Yanga wasipojizatiti wataula wa chuya

06Feb 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Yanga wasipojizatiti wataula wa chuya

WAJUA kilichotokea siku ya kwanza ya duru la pili la Ligi Kuu ya Vodacom katika majiji ya Tanga na Dar es Salaam?
Jijini Tanga hususan kwenye uwanja maarufu wa Mkwakwani, wenyeji Coastal Union waliitumia vizuri methali isemayo “Mgeni aje mwenyeji apone.” .

Mgeni kwa muktadha huu, ilikuwa Yanga iliyosafiri kutoka Dar es Salaam kupimana ubavu na Coastal Union, maarufu kwa jina la ‘Wagosi wa Kaya.’

Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mabingwa watetezi, Yanga, waliifunga Coastal Union mabao 2-0 wasijue kitakachowakuta watakapokwenda Tanga kwenye mechi ya duru la pili.
Nikumbushe tu kuwa Coastal Union ni ndugu wa Simba. Rangi zao ni nyekundu na nembo za vilabu vyao zina picha za wanyama. M-mbwa mwitu kwa Coastal Union na ‘Wekundu wa Msimbazi’ ni mnyama aitwae mfalme wa nyika yaani Simba.
Simba nayo katika duru la kwanza ikiwa ugenini jijini Tanga kupambana na African Sports ‘Wana Kimanumanu’ kwenye uwanja uleule uliokuwa kaburi la Yanga Jumatano iliyopita, iliikaribisha African Sports kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
‘Wekundu wa Msimbazi’ nao kama ndugu zao, Coastal Union, walidhihirisha methali ya “Mcheza kwao hutuzwa” walipoichapa bila huruma African Sports mabao 4-0 na kuwajongelea karibu zaidi Yanga na Azam kwa tofauti ya alama tatu tu.
Yasemwa African Sports na Yanga ni ndugu. Wahenga walisema “Udugu wa nazi mkutano pakachani.” Kama ndivyo ulivyo udugu wa timu hizo, Allahu ya aalam (Mungu ndiye ajuaye zaidi).
Kama methali ya “udugu wa nazi …” yamaanisha hivyo, basi ilikuwa siku mbaya kwa Yanga na African Sports kwani wote walikiona cha mtema kuni katika mechi zao za ugenini. Ilikuwa siku ya wanyama – Simba na m-mbwa mwitu -- kutamba kwenye miitu yao.
Mpaka Jumamosi iliyopita, nafasi ya Yanga kutetea ubingwa wake ilikuwa wazi kwa timu nne zilizo juu – Yanga, Azam na Simba (zote za Bandari ya Salama) na Mtibwa Sugar ya Turiani, Morogoro.
Hiki ni kipindi cha ‘lala salama’ au ‘buriani’ kwani timu itakayopoteza mechi katika duru hili la mwisho itakuwa imejiweka katika hali tete.
Simba waliwaambia ndugu zao, Coastal Union: “tupigie hao jamaa wa Jangwani kelele zipungue jijini nasi tutawanyamazisha watani wenu (African Sports). Wale warejee Dar na hawa warudi Tanga vichwa chini.”
Ndugu wawili walishinda nyumbani ilhali wawili walishindwa ugenini. Ilikuwa ‘kaka nipigie’ chambilecho vijana wa mjini.
Ni kama Coastal Union waliiambia Yanga kuwa “Hakuna mrukaji aliyefaulu kukwepa kifo.” Maana yake hata mtu akawa mrukaji kiasi gani hawezi kukikwepa kifo. Ni kweli kwamba mpaka Jumamosi iliyopita, Yanga walikuwa hawajafungwa mpaka walipotiwa nuksi (kisirani) na Coastal Union.
Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, ‘Wagosi wa Kaya’ (Coastal Union) walikuwa mbele kwa bao moja lililofungwa na mchezaji wa zamani wa Simba, Miraj Adam kwa mkwaju ya adhabu ndogo uliomparaza kipa wa Yanga, Deo Munishi na kutinga kimiani.
Hiyo ilikuwa dakika ya 27 ya kipindi cha kwanza huku mashabiki wa Coastal wakiwaambia Yanga warejeshe, vinginevyo wafungwe bao la pili. Haikuwa hivyo kwani mpaka mwisho wa kipindi cha kwanza, Yanga walishindwa kurudisha.
Katika juhudi za kutaka kurejesha bao, Yanga ikaongezwa bao la pili lililofungwa na Juma Mahadhi aliyepokea pasi kutoka kwa Hamad Juma. Bila ajizi aliutumbukiza wavuni na kuwaacha wachezaji na mashabiki wa Yanga katika bumbuwazi.
Oh! masikini Yanga! Maji yakimwaika hayazoleki. Ni methali ya kupigia mfano mambo yaliyoharibika; kuwa yamekwisha haribika wala hayawezi kutengenezeka tena na hata kama ingewezekana hayawi kama awali.
Ligi ya msimu huu ndio mwisho wa Yanga na Coastal Union kwani hili ni duru la pili. Coastal Union imesawazisha mambo kwani duru la kwanza ilifungwa na Yanga mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Labda ni jambo lililowapa Yanga jeuri kuwa wangekwenda kuongeza alama zake kutoka 39 kuwa 42 lakini Wagosi wa Kaya wakasema “abadan kufungwa mbele ya mashabiki wetu.” Wakalipa deni la mabao 2-0 waliyofungwa duru la kwanza jijini Dar es Salaam.
Wahenga walisema “Ukiujua huu, huu huujui.” Maana yake ukilijua jambo hili kuna jingine usilolijua. Hutumiwa kutukumbusha kwamba hamna binadamu anayeweza kuyafahamu mambo yote. Lazima yatakuwepo mambo asiyoyajua.
Ligi imefika patamu.
marobarnabas@yahoo.com
0715/0784 33 40 96