Sambamba na kuimarisha viwanda serikali, inakusudia kufikisha nchi kwenye uchumi wa kati kwa kuwa na viwanda vipya vya kisasa zaidi, kufufua vilivyokwama ili kufanya kazi tena na kuhamasisha wawekezaji kuja nchi kufungua miradi ya kiuchumi.
Kuwekeza kwenye viwanda kunategemea wasomi na watafiti na hilo halikuachwa nyuma, serikali inajenga shule za sayansi kwa kila mkoa kwa ajili ya kufundisha wasichana ili taifa liwe na wasomi wanasayansi kinamama.
Ni jambo jema na la muhimu kuwekeza na kuwa na taasisi imara za kitafiti zinazoweza kuuhamisha utafiti kutoka maabara na kuufikisha kwa wananchi vijijini ili kitendawili cha kuwa na uchumi wa viwanda kuteguliwa.
Hivyo, kuwekeza katika teknolojia ni muhimu na kuanzisha uwekezaji mkubwa wa kiutafiti hasa kwenye kuboresha kilimo ambacho ndicho mzalishaji mkubwa wa malighafi za viwanda hivyo.
Tanzania inahitaji kukabiliana na changamoto za uzalishaji mashambani ili kuiwezesha nchi kuwa na malighafi za kutosha viwandani, utoshelevu wa chakula na kutibu hali ya mazingira inayoharibiwa na kilimo kisichojali mazingira.
Utafiti ni vyema uanze kuelekezwa kwenye kilimo ambacho sasa kipo taabani kutokana na ukame, wadudu waharibifu na matumizi makubwa ya viuatilifu ambavyo vinatishia afya za walaji na mazingira.
Baadhi ya mikoa wakulima wakubwa wa mahindi, mboga na matunda wanalizwa na wadudu waharibifu wa mazao.
Mathalani, wadudu wanashambulia mboga na kuwalazimisha wakulima kutumia viuatilifu vingi kupindukia bila mafanikio.
Mahindi yanashambuliwa na kusababisha hasara ya mabilioni ya pesa kila mwaka na kinachohitajika ni uwekezaji kwenye utafiti na kutambua aina za wadudu ili kuwadhibiti.
Utafiti huo ni vyema uanze kutengeneza dawa za asili ili kupunguza matumizi ya kemikali za viwandani.
Ikumbukwe viuatilifu vya viwandani ni sumu inayoathiri kila mmoja ambaye anaweza kukutana nayo katika vyakula, hewa anayovuta na maji anayotumia.
Hivyo basi, kuna kila sababu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika suala la kuwekeza kwenye utafiti na kusomesha wataalamu wenye uwezo wa kusimamia viwanda na kazi za kutafiti.
Kuwapo na wataalamu kunamaanisha kuajiriwa Watanzania walio na sifa za kusimamia viwanda hivyo na kufanya utafiti huku wakisimamia viwanda.
Wataalamu watafanya utafiti kwa kupima virusi, vimelea na wadudu mbalimbali wanaoshambulia mazao.
Lakini pia, kupitia utafiti watatengeneza mbegu zenye ukinzani na virusi, wadudu na viwavi baada ya kutambua aina ya virusi na mahali vinapopatikana
Watafiti hao na watalaamu watasaidia kufunza wakulima mbinu za kutumia kanuni za kilimo bora na kustawisha mazao ili kupata tani nyingi za mazao hayo ikiwa ni kuzalisha malighafi za kutosha viwandani.
Ni wataalamu na watafiti watakaofanikisha kusambaza mbegu kimkakati ili kudhibiti magonjwa badala ya kutibu mazao yakiwa yameathirika.
Utafiti utawezesha wakulima kumiliki viwanda vyao, kuwa na soko la mazao yao na kupunguza umaskini hivyo Watanzania kunufaika na kilimo chao mashambani.
Changamoto za kukosekana wataalamu zitamalizika kwa kuwekeza kwenye masomo ya sayansi, kuandaa walimu, maabara na vifaa vya kutosha vya maabara katika shule hizo maalumu.
Wimbo wa Tanzania ya viwanda inawezekana utakuwa na uhalisia kama taifa litawekeza na kuimarisha utafiti unaotatua matatizo hasa kwenye kilimo ambacho ni uti wa mgongo wa uchumi wa taifa.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








