Waliokaidi amri ya Magufuli kushtakiwa

27Jan 2016
Salome Kitomari
Nipashe
Waliokaidi amri ya Magufuli kushtakiwa

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imesema inakamilisha taratibu za kisheria za kuwashtaki waliokaidi agizo la Rais Dk. John Magufuli la kulipa kodi kwa makontena yaliyotolewa bandarini.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi TRA, Richard Kayombo, alisema jana kuwa hatua za kisheria zitakazochukuliwa ni pamoja na kulipa faini mbalimbali na kodi inayotakiwa.

“Taratibu za kisheria zinaendelea ikiwamo kushikilia mali zao na ni lazima walipe kodi na adhabu mbalimbali,” alisema.

Tangu Rais Magufuli atoe muda wa siku saba, wafanyabiashara 19 wamelipa zaidi ya Sh. bilioni 11.8.

Mapema Disemba, mwaka jana, Rais alipokutana na wafanyabiashara alitoa muda wa siku saba kwa wafanyabiashara hao waliobainika kukwepa kodi kuzilipa na watakaoshindwa mkono wa sheria utachukua mkondo wake.

Wafanyabiashara hao ni wale waliobainika kukwepa kodi katika makontena 329, ambayo yalibainishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza Novemba, mwaka jana, katika bandari ya Dar es Salaam.

Kutokana na madudu hayo, Rais alitengua uteuzi wa aliyekuwa Kamishna Mkuu wa TRA, Rashed Bade, na Waziri Mkuu aliwasimamisha vigogo wengine ambao wanadaiwa kuhusika na upotevu huo.

Pia Waziri Mkuu alifanya ziara ya kushtukiza Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kubaini zaidi ya makontena 2,000 yalipita bila kulipiwa kodi na kuagiza kuchukuliwa hatua kwa wahusika wote wakiwamo watumishi wa Bandari Kavu (ICD).

Kutokana na hali hiyo, Rais alivunja Bodi ya TPA na kumtimua Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Awadh Massawe.

Hadi sasa zaidi ya watumishi 70 wa TPA na TRA wamesimamishwa kazi kwa uchunguzi zaidi, huku wengine wakifikishwa mahakamani kujibu tuhuma za uhujumu uchumi.
0000