Rais Magufuli endelea kuwakomesha hawa wezi

24Feb 2016
Richard Makore
Nipashe
Mjadala
Rais Magufuli endelea kuwakomesha hawa wezi

MKUU wa nchi ambaye ni Rais John Magufuli ametangaza rasmi kwamba amekuta ndani ya serikali hali ni mbaya 'imeoza' na kila mahali anapogusa pameharibika kwa rushwa.

Rais Magufuli ambaye aliingia madarakani Novemba 5, mwaka jana, amekuwa akirudia kauli hiyo mara kwa mara anapopata nafasi ya kuzungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari.

Kauli hii ya Rais ni nzito, lakini mbaya zaidi inatia huruma na simanzi kwa nchi na kwa Watanzania wote bila kujali tofauti zao.

Nasema hivyo kwa sababu kabla ya Rais Magufuli hajatoa kauli hiyo, Watanzania wengi na mimi nikiwamo tuliamini kwamba kila kitu ndani ya serikali kilikuwa kinakwenda vizuri.

Binafsi nilikuwa naona maisha yanaenda vizuri, napanda gari naenda kazini narudi, nalala vizuri naamka, nasafiri huku na kule narudi na kila kitu nilikiona kipo safi.

Lakini kumbe nchi ilikuwa imefika mahali pabaya kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ubadhirifu ndani ya serikali huku kukiwa na wanyonyaji wa kutupwa ambao wao fedha siyo tatizo kwao kama alivyosema Rais Magufuli.

Uozo huu umejulikana kutokana na uzalendo wa dhati alionao Rais Magufuli kwa nchi yake kwa kuwa mamlaka aliyonayo hata kama asingetoa siri hii , hakuna mtu ambaye angehoji ama angemlazimisha aseme.

Kama Rais Magufuli asingekuwa mkweli, Watanzania tungeendelea kuamini kwamba kila kitu ndani ya serikali kinakwenda vizuri.

Kwa kauli yake amesisitiza kwamba wakati anaingia madarakani alikuta rushwa imeshamiri ndani ya serikali na hadi sasa ni mbaya na ndiyo maana ameanzisha utaratibu wa kuwawajibisha watumishi wa serikali wanaotafuna fedha za umma.

Mpango huu unaweza kuchukua miaka mitano kwa Rais Magufuli kufumua serikali na kuijenga upya kwa kuwa hali ilivyo inaonyesha kuwa uongozi uliopita haukufanya jitihada za kutosha kwa muda mrefu kupambana na vitendo hivyo.

Wakati wote tangu tupate uhuru Tanzania haijawajhi kukaa bila serikali, lakini haya anayosema Rais Magufuli mtu anaweza kudhani kuwa huko nyuma serikali ilikwenda likizo.

Haya ni maneno ya Rais mwenyewe ambaye anasema Tanzania ilikuwa imefika mahala pabaya na akasema hiyo ndiyo hali aliyoikuta wakati anaingia madarakani.

Mtu unaweza kujiuliza nani aliifikisha nchi mahali ilipo kiasi kwamba Rais anapata shida kuirekebisha ili Watanzania wote wanufaike na matunda ya nchi yao.

Wakati Rais Magufuli akitoa kilio hiki, watumishi wa serikali wamebakia kuwa wale wale na sasa wanajifanya kushtuka kana kwamba walikuwa hawajui kilichokuwa kikiendelea.

Ili Rais Magufuli amalize kazi hii ya 'kutumbua majipu’ kwa haraka, anatakiwa kuwaondoa wote walioifikisha nchi hapa ilipo.

Watendaji wa kata, tarafa, wilaya, mkoa, wakurugenzi wa taasisi za umma pamoja na mawaziri wengi wao ni wale wale na walikuwapo wakati nchi inafika hapa ilipo.

Siyo hao tu, hata baadhi ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama nao wanalalamikiwa kwa ubadhirifu wa fedha za umma japo hawajafikiwa kutumbuliwa majipu.

Nasema hivyo kwa sababu Rais Magufuli amekiri kwamba kila mahali anapogusa pameoza na hali hii inatisha kwa kuwa ni hatari kwa nchi yetu.

Hawa watendaji wa serikali ndiyo majipu sugu na ambayo Watanzania wangependa kuona yanatumbuliwa.
Kwa bahati nzuri, Rais Magufuli inaoonekana anazo taarifa nyingi na za kutosha kuhusu haya majipu na anachotakiwa kukifanya ni kupambana nayo mpaka mwisho.

Kwa kifupi, Watanzania wengi wamefurahia sana jitihada za Rais Magufuli za kuyatumbua majipu, lakini wanachohoji ni je, pamoja na kazi hiyo atafanikiwa kujenga mfumo imara wa kuweka nidhani na uadilifu serikalini?
Bila kuzingatia hilo, maana yake Rais Magufuli akimaliza muda wake na kuondoka anaweza kuja mtu mwingine akaturudisha nyuma badala ya kwenda mbele.

Rais Magufuli ahakikishe anateua wakuu wa wilaya wazuri na waandilifu, wakurugenzi wa halmashauri waadilifu na wachapa kazi, wakuu wa taasisi za umma na kuajiri watumishi wazuri ndani ya serikali.

Tanzania hapa ilipo haina uhaba wa wasomi ambao ni wachapa kazi na waadilifu na lazima tuondokane na utaratibu wa kuteua watu kwa kujuana hususani makada wa chama tawala kupewa kipaumbele hata kama hawana uwezo wala uadilifu.
Kila uteuzi utasikia watu walewale kana kwamba hakuna watu wengine na tabia hii inatakiwa kuachwa na ifike mahali masuala ya kuteua watu kwa kuangalia itikadi za vyama yaishe.

Kulikuwa na mazoea siku za nyuma kwamba mtu akiwa kada mzuri wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) anayejua kuongea sana hata kama siyo muadilifu, basi atateuliwa kuwa mkuu wa wilaya au mkoa.

Hayo tuachane nayo kwani inawezekana utaratibu huu ndiyo ulioifikisha nchi hapa ilipo mpaka Rais Magufuli anasema hali ya rushwa na ubadhirifu ndani ya serikali inatisha.

Mheshimiwa Rais, endelea kutumbua majipu na yanayogoma kutumbuka yafanyie upasuaji mkubwa ili kukata nyama yote inayong'ang'ania na kuitupa.

Hii inaweza kuwa njia pekee ya kukusanya mapato ya kutosha ili kuiwezesha serikali kupanga mipango ya maendeleo kwa ajili ya wananchi wote.