Laiti tungejua yale yatakayotokea mbele yetu muda mfupi ujao, mambo tuyafanyayo sasa tungeyaepuka au kuyabadilisha kabla ya hatari. Hebu sikia kilio cha kijana huyu kabla sijaendelea kujadili. “Mimi yamenikuta makubwa. Nilianza mahusiano na dada mmoja akiwa amehitimu kidato cha nne. Anatoka kaya masikini, nikaanza naye mahusiano. Wakati huo mimi ni mganga wa hospitali ngazi ya cheti. Nikaamua kumpeleka chuo akasome uuguzi (nursing). Nikamgharimia masomo na mavazi, matibabu kwa miaka miwili. Alipohitimu akaja kwangu akakaa wiki tatu kisha akasema amepigiwa simu amepangiwa sehemu ya kufanyia kazi katika zahanati ya serikali, nikamruhusu kwenda kuripoti. "Cha ajabu aliporipoti tu kazini akakata mawasiliano na mimi mpaka hivi sasa. Ilikuwa ni tangu mwaka jana mwezi Oktoba; hadi leo hanipigii simu wala nini. Tayari amesahau kuwa nilimtoa mbali katika mazingira magumu ya shida. Na kwao ni familia masikini sana hata nyumba imeezekwa kwa manyasi. "Nilimtafutia chuo kizuri kwa gharama ya shilingi milioni 1.3/- kwa mwaka, mbali ya chakula. Lakini sasa amenitelekeza bila kujua sababu. "Naomba ushauri dada Flora. Napatikana Ushetu katika kituo cha afya Bulugwa, Kahama. Naitwa Kuya Magetta (0689949301) Nifanyeje?" Msomaji wangu, bila shaka umemsikia mwenzetu na masahibu yaliyomkuta. Ama kweli Maisha Ndivyo Yalivyo. Mwanadamu hata umfanyie wema kiasi gani atakulipa mabaya tu. Angalia bibie huyo, baada ya kupata mafanikio katika elimu na hivyo kupata kazi, tayari amemsahau yule aliyemfungulia njia. Hakuweza kurudi nyuma na kutambua kwamba yupo mtu aliyejiunganisha naye ambaye ndiye aliyekuwa chimbuko la baraka zake. Mtu anakuhangaikia, anakusomesha shule nzuri, chuo kizuri, unamaliza masomo, unapata kazi, halafu mtu huyu unamsahau? Ajabu na kweli. Haya mambo yanatokea sana lakini ni hatari kwa kuwa yanapingana na maagizo ya Mwenyezi Mungu. Mungu anasisitiza kwamba unapofanikiwa usimsahau. Hii akimaanisha kwamba kama amekutoa katika mateso makubwa akakuepusha nayo, halafu unamsahau, hata yeye anabaki anashangaa na kujiuliza; ni mwanadamu wa aina gani huyu? Nabii Musa aliwaambia Waisrael kwamba wanapofanikiwa wasimsahau Mungu. Na hii ni baada ya kuwavusha jangwani miaka 40 pasipo kudhurika. Katika Biblia Takatifu kitabu cha Kumbukumbu la Torati 8:14-17; neno la Mungu linasema; Basi hapo moyo wako usiinuke, ukamsahau BWANA, Mungu wako, aliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa. 15; Aliyekuongoza katika jangwa lile kubwa lenye kitisho, lenye nyoka za moto na nge, nchi ya kiu isiyokuwa na maji, aliyekutolea maji katika mwamba mgumu. 16; Aliyekulisha jangwani kwa mana, wasiyoijua baba zako, apate kukutweza, apate kukujaribu, ili kukutendea mema mwisho wako. Ujumbe katika maandiko haya ya Mungu unatuonyesha kuwa Mungu ndiye aliyekuwa amebeba baraka za wana wa Israel. Na kwa kisa cha hapo juu, huyo bibie ameona amefanikiwa na kusahau mara chanzo cha mafanikio yake ambaye ni huyo mpendwa wake. Hata Mungu akasisitiza kuwa unapofanikiwa usimsahau aliyewezesha mafanikio yako, ina maana yapo madhara yanayoweza kumpata yule aliyesahau chanzo cha mafanikio yake. Huyo msichana ambaye alikuwa si chochote wala lolote, akaendelezwa na kijana huyo akitegemea ndiye mke wa ndoto zake, leo hii amefanikiwa badala ya kumshukuru anakata kabisa mawasiliano naye. Kijana huyu ushauri wangu kwake nimemuomba awe mtulivu, amuombe Mungu amuonyeshe mwanamke aliyemkusudia yeye kuwa ndiye atakuwa mkewe. Inawezekana hicho kituko alichofanya bibie huyo, siyo kwa bahati mbaya, lipo jambo ambalo kijana ameepushwa. Akumbuke kuwa mwanadamu hataishi kwa mikate tu bali kwa kila litokalo katika kinywa cha BWANA. Yapo mambo mengine unapoyatafakari sana, hupati majawabu, hayo mwachie Mungu ambaye anayajua yote yanayoonekana na yasiyoonekana. Mambo mengi tumefichwa, ungejua mapema ungeyakwepa lakini kwa Mungu haiko hivyo. Angalia andiko hili: Mhubiri 8:7 imeandikwa; kwa kuwa hajui yatakayokuwako; kwa maana ni nani awezaye kumweleza jinsi yatakavyokuwa? Kijana huyu angejua yatakayotokea wakati anamsomesha bibie, pengine angesitisha, lakini alifichwa hakujua kitakachotokea baadaye. Sasa anagumia maumivu moyoni. Alimtoa kipofu tongotongo, muziki wake sasa ndio huo! Asiogope, maadam anaishi atampata mwingine wa baraka zake. Naishia hapa kwa leo, mpe ushauri kijana mwenzako. Ukiwa tayari kuwa huru kuwasiliana nami kwa ujumbe mfupi kupitia simu ya ofisi namba 0715268581 (usipige), au barua pepe; HYPERLINK "mailto:[email protected]"[email protected] au HYPERLINK "mailto:[email protected]"[email protected]
Nilimsomesha, amepata kazi kanitosa! Nifanyeje?
07Feb 2016
Flora Wingia
Nipashe Jumapili
Maisha Ndivyo Yalivyo
Nilimsomesha, amepata kazi kanitosa! Nifanyeje?
MPENZI msomaji, yapo mambo mengine ukiyasikiliza unabakia kucheka badala ya kusononeka. Ndipo ninapojiuliza; tutaondokana na vifungo hivi lini?