Wengine wanasema ni mawazo au hisia ya kutoweza kukabiliana na mahitaji yatokanayo na kazi, uhusiano, shinikizo la kifedha na hali zingine kimaisha.
Mtu au binadamu akifikia hali hiyo, inatajwa kuwa hatari sana, kwani anaweza kufanya lolote kama kujidhuru au kumdhuru mwingine, hata kama hahusiki na mkasa wake.
Bungeni Dodoma, ilitangazwa serikali imekubali kupunguza tozo za miamala ya simu na ving'amuzi, baada ya kufanyika majadiliano na Kamati ya Bunge ya Bajeti.
Katika punguzo hilo, tozo ya ving'amuzi zimeshuka kutoka Sh.3, 000 hadi viwango kati ya Sh.500 na 2,000, tozo za miamala ya simu nazo zikishuka kutoka Sh. 10,000 hadi Sh.4, 000.
Ni uamuzi, unaobeba suala la kuweka kando sharti la lazima kwa kila Mtanzania mwenye umri miaka 18, akinunua au kuuza bidhaa ni lazima awe na namba ya mlipa kodi (TIN).
Tuna ushuhuda siku kadhaa, serikali ikisikiliza sana maoni ya wananchi wake, hivi karibuni ilitoa Sh. Bilioni 100 kwa ajili ya ruzuku, kupunguza bei ya mafuta nchini.
Pia, Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Mwigulu Nchemba, alipendekeza kufutwa ada kwa wanafunzi wa kidato cha sita, ikiendeleza kuwapunguzia wananchi gharama za maisha.
Naamini, bado serikali inaendelea na mipango mingine kuhakikisha mzigo haumuelemei mwananchi kwenye nyanja mbalimbali, ili kumboreshea maisha.
Niipongeze serikali kwa kuendelea kugusa sehemu zinazoonekana mwananchi anaumuia, hata kumuepushia msongo wa mawazo.
Ni hivi karibuni, kumekuwapo matukio mengi ya watu kujeruhiana au kuuana, hasa wanandoa, wapenzi, familia moja, mtu na baba yake au mtu na mama yake. Sababu nyingi zinatajwa, mojawapo ni msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa maisha.
Gharama za vitu mbalimbali na ugumu wa maisha zimekuwa zikisababisha hata matukio tunayoyaona na kuyashangaa, tukijiuliza “kwanini yameibuka kwa kasi hivi karibuni?”.
Ni kweli, hata zamani wanandoa wamegombana, pia kuwapo migogoro kwenye familia, lakini hakukuwapo sana ushuhuda wa mengi ya kikatili kama ya sasa, ingawaje kidunia, hakuna kinachofanyika sasa ambacho ni kigeni duniani.
Itikadi, sera na siasa ya Ujamaa, kila kitu kumilikiwa na umma, huku wananchi wakipata bure mahitaji yao kama elimu, afya, maji na mengine yanayofanana na hayo.
Ni hatua iliyowanyima msongo mkubwa wa mawazo kiasi cha kuchanganyikiwa na kufanya maamuzi ya ajabu anapoudhiwa, japo kidogo.
Pia, hakukuwapo mahitaji mengi kama sasa, ikizingatiwa, sasa kuna maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Mtu alitafuta pesa ya chakula, nguo, nauli na mahitaji mwengine machache. Dunia nayo imebadilika na haiwezekani kuishi kama ilivyokuwa zamani. Kama nchi nyingine zilivyobadilika, Tanzania haikuachwa nyuma kwa mabadiliko ya sera na maendeleo ya teknokojia.
Kwa maana hiyo, mtu anaamka, anatakiwa pesa ya chakula, nauli za watoto shuleni, ada, bili ya umeme, maji, pesa ya kupeleka watoto hospitali na madeni juu.
Kutokana na maendeleo ya teknolojia hasa ya simu za mkononi, anatakiwa kuwa na salio lake wakati mwingine na mkewe, ‘bando’ kwenye simu, ili dunia iwe kiganjani.
Pia, mtu anatakiwa kulipia ving'amuzi ili watoto waangalie katuni, familia iangalie filamu na tamthilia, yeye mwenyewe aangalie soka.
Ukichanganya vitu hivyo, kuna wakati vinamtoa jasho au kumshinda kutokana na tozo za kodi na ushuru kuwa juu, hivyo kumsababishia msongo wa mawazo kutokana na kushindwa kuzimudu.
Mtu kama huyu akiudhika, au kuudhiwa na mwenzake, hata akichanganya na ugumu wa maisha, anaweza kufanya chochote kile. Sababu kuu ni uhalisia ulioelezewa.
Nirudie tena kusema, serikali imefanya hivi kwa mapenzi na wananchi wake, pia itakuwa kwa kiasi kikubwa inawapunguzia wananchi wake msongo wa mawazo, kwani inawatua mzigo, maisha walau yawe na sura ya amani.



.jpg?itok=nfwjwDzv)








