SMZ ‘yawachimba mkwara’ mabalozi

12Jan 2016
Nipashe
SMZ ‘yawachimba mkwara’ mabalozi
  • “Itakuwa ajabu Balozi kususia sherehe za Mapinduzi wakati hazina uhusiano na mambo ya uchaguzi, hivyo na yeye atakuwa sehemu ya wapinga Mapinduzi ya Zanzibar.”

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema mabalozi watakaosusia sherehe za Maadhimisho ya Miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar leo kwa sababu ya matatizo ya uchaguzi wa Zanzibar, watakuwa sehemu ya wapinga Mapinduzi ya mwaka 1964.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Balozi wa Cuba nchini, Jorge Tormo

Msimamo huo ulitolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mohamed Aboud Mohamed, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana.
Alisema matatizo yaliyojitokeza kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu na kufutwa matokeo yake na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) hayana uhusiano na sherehe za kitaifa, ikiwamo Maadhimisho ya miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Itakuwa ajabu Balozi kususia sherehe za Mapinduzi wakati hazina uhusiano na mambo ya uchaguzi, hivyo na yeye atakuwa sehemu ya wapinga Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema.
Waziri Aboud alisema mabalozi wote wamealikwa kuhudhuria sherehe hizo kupitia Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kikanda, Kimataifa na Afrika Mashariki.
Alisema hata hivyo wanataarifa ambazo sio rasmi kuwa, kuna mabalozi wa nchi tatu hawatahudhuria kwa sababu ya matatizo ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, ambao matokeo yake yalifutwa Oktoba 28, mwaka huo, kwa madi ya kufanyika udanganyifu.
Aidha alisema wana taarifa za siri za kuwapo baadhi ya mabalozi ambao wanashirikiana na vyama vya upinzani Zanzibar kuzorotesha hali ya amani na utulivu visiwani humo baada ya kujitokeza kasoro za uchaguzi huo.
Alisema kwa mujibu wa sheria za kimataifa, mabalozi wanatakiwa kuwa sehemu ya kusadia kudumisha amani na kuimarisha ushirikiana baina ya nchi na sio kusadia kuchochea vitendo vya uvunjifu wa amani katika nchi.