Mfumo majitaka Mwenge Mlalakuwa una sababu zote za kufanyiwa kazi

10Jun 2022
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mfumo majitaka Mwenge Mlalakuwa una sababu zote za kufanyiwa kazi

NI kawaida kwa serikali zote duniani, kwamba huwa zinatafuta mbinu mpya za kugharimia kuziba mapengo ya ugharimiaji wa miundombinu yake, ili kuwezesha malengo ya maendeleo endelevu iliyo nayo.

Hapo inajulikana kwamba vyanzo vikuu vya mapato ya serikali duniani huwa ni kodi, sambamba na vyanzo kama misaada kwa baadhi ya serikali zenye uwezo wa chini.

Penye shida mbalimbali za mahitaji tajwa, ni bahati mbaya lingine hujitokeza kwamba hakuna mipango thabiti katika kupanga uwiano sahihi kati ya mahitaji na bajeti kiserikali na hilo hushuhudiwa sana katika ngazi ya serikali za mitaa.

Bajeti ya nchi hasa katika serikali za mitaa kuna mengi hujitokeza kuachwa nyuma mahitaji ya umma katika kukidhi vifaa vinavyohitajika kusimamia rasilimali za miundombinu katika kipindi chote cha mahitaji ya umma, iwe huduma za muda mfupi au za kudumu.

Katika mazingira ya utawala bora duniani kote, serikali za mitaa na serikali kuu, kila moja kwa nafasi yake inatakiwa kuimarisha usimamizi wa rasilimali za miundombinu pamoja na mwongozo wa namna ya kutumia zana hizo, katika mazingira ya changamoto ilizo nazo katika jamii, kiuchumi na kimazingira.

Hali ya kuzingatia umadhubuiti katika ‘upya na uimara’ wa rasilimali za zamani, mara nyingi kuna kusahaulika namna rasilimali mpya zinapojengwa, pale pasipo kuwekwa muundo wa usimamizi utakuwa wa uhakika, jumuishi na endelevu katika huduma muhimu, kunakuwepo kasoro. 
  
Nikirejea pale yalipo makazi yangu eneo la Mwenge - Mlalakuwa, wilaya ya Kinondoni jijini, Dar es Salaam, nashuhudia namna wazazi wanapata changamoto ya kupasuka kwa mifumo ya majitaka kwa muda mrefu na hapo kuna sababu kuu kwamba huo ni mfumo mkongwe, aina ya mazingira yanayokumbusha haja ya kuboreshwa mfumo wa majitaka kuwanusuru wakazi katika mazingira endelevu kwao. 
 
Daima panapokosekana suala la utunzaji miundombinu, kunatakiwa kujiweka katika mazingira magumu. Kuna wakati nadodosa takwimu za nchi nyinginezo na kubaini ni jambo linalogharimu wakati fulani hadi asilimia ya pato la ndani ya nchi, kuwekeza katika eneo la miundombinu ya mfumo wa maji safi na majitaka.

Pale penye miundombinu isiyotunzwa rasilimali zake, huwa kuna uwezekano mkubwa wa kushindwa kufanya kazi inavyopaswa, hata kukatisha huduma stahiki kwa umma na nyinginezo, ikiwamo kama usafiri, kupatikana majisafi na majitaka au usimamizi wa taka ngumu.

Kuna maeneo tunawaza kutumia uzoefu wake kujifunza. Suala la uahatarishi wake katika mazingira magumu kama penye mlipuko wa maradhi Uviko 19, ni suala muhimu sana kwa umma, ikiendana na madhara ya matatizo kama vile hali mbaya ya hewa au dharura za kiafya, mlipuko huwa na athari mara mbili zaidi. 
 
Wakati serikali inaendelea kuboresha miundombinu  katika eneo hilo, kuna njia muafaka ya kutatua changamoto za majitaka yanayosambaa mitaani katika maeneo wanayoishi watu na kuzalisha kero kubwa kwa umma jirani, hata kuhatarisha afya ya wakazi wa eneo na hasa watoto wanaocheza maeneo ya jirani na majitaka. Hili ndilo niseme linatusibu wakazi wa Mwenge - Mlalakuwa.
 
Nikiwa ni sehemu ya wakazi hao, nina upande wa pili wa shilingi, nikipongeza juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan, kujali umma kwa kuboresha huduma za miundombinu ya majitaka katika eneo hili.

Ili kuitikia wito wa Rais Samia, ni vyema wananchi kwa pamoja kuwa mstari wa mbele katika kushirikiana kuilinda miundombinu hiyo, ili iweze kudumu kwa muda mrefu na hivyo kuboresha maendeleo kwa ujumla wake. 
 
Matokeo yake serikali kuu na serikali za mitaa zinapaswa kutafuta rasilimali muhimu kama vile rasilimali za miundombinu ya umma, kwani ni msingi wa uchumi wa taifa na kushughulikia athari za kiuchumi na kijamii.