wengi kujiajiri na kujiingizia kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku, huku wakilipa kodi za serikali.

Lakini ni vyema biashara zao zikafanyika katika mazingira ya usafi na usalama kuliko ilivyo sasa, ambapo wengi wao 'wanavamia' hata maeneo yasiyo rasmi na kusababisha usumbufu kwa wengine.

Jambo lingine ambalo hujitokeza, ni pale mpita njia anapogusa bidhaa zao, hutolewa matusi mazito yakiwamo ya nguoni, na wengine kudiriki kuwapiga baadhi ya watu kwa kukanyaga bidhaa hizo.

Kwa mazingira kama haya, tunaamini kwamba, hatua zinazochukuliwa na serikali za kuwahamisha kutoka kwenye maeneo yasiyo rasmi, zitapunguza kero mbalimbali zinazosababishwa na wafanyabiashara hao.

Rais ameagiza uhamishaji wa machinga ufanyike kistaarabu, na ndivyo tunaona ikifanyika, na matarajio yetu ni kwamba kila kitu kiende sawa, hatimaye maisha yaendelee kama kawaida.

Hata hivyo, tunasisitiza kwamba wamachinga wanawajibika kuheshimu maagizo na maelekezo ya serikali kwa kukubali kuyahama maeneo yaliyokatazwa bila shuruti, kwa kuwa kufanya hivyo ni kutaka kupimana ubavu na serikali, kitu ambacho hawataweza.