Mchakato maoni uraia pacha ni habari njema

15Oct 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mchakato maoni uraia pacha ni habari njema

SERIKALI imesema inakamilisha mchakato wa kupitia maoni ya Watanzania wanaoishi nje (Diaspora), kuhusu kupewa hadhi maalumu itakayowawezesha kushiriki masuala mbalimbali ya maendeleo nchini.

Uraia pacha ni kilio cha muda mrefu cha Watanzania wanaoishi nje na kuwa na uraia wa nchi nyingine kutokana na kushindwa kupata baadhi ya haki kwenye nchi yao na kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ukishakubali kuwa raia wa nchi nyingine basi unakuwa umeukana uraia wa nchi yako.

Licha ya kuwa walizaliwa, kukulia, kusoma, kuishi na kuwa na familia zao Tanzania, haki zote muhimu hupotea wanapopata uraia wa nchi nyingine na kila wanapokuja nchini wanakuja kama wageni licha ya kwamba asili yao ni nchini.

Aidha, kutokana na hali hiyo wameshindwa kufungua akaunti na kuweka fedha kwenye benki za nchini, jambo ambalo kwao ni kikwazo kikubwa, kumiliki ardhi au kama alipewa mgao wa mali za urithi au ardhi anapoteza umiliki wake.

Uamuzi wa serikali wa mchakato wa kupitia maoni yao kwa ajili ya hatua zaidi za kwenda bungeni kupitishwa kwa ajili ya utekelezaji unaleta matumaini ya uwezekano wa Watanzania hao kupata haki zao muhimu.

Tunapongeza uamuzi huo kwa kuwa kwa miaka mingi imekuwa hitaji la kila Mtanzania anayeishi nje, lakini imeshindikana kutekelezeka kwa sababu mbalimbali ambazo serikali imezieleza, na sasa imeona kuna umuhimu wa kuchambua maoni yao na kuyafanyia kazi.

Zipo nchi zinaruhusu uraia wa nchi mbili na umekuwa ni wenye manufaa kwa nchi zinazoendelea kwa kuwa wananchi wenye uraia wa nchi nyingine wamewekeza na kufanya shughuli za maendeleo ambazo zimekuwa zenye manufaa kwa nchi zao za asili, wengine wamerudisha utaalamu nyumbani.

Tunaamini mafanikio yao ni ya Watanzania wote kwa kuwa kama wakiweka fedha kwenye benki za nchi yao ya asili zitazunguka ndani na kukuza uchumi wa nchi, kuongeza ajira na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Pia, kukiwa na uhakika wa kupata haki yao ni rahisi kuleta wawekezaji wengi na wao kuwekeza nchini kwa kuwa wana kuwa na haki ya ardhi na mali nyingine watakazowekeza.

Wapo Watanzania wanaomiliki mali kwenye nchi mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zimenufaisha uchumi wa nchi hizo.

Kwa Mtanzania aliye na uraia wa nchi nyingine hana haki ya kupiga kura kwa kiongozi yeyote katika uchaguzi wowote unaofanyika nchini, bali anakuwa na haki ya kuchagua viongozi kwenye nchi ambayo amepata uraia.

Watanzania hawa ambao wamepoteza haki yao ya kuzaliwa kwa kuwa walipata uraia wa nchi nyingine miongoni mwao kuna wataalamu wa fani mbalimbali ambazo zingeweza kulisaidia taifa kwa kiasi kikubwa iwapo wangepewa nafasi ya kuwekeza nchini.

Iwapo wangewekeza maana yake utaalamu wao ungebaki nchini, ungerithishwa kwa Watanzania wengine na kusaidia kuboresha huduma mbalimbali za kijamii, kwa kuwa utaalamu walionao wakati mwingine hapa nchini haupo au umekosa watu wa kuonyesha kwa vitendo, na wakati mwingine kutumika gharama kubwa kumuita mtaalamu kutoka nje ya nchi.

Wakati wa Bunge Maalum la Katiba hoja ya uraia pacha iliibuka na katika Rasimu ya Katiba ya Tume ya Marekebisho ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba, liliwekwa kama sehemu ya mapendekezo ya Watanzania wanavyotaka Katiba mpya iwe.

Aidha, Watanzania waishio nje ya nchi zaidi ya milioni mbili walisaini waraka maalum kwamba Watanzania hao wapate haki ya kupiga kura kwa kuwa wana haki ya kuzaliwa nchini.