Kama ulipata bahati ya kutazama mechi kati ya timu ya vijana ya Tanzania chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) dhidi ya timu ya 'Mafarao Watoto' Misri iliyofanyika kwenye Uwanja wa Taifa, utakubaliana nami.
Vijana wa Kitanzania walipiga 'mpira mwingi' kiasi cha 'kuwakuna' waliokuwa wakishuhudia mchezo huo na hata wale waliokuwa wakiutazama kwenye luninga.
Si kama vijana wa Misri hawana vipaji, la hasha. Walionekana kucheza vile vile kama kaka zao. Kwa staili yao ile ile. Misri ni moja kati ya mataifa ambayo pia yamejaaliwa na vipaji vya wachezaji.
Lakini nilichoona ni kwamba bado wanaonekana kucheza kitoto mno, wakiwa hawana mbinu nyingi kama kaka zao, lakini pia miili yao bado haijapata misukosuko, yaani hawajakomaa.
Kwa upande wa Serengeti Boys walionekana moja kwa moja ni wachezaji waliokamilika, baadhi wakiwa na uwezo wa kucheza hata Ligi Kuu Tanzania Bara.
Baadhi walionekana kabisa kuwa huenda wanacheza soka la ushindani huko mitaani kwao na watu wazima, ndiyo maana walikuwa wanacheza wakiwa wana nguvu, kasi na kucheza soka la moja kwa moja la ushindani.
Matokeo yake ni kwamba Serengeti Boys ilifanikiwa kushinda mabao 2-1 kwenye mechi hiyo ya kimataifa ya kirafiki.
Timu hizo zinatarajia kurudiana tena kesho kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Hii si mara ya kwanza kuona timu nzuri za vijana hapa nchini.
Lakini cha ajabu ni kwamba baada ya muda mfupi, ni wachezaji wachache tu ndiyo wataonekana kwenye medani ya soka. Wengine wala hatutajua wanakoishia.
Kwa wenzetu Wamisri sina shaka. Majina haya haya ya wachezaji kama utayahifadhi sehemu, baada ya miaka mitatu au minne utayakuta ndiyo wapo kwenye timu za Ligi Kuu nchini Misri ikiwemo Zamalek au Al Ahly.
Baadhi yao unaweza kuona wakiwa nje ya nchi yao wakicheza soka la kulipwa kwenye klabu kubwa tu Ulaya.
Uzuri wa wenzetu hawaendi kinyume cha mfumo wa soka jinsi ulivyo.
Wachezaji hawa hawa tuliowafunga ndiyo wanawalea na baadaye kuliletea taifa na klabu zao sifa tele pamoja na mataji.
Labda ni wachezaji wachache sana na wenye vipaji maalum, ndiyo wanaoweza kupatikana bila kupitia kwenye timu hizi za vijana, pamoja na mpango maalum ya kukuza vipaji.
Ni wachezaji hawa hawa baada ya miaka kadhaa ndiyo utakuta wanaunda timu ya taifa ya kutisha ya Mafarao, huku sisi tukiwa wakati mwingine hatuna hata mchezaji mmoja kati ya hawa waliocheza juzi kama ilivyokuwa kwa nyota wale waliong'ara Brazil kwenye michuano ya vijana.
Tofauti ya mafunzo pia itaonekana, kwani watakuja tena wachezaji hawa wakiwa hawachezi tena kitoto, wakiwa wamekomaa, kasi, ujuzi na ujanja zaidi.
Hii inaonyesha kuwa wa wachezaji wenzetu wanakuwa kwenye mafunzo na kila wanavyozidi kukua wanazidi kuongezewa mbinu zaidi.
Kwa upande wetu unaweza kukuta badala ya wachezaji kuongezeka uwezo, wengi wao unaporomoka.
Hii haitokani na kukosa mafunzo tu peke yake, lakini hata mazingira ya maisha yetu hapa nchini yanachangia wachezaji kutomudu kuendelea kujibidisha kwenye soka, badala yake mchezaji anaangalia kitu kingine cha kuweza kujikwamua kimaisha na hapo ndipo anaposhindwa kufanya mambo mawili kwa wakati mmoja.
Wakati mwingine wachezaji hawa hawa tena wanalewa sifa za mapema na kuanza kufanya mambo ambayo yanakwenda kinyume na maadili ya soka na kujikuta wakiishia njiani.
Kwa miaka mingi hizi zimekuwa sababu ya Bongo kuwa na wachezaji wazuri wa timu za taifa za vijana, lakini baada ya miaka michache wengi wao hupotea kwenye medani ya soka, badala yake wanabaki wachache mno.
Hata kwenye klabu za Ligi Kuu Tanzania Bara, ni wachezaji wachache ambao wamewahi kupitia timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17.
Itakuwa tunafanya kazi ya bure kama wachezaji hawa waliowafunga Misri kutowaona wakicheza kwenye timu mbalimbali za Ligi Kuu ili kuendeleza vipaji vyao na baadaye kuwa msaada kwenye kikosi cha Taifa Stars.
Kinachohitajika sasa ni matunzo, pamoja na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) na kuwa mashindano mengi ya vijana ili kuwaweka wachezaji wao kwenye hali nzuri ili wasiishie kusikojulikana kama ilivyotokea kwa wengine huko nyuma.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








