Lengo la kuondoa ombaomba hao ni kutaka kuliweka jiji katika hali ya safi, kuondoa fikra tegemezi akilini mwa wananchi hao lakini pia kuwezesha watoto wa ombaomba hao ambao hutumiwa kama vitega uchumi, kurudi shuleni.
Akizungumza jijini mapema wiki hii, Mkuu wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliwataka ombaomba hao kurudi makwao wenyewe na iwapo watashindwa, watarudishwa kwa nguvu kuanzia kesho Jumatatu.
Mkuu huyo wa mkoa ambaye kitaratibu Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, akalitaka Jeshi la Polisi kushiriki kukamilifu kwenye operasheni hiyo ili kuhakikisha hakuna ombaomba atakayebaki kwenye mitaa ya jiji.
Uamuzi wa RC Makonda ni mzuri na utasaidia kuepusha si tu kuchafua mazingira, bali pia ajali ambazo ombaomba wanaweza kukutana nazo wanapokuwa katika harakati za kuomba msaada.
Ni kawaida kuwakuta ombaomba wakiwamo watoto na hata watu wazima wakiwa kwenye makutano ya barabara wakivizia magari yasimame ili waombe kwa abiria na madereva.
Wakati mwingine ombaomba hao hukaa ama kwenye maeneo ambayo ni hatari kwa usalama wao hasa kwa kuzingatia kwamba ajali haina kinga.
Kwa maana hiyo, hatua zilizochukuliwa na Makonda ni za kuungwa mkono hasa ukizingatia tatizo la ombaomba mijini linaenda sambamba na kuwakosesha masomo watoto wao, kwani kuna kundi kubwa la watoto wenye umri wa kwenda shule, lakini wamekuwa wakitumika kuomba fedha na kukosa haki yao ya msingi ya kupata elimu.
Inafaa tujiulize, watoto wanaotumika kuomba msaada wa fedha badala ya kupelekwa shule watakuwa ni Watanzania wa aina gani hapo baadaye?
Hatua inayochukuliwa na Makonda, hivyo basi, ni ya kuungwa mkono.
RC ameshasema kuwa operasheni ya kuwaondoa ombaomba itakuwa endelevu, lakini mimi ninaongezea kwamba iwe endelevu kwa vitendo na siyo kwa maneno.
Ninasema hivyo kwa sababu operesheni ya kuwaondoa ombaomba jijini Dar es Salaam haikuanza leo wala jana bali ni miaka mingi na wamekuwa wakiondolewa lakini ya muda wanarudi na kuendelea na shughuli zao kama kawaida kama ambavyo imewahi kutokea miaka ya nyuma kabla yake wakati wa uongozi wa Yusuf Makamba, Said Kandoro na Said Mecky Sadik.
Kurejea kwa ombaomba walioondolewa na MaRC waliopita hao kulitokana na operasheni zao kuwa endelevu kwa maneno na siyo kwa vitendo.
Ili operesheni iwe endelevu kwa vitendo ni lazima, baada ya kuwaondoa, vyombo vya mkoa visimamie kwa karibu ili kila atakayejaribu kurejea akutane na mkono wa dola.
Vinginevyo mambo yanaweza kuwa yale yale ambayo tumekuwa tukiyashuhudia ya kuwaondoa kisha wakarejea.
Binadamu huwa ana kawaida ya kujaribu jambo na akikuta hakuna kizuizi, basi anaweza kufanya mambo yake aliyokusudia, lakini akijaribu na kukuta kibano, basi huogopa.



.jpg?itok=nfwjwDzv)







