Jamal Malinzi alipata kuwa Katibu Mkuu wa Yanga miaka ya nyuma. Sasa ndiye Rais wa TFF. Vilabu vyote vya kandanda (ikiwamo Yanga) nchini vipo chini ya TFF. Vinapaswa kufuata kanuni zilizowekwa na shirikisho hilo.
Aidha, shirikisho hilo lina wajibu wa kuvisimamia vilabu vyote vya kandanda kwa ushauri, kuvikosoa na kuviadhibu vinapokwenda kinyume cha katiba zao zinazotambuliwa na TFF.
Nauliza: Rais wa TFF, Malinzi anaona haya kuikemea klabu yake au anaiacha iende hovyo bila kufuata katiba?
Shirikisho hilo linapaswa kujua kila kitu kinachoendelea kwa wanachama wake. Mikataba ya makocha, wachezaji na mishahara yao. Pia kuhakikisha uhamisho wa wachezaji wa kigeni na vibali vya kufanya kazi nchini.
Vilevile kuweka rekodi sahihi za adhabu wanazopewa wachezaji wakati wa mechi, orodha ya wachezaji wa timu za taifa wenye matatizo, maradhi na waliofariki. Kuwa na picha zao pamoja na mechi walizocheza mpaka walipostaafu kucheza kandanda.Wapo wachezaji wengi walioichezea Taifa Stars lakini wametangulia mbele ya haki.
Wajibu wa TFF ni kuhakikisha vilabu vinafanya chaguzi zao kama katiba zao zinavyoelekeza. Mara nyingi Simba na Yanga hubabaisha kufanya chaguzi zao kwa madai kuwa zipo kwenye ligi au michuano ya kimataifa.
Kutofanya uchaguzi kwa visingizo vya timu kuwa kwenye ligi au mechi za kimataifa kutasimamishaje uchaguzi ilhali wanaochagua ni wanachama na si wachezaji?
Kwa muda sasa kumekuwa na vuta-nikuvute baina ya Yanga, TFF na Wizara ya Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo kuhusu Katiba ya Yanga inayoonekana kuwa kitendawili. Ofisa wa wizara anayeshughulikia usajili wa wachezaji amesema mabadiliko ya Katiba ya Yanga hayatakubaliwa bila kusajiliwa.
Katiba mpya ya Yanga tayari imeleta mgawanyiko miongoni mwa wanachama. Baadhi wanaikubali na wengine wanasema ilipitishwa na wanachama kwenye mkutano ulioitishwa bila kufuata taratibu.
Ni kweli kwamba Simba na Yanga ndizo timu zinazoingiza watazamaji wengi popote zinapocheza nchini. Pia ni dhahiri kuwa TFF linanufaika kwa fedha za viingilio vya mechi zao. Hali hiyo pengine, imesababisha shirikisho hilo kuwa legelege kwa timu hizo.
Mara nyingi vilabu hivyo hukatiza mikataba ya wachezaji na makocha bila kuwalipa stahiki zao. Badala ya shirikisho kushughulikia matatizo hayo, walalamikaji kupeleka kesi kwenye mashirikisho ya kimataifa kama CAF na FIFA ili kupata ufumbuzi. Matatizo hayo yangemalizwa hapa nchini na TFF badala ya kupelekwa nje ya nchi.
Ni wajibu wa TFF pia kuhakikisha adhabu zitolewazo na vilabu kwa wachezaji zinastahili ama la. Vilevile kuhoji ni kwa nini wachezaji watovu wa nidhamu ndani na nje ya uwanja hawachukuliwi hatua na viongozi wao.
Kufanya hivyo kungesaidia kudumisha nidhamu ya wachezaji si viwanjani tu bali hata nje ya viwanja. Vilabu vishinikizwe kufuatilia mienendo ya wachezaji kama ulevi wa pombe na mihadarati (dawa za kulevya), dawa za kuongeza nguvu.
Endapo kutakuwa na ushirikiano mzuri baina ya TFF na vilabu, hapana shaka ushirikiano kama huo waweza kuleta mafanikio muhimu katika kandanda humu nchini kuliko ilivyo sasa.
Nilipokuwa naandaa makala haya, kulikuwa na habari kuwa Mkurugenzi wa Uanachama wa TFF, Eliud Mvella alisema shirikisho hilo limeiandikia Yanga na vilabu vingine nchini kuhusu kufanya uchaguzi.
marobarnabas@yahoo.com
0715/0784 33 40 96


.jpg?itok=nfwjwDzv)








