Tutazalisha maskini mbumbumbu

25Mar 2016
Restuta James
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Tutazalisha maskini mbumbumbu

UNAWEZA kudhani ni simulizi za zamani za kale, lakini ndio hali halisi ya Tanzania yetu.

Kwamba wanafunzi katika Shule ya Msingi Zawa, Wilaya ya Maswa mkoani Simiyu, wanalazimika kusoma darasa moja kwa kupeana migongo.

Shule hiyo ina vyumba vitatu vyenye wanafunzi 513, kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, huku wakitumia mbao mbili za ubao katika chumba kimoja wakati mwalimu akifundisha darasani hali inayosababisha mwingiliano wa masomo.

Wakati fulani niliwahi kusema kwamba Watanzania wengi wanamatumaini bandia. Wanamatumaini bandia kwa sababu baadhi ya wanafunzi wanaenda shule kucheza, walimu wanafundisha wanafunzi wasio wategemea, kwamba wanafunzi wa darasa la pili na la tatu wanakaa kwenye darasa moja wakipigana visogo. Hawa wanafundishwa Kiswahili, wenzao wanafundishwa hisabati, ndani ya darasa moja!

Hawa lazima wawe na matumaini, lakini ya bandia kuhusu hatma ya maisha yao.

Walimu na wanafunzi hawa wawapo shuleni wanaomba wasipate haja, maana hakuna choo; miaka 50 baada ya uhuru wa nchi yao.

Mwanafunzi huyo akihitimu elimu ya msingi, anahamia sekondari ya kata tena isiyo na walimu wala madawati, maabara wala maktaba, umeme wala maji, akifanikiwa kufika chuo kikuu, inamlazimu kuandamana kudai mkopo; lakini bado anamatumaini ya maisha yake baada ya chuo.

Ukienda hospitali ndio usiseme, wajawazito wamelala mzungu wa nne hata hawajui ni saa ngapi watapata huduma; kwa sababu halmashauri imeshasema tatizo si vitanda ila pa kuviweka, kwa maana ya kwamba hakuna sehemu ya kujenga jengo jipya! Kwamba eneo la hospitali ‘limevamiwa’ na wananchi, bajeti ya serikali imefika kikomo, haiwezi kuwalipa wavamizi hao ili ipanue hospitali na kuokao maisha ya walioko hospitalini.

Hata kwenye zahanati na vituo vya afya vichache vilivyopo, dawa hakuna, kisa; sera inatoa mwongozo wa ugawaji wa dawa kulingana na hadhi ya majengo! Kwamba zahanati bila kuzingatia inahudumia watu wa vijiji vingapi, haiwezi kupata dawa sawa na kituo cha afya. Vivyo hivyo kwenye hospitali ya wilaya, mkoa na rufaa. Yaani wagawaji hawaangalii idadi halisi ya watu, bali wameng’ang’ania kuangalia zahanati inauwezo wa kuhudumia watu wangapi kinadharia sio kivitendo.

Ni katika mipango hii, wananchi wameendelea kuwa na matumaini bandia wakisubiri kukamilika kwa michakato, mikakati na tafiti mbalimbali zinayofanywa na serikali yao kuona namna nzuri ya kutumia zahanati, vituo vya afya na hospitali zilizopo kuwapatia huduma bora.

Lakini pia, wapo Watanzania wenzetu wanaohitaji chakula cha dharura, wana njaa kwa sababu mvua hazikunyesha kama inavyotakiwa na hivyo kusababisha mavuno kidogo. Kwenye maeneo mengine, mvua zimeharibu mazao, njaa inawanyemelea.

Katikati yao wapo wateule wachache wanakula na kusaza, wanaohujumu jasho lao kwa kugawiana mishahara na posho nono.

Mathalani, kuna wakala mmoja wa serikali ambaye mtendaji wake mkuu analipwa mshahara wa zaidi ya Sh. 18 milioni kwa mwezi, Sh. 800,000 kila mwezi kwa ajili ya nyumba, ana shangingi la bure la kutembelea, dereva na familia yake inatibiwa na serikali; hii ni anasa na dharau kwa Watanzania maskini wasiomudu hata mlo mmoja kwa siku.

Mara kadhaa nimeandika hali hii na kuna watu wamenikosoa kwamba hali ya nchi sio mbaya kiasi kinachoelezwa.

Wao wanakwenda mbali zaidi na kueleza kwamba hata hao wanafunzi wa vyuo vikuu wanaolilia nyongeza ya posho, wanakaa Mlimani City! Mimi sipingani sana na wanaokutana na wanafunzi kwenye sehemu hiyo wakistarehe, shida yangu ni kwa wale wanaofikia hatua ya kukatisha masomo kwa kukosa nauli ya kwenda chuo kutoka hosteli anapokaa.

Shida yangu ni hao wajawazito wanaolala mzungu wa nne, shida ipo kwa viongozi wachache wanaojimegea maeneo makubwa ya ardhi kama miliki zao sasa na vizazi vyao baadaye, huku wananchi wengi wakihamahama kupisha umegaji huu.

Kuna haja ya serikali kuchukua hatua za haraka kupunguza ufa kati ya watawala na watawaliwa, maskini na matajiri vinginevyo kwa elimu hii, tunazalisha maskini mbumbumbu.