Timu ziepuke kusajili kwa mazoea

29Feb 2016
Adam Fungamwango
Nipashe
Mjadala
Timu ziepuke kusajili kwa mazoea

LIGI Kuu Tanzania Bara imeingia mzunguko wa pili na tayari inaelekea ukingoni.

Kwa klabu ambazo zina viongozi na mabenchi wa ufundi makini na masuala ya soka ni wakati ambao wameshaanza kuona wachezaji itakaowahitaji kwa ajili ya msimu ujao.

Ni wakati ambao timu inayohitaji mabeki wa pembeni, wa kati, viungo wa pembeni na mastraika imeshawaona kwenye mechi za ligi zinazoendelea na labda mazungumzo yameanza kufanyika.

Ulaya baadhi ya timu zimeshaanza kuwanyemelea baadhi ya wachezaji ambao imeshawaangalia na kuridhika nao.
Kwa makocha viongozi wenye maskauti, au watu wanaotambua vipaji vya wachezaji, tayari watakuwa wameshaona japo baadhi ya wachezaji wanaoweza kuwasajili.

Hivi karibuni michuano ya fainali za Mataifa Afrika (CHAN) iliyomalizika nchini Rwanda kwa Congo DR kutwaa ubingwa, kulikuwa na wachezaji wazuri wanaoweza kusajiliwa na timu za Simba, Yanga na Azam zenye utamaduni wa kupenda kusajili wachezaji wa kigeni.

Mfano zingeweza kuwatuma hata wachezaji wao wa zamani kwenda kuangalia baadhi ya mechi kwa ajili ya kuangalia vipaji na uwezo wa wachezaji kulingana na maeneo wanayohitajika kuziba mapengo.

Staili hii inafanya ligi inapomalizika tu viongozi kuanza kufanya mazungumzo na wachezaji inaowahitaji.
Hii itafanya kazi hiyo kumalizika mapema na makocha kupata muda wa kuanza maandalizi.

Tumeshuhudia msimu uliopita ikishindwa pia kumsajili Kelvin Nadisenga kutokana na muda na kuangukia kwa Pape Abdoulaye Ndaw.

Kumsajili mchezaji wakati yupo nyumbani ligi imeisha ni kama kucheza kamari, kwa sababu huwezi kujua kiwango chake kwa wakati huo.

Mchezaji husajiliwa baada ya kuonekana kuwa na kiwango bora kwenye ligi au michuano iliyomalizika karibuni.

Huwa tunashuhudia kapashika nguo kuchanika kwa klabu za Simba na Yanga kugombania wachezaji na hii ni kutokana na kutojipanga mapema na kuanza shughuli hiyo wakati muda umekwisha.

Kuna kipindi Azam ilikuwa na mfumo mzuri wa kusajili wachezaji mapema baada ya ligi kumalizika.
Wakati Simba na Yanga zikigombea wachezaji, Azam inakuwa tayari imemaliza kazi ya usajili.

Lakini kwa siku za karibuni, naiona Azam nayo kama imeshaanza kufuata mkumbo wa klabu za Simba na Yanga.
Ni wakati sasa wa viongozi kuangalia masilahi mapana ya klabu, kutafuta wachezaji mapema kwenye uwezo na kuingia nao mikataba mapema.Kwa kufanya hivyo itawasaidia kuepuka kusajili wachezaji wasio na sifa.

Simba na Yanga lazima zitambue kuwa ndizo klabu kubwa Tanzania na hata Afrika Mashariki na Kati, hivyo lazima zifanye usajili kwa mahitaji na siyo kwa ajili ya kujifurahisha.

Viongozi wa klabu na makocha waache kufanya kazi kwa mazoea na badala yake wanapaswa kubadilika kutokana na mazingira au wakati.Kwa kufanya hivyo kutasaidia kunua soka la Tanzania na kuleta ushindani katika michezo kwa jumla.