Ni wakati wa kurudi kwenye maadili

15Dec 2016
Sabato Kasika
Nipashe
Mjadala
Ni wakati wa kurudi kwenye maadili

MWAKA huu wa 2016, Desemba 9 nchi yetu ilitimiza miaka 55 ya uhuru ilioupata mwaka 1961 kutoka kwa wakoloni wa Kiingereza.

Na miaka mitatu baadaye, Tanganyika ikaungana na Zanzibar na kuzaliwa nchi inayoitwa Tanzania.

Kila inapofika Desemba 9, Watanzania huwa wanakumbuka kuzaliwa kwa taifa lao la Tanganyika huru, ambalo waasisi wake waliweka mambo muhimu ya kuzingatiwa, yakiwamo maadili ya viongozi na watu kuwa wazalendo kwa nchi yao.

Hayo ni miongoni mwa mambo muhimu kwa nchi, ambayo viongozi walitambua thamani na faida ya maadili huku Watanzania wakitumikia zaidi nchi yao kwa kuzingatia dhana ya uzalendo.

Maadili ni hali anayopaswa kuwa nayo kiongozi aliyepewa dhamana ya kuongoza wizara, taasisi au idara ya serikali kwa kuangalia zaidi maslahi ya umma, badala ya kujiangalia yeye binafsi au na familia yake tu.

Wakati huu ambao nchi imetimiza miaka 55 ya uhuru, kila Mtanzania anajua fika jinsi baadhi ya viongozi walivyopoteza maadili ya uongozi na baadhi ya watu wake kupoteza uzalendo kwa nchi yao.

Hayo yote ndiyo chanzo cha Rais John Magufuli kuibuka na mpango usiotarajiwa wa kutumbua majibu unaoendelea nchini kwa lengo la kutaka kuhakikisha viongozi wanarudi kwenye mstari.

Viongozi wa aina hiyo ndiyo ambao wamekuwa wakichangia kuyumbisha nchi kwa vile baadhi yao hushiriki moja kwa moja kufilisi nchi, au kuielekeza katika mikataba tata inayowapa maslahi makubwa watu binafsi.

Kuna mifano mingi ya mikataba hiyo, ambayo sioni haja ya kuitaja kwa sababu imekuwa ikisemwa mara kwa mara na sasa tunashuhudia jinsi Rais Magufuli anavyopambana kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa.

Ukifuatilia kwa wananchi wa kawaida, hali ni kama hiyo, ambapo ni jambo la kawaida kukuta mzazi akimwacha mtoto akifanya mambo yasiyolingana na maadili kwa sababu tu hakumzaa yeye.

Siyo hapo tu, unaweza kukuta watu wakiharibu mazingira au kuhujumu nyara za serikali, lakini hakuna atakayethubutu kusema au kuzuia hali hiyo isiendelee kana kwamba hakuna madhara yoyote.

Kwa mifano hiyo michache kati ya mingi, utaona ni kwa jinsi gani nchi ilivyochakachuliwa na kubaki kila mtu akimnyooshea kidole mwenzake, bila kujua nani kati yao ana mamlaka gani katika kusimamia maadili na kujenga uzalendo mioyoni mwao.

Nijaribu kukumbusha tu kwamba wakati ule utaratibu wa Watanzania kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kama moja ya mikakati ya kuwajaza Watanzania uzalendo, kulikuwa na njia mbili muhimu.

Mojawapo ilikuwa ni kwa mujibu wa sheria ambapo wanafunzi waliokuwa wakihitimu kidato cha sita walilazimika kwenda kwanza JKT, kabla ya kuanza vyuo vikuu au vile vya elimu ya juu.

Na njia nyingine iliwalenga watu waliojitolea wenyewe kujiunga na jeshi hilo.

Utaratibu huo ulisimamiwa vyema na serikali ya awamu ya kwanza na ya pili, ambako Watanzania wakiwa JKT, walijifunza mbinu za ulinzi wao binafsi, wa nchi lakini pia walijifunza maadili na uzalendo kwa nchi yao.

Kwa Watanzania waliowahi kupitia JKT wanaelewa ninachosema hapa, lakini kwa wale ambao hawakupata bahati hiyo nawajulisha kwamba, JKT ilikuwa ni moja kati ya taasisi za kijeshi za serikali zilizokuwa mhimili mkubwa wa maadili na uzalendo.

Lakini sasa yote hayo ni kama yameachwa, na matokeo yake kila mtu bila kujali wadhifa wake anafanya atakalo hata kama halina maslahi kwa Watanzania na taifa kwa ujumla.

Ingawa utaratibu wa watu wakiwamo wanafunzi kwenda JKT umerejeshwa upya, lakini ni wazi kwamba kusimama kwa muda mrefu kwa utaratibu huo kumechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uzalendo.

Binafsi ningekuwa mmoja kati ya watu mashuhuri wanaoweza kusema wakasikilizwa mara moja ndani ya nchi hii, ningeshauri nchi iandae makongamano ya mara kwa mara ya kujadili maadili na uzalendo kwa taifa.

Ninasema hivyo kwa sababu sina uhakika iwapo tutaandika au kuifanyia marekebisho makubwa katiba ya nchi lakini tukaendelea kuwa na baadhi ya viongozi wasiojua nini maana ya maadili na uzalendo.

Maana yangu ni kwamba, wananchi wa kawaida nao wasipojitambua kuwa wanao wajibu wa kulilinda na kulipigania taifa lao dhidi ya maovu, siamini kama Katiba mpya pekee inaweza kusaidia kutuondoa hapa tulipo.

Labda katika mabadiliko yanayopiganiwa ya Katiba, kama yataendelea, mambo hayo yaingizwe katika Katiba na yafafanuliwe wazi kuwa kiongozi atakayekutwa na kosa la kuvunja maadili ataadhibiwaje.