Mapumziko Ligi Kuu Bara yatumike kuboresha viwanja

02Jan 2023
Adam Fungamwango
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Mapumziko Ligi Kuu Bara yatumike kuboresha viwanja

LIGI Kuu Tanzania Bara itasimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya kila mwaka ya Kombe la Mapinduzi ambayo hufanyika mjini Zanzibar kwenye Uwanja wa Amaan.

Ni michuano mikongwe ambayo kilele chake huwa Januari 12, siku ambayo huadhimishwa Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika usiku wa tarehe hiyo na kumng'oa Sultan wa huko mwaka 1964.

Mara nyingi ni michuano ambayo huzishirikisha baadhi ya timu za Tanzania Bara, hususan Simba na Yanga na zingine ambazo huwa ni maarufu au zinazotoa ushindani kwa wakati husika, lakini baadhi ya timu za Zanzibar kushiriki pia.

Mwaka huu kutakuwa na makundi manne, ambapo Kundi A litakuwa na timu za Azam FC, Malindi SC, na Jamhuri, huku Kundi B likiwa na timu za Yanga, Singida Big Stars na KMKM.

Simba ambao ni mabingwa watetezi, wapo Kundi C, wakiwa pamoja na timu za Mlandege na KVZ, Namungo ikiwa Kundi D na timu ya Chipukizi na Aigle Noir ya Burundi, ambayo ndiyo timu pekee kutoka nje ya nchi iliyoalikwa msimu huu.

Tuanze kwa timu ambazo hazipo kwenye michuano hiyo, badala yake zitakuwa nyumbani zikifanya mazoezi kwa ajili ya kuzisubiri zingine, huu siyo muda wa kupumzika sana, au kulala. Nadhani mapumziko ya wiki moja tu yanatosha kabla ya kuwarejesha wachezaji mazoezini kwa sababu wenzao watakuwa wanaendelea kucheza, hivyo kuwaweka fiti wachezaji wao.

Na ikiwezekana baadhi ya timu zingekuwa zinatumia muda huu kucheza mechi za kirafiki ili kuwaweka wachezaji kwenye utimamu wa mwili.

Zikiona huu ndiyo wakati wa kupumzisha wachezaji wao itakula kwao, kwani wakati timu zilizotoka huko wachezaji wao wakiwa fiti, wao wanakuwa ni kama wanaanza upya. Kwa timu ambazo zinashiriki michuano hiyo, ni wakati wa kuwatumia baadhi ya wachezaji ambao hawapati namba kwenye vikosi vya kwanza.

Sisemi wapange wachezaji wote, hapana, nasema wawachanganye, kwani baadhi ya si kwamba viwango vyao vimeshuka, bali hawapati tu muda wa kucheza.

Hii si michuano ya kuleta wachezaji kutoka nje ya nchi na kuwajaribu. Msimu uliopita tuliona hata Simba na Yanga zilileta wachezaji kwa ajili ya majaribio. Kwa bahati nzuri au mbaya, hakuna hata mmoja aliyeridhishwa na wachezaji hao. Wote wakaachwa.

Simba na Yanga kwa sasa zinatajwa kuwa moja ya klabu zinazokuja juu kisoka Afrika, ni aibu leo kuokoteza wachezaji na kuwapeleka kuwajaribu.

Klabu hizi zimeshapita huko, zinatakiwa kusajili wachezaji ambao wanajulikana kuwa hawa ni wa viwango vya juu na kuingia moja kwa moja kucheza na si kujaribiwa kama gari lililotoka gereji.

Labda tunachotaka kuona huko ni wachezaji wapya waliosajiliwa kuanza kuonekana kwenye michuano hiyo na si wale wa mafungu na majaribio.

Kingine ni upande wa wamiliki wa viwanja na mameneja wao. Kwa muda huu wa wiki mbili mechi hazitochezwa, huu ndiyo wakati wa kuanza kufanya maboresho ili ligi ikirejea ionekana kama vile inaanza upya kutokana na ubora wa viwanja.

Viwanja vya Tanzania mara nyingi huonekana vizuri pale ligi inapoanza, ambapo vinakuwa vimefungwa kwa ajili ya marekebisho, lakini timu ya nyumbani ikicheza mechi tatu au nne, vinarudi kuwa vibovu.

Naipongeza Bodi ya Ligi nchini (TPLB), msimu huu kwani imekuwa ikihakikisha viwanja vinakuwa bora na imefungia vingi hadi pale vilipofanyiwa marekebisho bila upendeleo, wala kuoneana haya.

Na kweli msimu huu angalau viwanja vinatazamika, licha ya matatizo ya hapa na pale ambayo nimeyaainisha.

Ni kipindi ambacho mameneja ambao kila mwezi hushindanishwa ili kupata mshindi wa tuzo ya meneja bora, kuanza kushindana kumwagia maji ili kuziweka nyasi kwenye hali nzuri pamoja na maeneo mengine ili Kombe la Mapinduzi likiisha na timu kurejea tena, mashabiki wapate burudani kuelekea mwisho wa msimu wa ligi.

Hii inawezekana kwa sababu tumeona viwanja vilivyofungiwa, vilipofunguliwa kwa sababu ya maboresho na kwa sababu havikuwa vinachezewa mechi vinakuwa vizuri kiasi cha hata mashabiki wa soka kubishana kwenye TV kuwa huenda si viwanja vile ambavyo wanavifahamu.