Napongeza mpango huu wa polisi lakini umakini utumike

02Mar 2016
Mashaka Mgeta
Nipashe
Mtazamo Yakinifu
Napongeza mpango huu wa polisi lakini umakini utumike

SERIKALI kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, imetangaza mkakati mahususi wa kuwakagua waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, ili kujiridhisha kwamba hawahusiani na mipango ya ujambazi na vitendo vingine vya jinai.

Waziri wa wizara hiyo, Charles Kitwanga, amesema kumekuwapo na taarifa zinazothibitisha ongezeko la matumizi ya bodaboda katika vitendo vya uhalifu kama ujambazi, hivyo wahusika katika biashara hiyo wanapaswa kuwa wavumilivu na kutoa ushirikiano kwa polisi.

Kwanza niwe miongoni mwa wanaoipongeza hatua hiyo ya serikali, lakini kwa kutambua kwamba itakuwa na changamoto nyingi zinazohitaji weledi mpana kwa askari polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vitakavyohusika.

Kwa maana bodaboda zimeripotiwa kutumika kwa namna tofauti katika matukio ya aina hiyo. Zipo zinazotumiwa na wahusika halisi wakiwa na silaha zinazotumia risasi za moto, nyingine zikitumika kwa kuwasafirisha wahusika kabla na baada ya ‘kumaliza kazi.’

Ndio maana ninapoipongeza serikali kwa hatua hiyo, ninawajibika kuitahadharisha serikali hususan polisi, wasiwekeza katika kuwasimamisha na kuwakagua bodaboda tu, bali kupata taarifa sahihi zitakazowasaidia kufuatilia mienendo ya wahalifu wanaojivisha taswira ya bodaboda ili kutimiza malengo yao.

Kwa upande mwingine, kuliainisha kundi la bodaboda si mara ya kwanza kwa kada za kijamii kuainishwa katika kufanikisha kudhibiti vitendo vya uhalifu.

Itakumbukwa kwamba wafanyabiashara wengine hasa wanawake wanaouza chakula maarufu kama ‘mama ntilie’ ama wanaotembeza bidhaa wakijulikana kama ‘wamachinga’, wamekuwa wahanga wa kadhia za matukio yanayohusiana na kudhibiti uhalifu.

Hivyo polisi wanapopewa jukumu la kuwasimamisha na kuwakagua bodaboda, serikali iwe makini ili mkakati huo mwema usigeuzwe kuwa ‘pango’ la unyanyasaji, dhuluma na kila aina ya uovu dhidi ya vijana wasiokuwa na hatia.

Hata kabla ya kutangazwa kwa mkakati huo, askari polisi hasa wanaotumia pikipiki wakijulikana kama ‘tigo’ wamekuwa vinara wa kuwanyanyasa, kuwadhulumu na kuwafanyia vitendo viovu vijana wanaoendesha bodaboda.

Hivi karibuni, baadhi ya askari polisi waliokuwa wanasimamia ubomoaji vibanda kwenye kituo cha daladala cha Kimara Mwisho, waliliacha jukumu la ulinzi kwa waliokuwa wanabomoa, badala yake wakaanza kuwakamata na kuchukua rushwa baada ya kuwatisha kwamba walikuwa wanavunja sheria za barabarani!

Vitendo kama hivyo vipo kwenye maeneo tofauti ya nchi na ambavyo kama vikiandikwa vyote, si ukurasa huu pekee, bali gazeti zima halitatosha kwa kuviainisha.

Hivyo wakati serikali ikiibua mkakati wa kuwakagua bodaboda, isifumbe macho pale watakapojitokeza askari polisi wasiokuwa waadilifu, wakaugeuza kuwa mradi wa kujipatia rushwa kwa njia za vitisho dhidi ya vijana wasiokuwa na hatia.

Kuliacha jukumu maalum la kudhibiti uhalifu kama ujambazi na kuanza kuwashughulikia bodaboda wasiokuwa na hatia, lengo likiwa ni kujipatia kipato cha njia haramu, hakutalisaidia taifa kukabiliana na uovu huo.

Badala yake umma utashuhudia ongezeko la uporaji hasa wa fedha kwa watu wanaotoka benki, huku askari polisi waliopaswa kushiriki katika kudhibiti, wakiendelea na ukusanyaji mapato kwa njia haramu kutoka kwa bodaboda.

Kama hali hiyo itaachwa ijitokeze, iendelee na kuwa sehemu ya utendaji wa askari polisi, kuna hatari kwa vijana wa bodaboda wakachoka na badala ya kuwa wadau muhimu kwa polisi kudhibiti uhalifu na wahalifu, watashiriki kutofanikisha utekeleza wa mkakati huo.

Ni vizuri serikali ikaweka bayana namna itakavyowashughulikia askari polisi wasiokuwa waadilifu, wale ambao badala ya kuwafanya bodaboda kuwa rafiki wa mkakati wa kudhibiti uhalifu na wahalifu, watageuza kuwa wasaliti wa mkakati huo.

Kutokana na mazoea na hulka za askari polisi wasiokuwa waadilifu, si ajabu kuanza kwa utekelezaji wa mkakati wa kuwakagua na kuwahoji bodaboda kukafanyika kwa haraka kwa maana miongoni mwa wahusika, wanaweza kuwa wahusika wakuu wa kuchukua fedha kutoka kwa bodaboda.

Wanaweza kujikusanyia kiwango chochote cha fedha na ikibidi fungu zima la mapato lililopatikana kwa biashara ya siku nzima.

Ikiwa hali kama hiyo itatokea, bodaboda na raia wengine hasa wenye wito kama wao hawatakuwa rafiki wa vyombo vya ulinzi na usalama katika kuwadhibiti.

Ujambazi hauvumiliki wala haustahili heshima hivyo mkakati wowote wenye lengo la kuudhibiti unapaswa kuwa shirikishi na usiokuwa na hata chembe ya mianya ya rushwa.

Ni kwa nadharia hiyo, hata wanaoshiriki vitendo viovu vyenye kuathiri mkakati wa kudhibiti majambazi, hawaistahili heshima badala yake wanapaswa kushughulikiwa kwa ukali na haraka.

Kuwaacha askari polisi ama mwingine asiyekuwa muadilifu kutamba, kutakuwa ni kushindwa kwa mkakati wa serikali, hivyo nguvu kubwa itumike kuwadhibiti maofisa wa ulinzi na usalama watakaobainika kuwa sehemu ya kadhia hiyo.
Kama askari polisi wataweka mbele maslahi mapana ya umma na kuwatendea haki bodaboda, mkakati huo utafanikiwa na kuleta mafanikio yenye tija kwa nchi na watu wake.

Halitakuwa jambo la heri akatokea askari anayeshindwa kulitimiza jukumu hilo, akabaki kuwa kinara wa kuwanyanyasa bodaboda ikibidi kwa kuwabambikizia makosa wasiohusika nayo, ili mradi kuwepo mazingira bora ya kupewa rushwa.

Mashaka Mgeta ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii. Anapatikana katika simu namba +255 754 691540, 0716635612 ama barua pepe:mgeta2000@yahoo.com au mashaka.mgeta@guardian.co.tz.