Ubungo mataa kipaumbele cha foleni barabara ipi?

14Jan 2016
Christina Mwakangale
Nipashe
Ubungo mataa kipaumbele cha foleni barabara ipi?

FOLENI katika mataa ya kuongoza magari eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam yawezekana ni sugu kuliko maeneo mengi ya jiji hilo.

Iwe siku za mwishoni mwa wiki au za kawaida ndio zinazidi iwe kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.
Eneo hili, foleni yake inatokana na makutano ya barabara nne zinazokutana hapo Ubungo.
Magari yatokayo mjini na ya Mbezi Luis kwenye barabara maarufu ya Morogoro yaelekea ndiyo mzizi wa foleni hii. Licha ya kujengwa barabara mpya kwa ajili ya mabasi yaendayo haraka(Dart) bado mambo sio shwari.
Licha ya hiyo, taa za kuongozea magari barabarani katika eneo hili, huachwa zikijiongoza zenyewe hasa majira ya usiku mwingi sana na alfajiri. Yaani kuanzia majira ya saa sita usiku hadi 11 alfajiri.
Badala yake, askari wa usalama barabarani huchukua fursa hiyo ya kuyaongoza magari kwa kuangalia wapi wanaona kuna kipaumbele kikubwa.
Hali hiyo inachochea wakati fulani kuongezeka foleni kutoka upande mmoja, hususan kwa magari yatokayo Mwenge, Buguruni kuonekana hayapewi kipaumbele.
Hali hii imekuwa ikilalamikiwa na kila anayepita au kutumia barabara hii, kwani lazima anakuwa ni moja kati ya wale walioonja joto ya jiwe ya foleni katika eneo hili.
Kukaa zaidi ya saa mbili au tatu katika taa hizo sasa limekuwa kama ni jambo la kawaida linalosababisha baadhi ya abiria kuamua kushuka usafiri wanaoutumia hasa wa daladala ili kuvuka mataa na kutafuta maarifa mengineyo.
Abiria hao, wanashuka si kwamba wanakuwa wamefika safari wanayokwenda la hasha lengo lao ni kuvuta taa na kwenda kutafuta usafiri mwingine upande wa pili.
Foleni katika jiji hili, kwenye makutano ya barabara ni kero kubwa licha ya serikali kuwa na mikakati ya kujenga ‘fly overs’ katika baadhi ya maeneo ikiwamo makutano ya barabara ya Nyerere na Mandelea, eneo la Tazara, jijini Dar es Salaam.
Oktoba mwaka jana Rais John Magufuri wakati huo akiwa Wazuiri wa Ujenzi, alishuhudia uwekaji saini wa mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo, uliotarajiwa kuanza Novemba mwaka huu.

Ujenzi huo unatarajiwa kutumia miezi 35 na utagharimu sh Sh. bilioni 100 utajengwa kwa msaada wa serikali ya Japan itakayotoa Sh.bilioni 93.43 na Tanzania sh. bilioni 8.26.

Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Patrick Mfugale, akizungumza katika hafla hiyo alibainisha kuwa mafanikio ya mradi huo, yanatokana na juhudi za serikali ya Tanzania kuomba msaada wa namna ya kutatua kero ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam, kutoka serikali ya Japan, mwaka 2008.
Serikali ya Japan kupitia Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), lilikubali ombi hilo na kutuma timu ya wataalam waliopendekeza eneo la Tazara na mengine kujengwa barabara za juu, ili kukabiliana na changamoto ya msongamano.
Ni muhimu sana utekelezaji wa mradi huo ukafanyika kwa wakati pamoja na kutafuta mikakati ya muda mfupi ili kupunguza tatizo hilo.