Wakati serikali inafanya jitihada za kutomomeza mimba hizo, ili kuwanusuru wanafunzi wa kike walioko katika hatari ta mimba za utotoni ambazo kimsingi si salama maendeleo yao ya elimu na maisha kwa ujumla.
Licha ya tatizo hilo kugusa hisia za kila mpenda maendeleo ya elimu, bado inaonekana kwamba jamii haijahamasika kutoa ushirikiano wa karibu kwa vyombo vya dola ili kuwafichua wahusika wa vitendo hivyo.
Baadhi ya wazazi na walezi hutuhumiwa kupokea rushwa kutoka kwa watuhumiwa ili wasifikishwe kwenye vyombo vya sheria na kuchukuliwa hatua stahiki iwe fundisho kwao na kwa wengine wenye tabia za aina hiyo.
Inawezekana tuhuma hizo zikawa na ukweli ndani yake, kwani kuendelea kuwapo kwa mimba nyingi za wanafunzi, huku idadi ya watuhumiwa ikiwa halingani na idadi ya waliopata mimba.
Inasikitisha kusikia kwamba ndani ya mwaka mmoja, katika kipindi cha kati ya mwaka 2021 hadi 2022, wanafunzi 9,011 wa shule za msingi na sekondari wamepata mimba. Hali inayoonyesha tatizo bado ni kubwa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga ndiye anayebainisha hayo hivi karibuni, jijini Dodoma na kufafanua kuwa
katika kipindi cha mwaka 2021 na 2022 wanafunzi wa shule za msingi waliopata ujauzito ni 1,554 na Sekondari ni 7,457.
Mimba kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari nchini, zinachangia kurudisha nyuma maendeleo yao kielimu, hivyo ni wazi ipo haja kwa wadau wote wa elimu kuendelea kushirikiana na serikali katika vita hii.
Ni vyema wazazi na walezi kushirikiana na vyombo vya dola kuhakikisha watuhumiwa wanakamatwa, ili sheria iweze kuchukua mkondo, kwani njia hiyo inaweza kupunguza wingi wa mimba hizo kama si kumaliza tatizo kabisa.
Kama jamii, lingekuwa jambo jema kama itaona umuhimu huu, kwani Tanzania yenye wasomi wengi wa kike waliobobea katika fani mbalimbali itawezekana na maendeleo inawezekana iwapo watalindwa.
Lakini kama jamii itaendelea kuwaficha wahusika wa vitendo hivyo, itakuwa ni sawa na kurudisha nyuma juhudi za serikali na wadau wa elimu za kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora.
Pamoja na hayo, ninadhani ipo haja kwa wanafunzi kupewa elimu ya kujitambua na kufahamu wajibu wao kwa jamii na taifa, ili wajithamini na kuepuka vishawishi vinavyosababisha wapate mimba au kuacha shule.
Kumekuwapo na sababu nyingi ambazo zimekuwa zikitajwa kuchangia kuwapo kwa mimba, mojawapo ikiwa ni wazazi na walezi kuwa na tamaa ya kutaka kupata mali.
Sababu nyingine ni ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, umbali wa shule na hasa sekondari za kata, ambazo husababisha wanafunzi kutembea kwa muda mrefu kufuata elimu na kujikuta wakikumbana na vishawishi njiani.
Hizo ni baadhi ya sababu zinazoendelea kutajwa huku kukiwa na juhudi mbalimbali zinazofanywa na serikali kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo linatakiwa kumalizwa ili watoto wa kike wawe huru.
Lakini ninaamini kuwa wanafunzi wa kike wakipewa elimu ya kujitambua na kufahamu wajibu wao kwa jamii na taifa, hawatakuwa tayari kukubaliana na uamuzi wa wao au kukubali vishawishi vya njiani.
Kwa ujumla ni kwamba, mimba bado zimeendelea kuwapo na sababu za mimba hizo ni zile zile, ambazo inawezekana bado huenda sasa zinatakiwa zifanyiwe kazi ili kupata ufumbuzi wa kudumu.
Njia mojawapo ya ufumbuzi wa kudumu ni kuwapo elimu ya kujitambua ili wasishawishike kirahisi na kujikuta wakipata na mimba na kukatisha masomo au kukataa shule na kuingia katika ndoa za utotoni.