Shule hiyo ambayo ipo chini ya Manispaa ya Sumbawanga imekuwa ikipokea fedha kutoka serikali kuu kwa ajili ya kujiendesha pamoja na gharama za kuwasafirisha watoto makwao wakati wa likizo na kuwarejesha shuleni baada ya shule kufunguliwa.
Aidha, shule hiyo ina idadi ya watoto 80, miongoni mwao walemavu wa ngozi ni 32, wavulana wakiwa 14 na wasichana 18 na waliobaki ni wasiiona na wenye uono hafifu.
Taarifa kutoka shuleni hapo zinaeleza kuwa, tangu shule hiyo ifunguliwe juzi ni watoto 12 tu walioripoti tena kwa kugharimiwa na wazazi au walezi wao.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo , Orthor Mkaranga, amethibitisha kuwapo kwa hali hiyo na kueleza kwamba, utaratibu ni kwamba watoto hao wanapofunga shule wanasindikizwa makwao na baadhi ya walimu na wafanyakazi wa shule.
“Shule inapokaribia kufunguliwa baadhi ya walimu na watumishi wa shule wanawafuta makwao na kuja nao hadi hapa shuleni, lakini kutokana na ukata wa fedha tumeshindwa kuwafuata ,” alisema.
Mkaranga alisema shule hiyo pia inakabiliwa na upungufu wa vitanda ambapo wanafunzi watatu wanalazimika kitanda kimoja na pia haina uzio na huduma za maji na umeme zimesitishwa kutokana na ufinyu wa bajeti .
Alisema wanafunzi hao wanatoka maeneo mbalimbali nchini, ikiwamo Dar es Salaam, Mbeya, Kahama (Shinyanga), Kigoma, Katavi na halmashauri zote za mkoa wa Rukwa .
Alipoulizwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Sumbawanga, George Lupilya, alisema hana taarifa juu ya changamoto hizo zinazoikabili shule hiyo na kuahidi kufuatilia.










