Machinga watafakari, wachukue hatua kuboresha biashara zao

14Jan 2022
Sabato Kasika
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Machinga watafakari, wachukue hatua kuboresha biashara zao

WAFANYABIASHARA wadogo (Machinga) wameondolewa katika maeneo yasiyo rasmi, katika miji na majiji nchini, kama alivyoagiza Rais Samia Suluhu Hassan, ili wapangwe vizuri waweze kufanya biashara zao bila bugudha.

Dar es Salaam ni jiji mojawapo ambalo lilikuwa na machinga wengi, waliokuwa wakifanya biashara zao katika maeneo mbalimbali yasiyo rasmi, lakini wameondolewa na kupelekwa katika masoko.

Hata hivyo, badala ya kwenda kwenye masoko waliyotengewa baadhi yao wameibuka na mbinu za kujificha vichochoroni wakati wa asubuhi hadi saa 10 jioni, wanaibuka na kurudi kwenye maeneo waliyoondolewa.

Machinga hao ni wa Mbezi Mwisho, wakiwamo wale wenye meza zao, wafanyabiashara kwenye masoko mapya na wengine wanaodai kuwa hawana meza hizo, wote kwa pamoja wamekuwa wakitumia mbinu hiyo.

Kwa mtazamo wangu ni kwamba kupitia mbinu hiyo wanayotumia inaweza kuwakwamisha kupata wateja wa kutosha, pia kukosa sehemu ya kuuzia bidhaa zao na kubaki wakiwa watu wa kutangatanga huku na kule.

Kwanini? Kwa sababu baadhi yao wanakiri kuwa wana meza za biashara katika masoko mpya na huweka vitu vichache, ili waonekane wapo na kisha wanaondoka na kwenda kujibanza vichochoroni.

Wanapoteza muda mwingi wakisubiri ifike jioni warudi kwenye maeneo waliyoondolewa, pia kama wana meza za biashara katika masoko walikopelekwa, inawezekana meza hizo wakapewa wengine.

Kwa hali hiyo ni kwamba, muda wanaoutumia wakiwa mafichoni unapotea bure kwani wanaporudi katika maeneo ya awali, wanafanya biashara kwa saa chache giza linaingia wanaondoka kurudi nyumbani.

Hivyo, ingekuwa vyema kama wangetambua hilo kwamba wanaweza kukosa wateja kwani mbinu wanayotumia inaweza isiwe na faida na badala yake wakajikuta wakipata hasara zaidi au kukosa meza katika masoko.

Pamoja na hayo ni vyema pia wakasoma ishara za nyakati, kwani zama zimebadilika, yawezekana wanaamini kwamba, ipo siku watarejea kinyemela kwenye maeneo ya awali na kumbe sivyo.

Ikumbukwe kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla ameshatangaza kila Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi, itakuwa siku maalumu ya kufanya usafi kwa wakazi wa mkoa huo.

Ni katika uzinduzi wa mkakati wa usafi na hifadhi ya mazingira wa mkoa huo uliopewa jina la 'Safisha Pendezesha Dar es Salaam', uliofanyika hivi karibuni baada ya kumaliza kazi ya kuondoa machinga kwenye maeneo yasiyo rasmi.

Hivyo, badala ya kufanya biashara kwa kuvizia, njia nzuri ni wao kwenda kwenye masoko huku wakiendelea kudai kile ambacho kwa muda mrefu wamekuwa wakikitaka kutoka manispaa na halmashauri.

Miongoni mwa madai yao ya muda mrefu, ni kuboreshewa miundombinu ya masoko, ikiwamo upatikanaji huduma ya maji, choo, usafiri wa daladala hadi kwenye masoko hayo.

Kimsingi, wao ni watu muhimu ni suluhisho la mahitaji kwa jamii kuanzia yenye kipato cha chini, kati na kipato cha juu na wanatajwa kuchangia katika kukuza pato la taifa, hivyo ni vyema wasiendelee kuhangaika huku na kule.

Badala ya kutumia mtindo huo ambao unaweza kusababisha waendelee kufukuzana na serikali, ni bora wakitulia kwenye masoko yao ili waweze kukuza uchumi wao na hata wa taifa na kusaidia kuondoa umaskini.