Mchezo wa kandanda una matukio matatu: kushinda, sare ya mabao au suluhu ya kutofungana. Ndio maana katika kandanda, timu zinapotoka sare/suluhu huongezewa muda au kupigiana penalti ili kupata mshindi.
Oktoba mosi kulikuwa na mechi ya Ligi Kuu kati ya wapinzani/watani wa jadi jijini Dar es Salaam -- Simba na Yanga.
Hapana aliyeibuka na ushindi kwani mchezo ulimalizika kwa ‘sare’ ya kufungana 1-1. Simba ilisawazisha kwa mpira wa kona iliyopigwa na Kichuya na kwenda moja kwa moja kwenye kimia cha Yanga.
Msimu uliopita, Yanga iliifunga Simba mechi zote mbili kwa mabao mawili kila mechi. Kwa jinsi nilivyouona mpira wa msimu huu kati ya timu hizo, nathubutu kusema Simba ililipiza kisasi cha msimu uliopita.
Kwa nini nasema hivyo? Waamuzi walishindwa kuzitendea haki timu zote. Wao ndio chanzo cha machafuko yaliyotokea hata mashabiki wapumbavu wa Simba wakang’oa viti walivyokalia na kuvirusha chini! Ni kutokana na ‘bao’ la mkono lililofungwa na Amiss Tambwe wa Yanga dakika ya 26 ya mchezo.
Bao lile halikuwa halali kwa namna yoyote. Soma alivyoeleza Amiss Tambwe, mfungaji wa ‘bao’ lile alipohojiwa na gazeti maarufu la michezo, Mwana Spoti:
“ Nashangaa watu wanaosema nimefunga kwa mkono, si kweli. Mpira ulikuwa juu na nikiwa na mabeki wawili wa Simba, wote tuliruka juu kuwania mpira ulionigonga kifuani na wakati nageuka ukanigonga mkono kwa bahati mbaya …” Hiyo ‘bahati mbaya’ yake ndio kosa.
Soma kwa tafakuri paragrafu hiyo. Tambwe anakataa kisha anakubali! Ni wazi kuwa mpira ulimgonga mkono ndipo alipopata nafasi ya kuwatoka mabeki wa Simba na kufunga. Simba wataachaje kusema Yanga inabebwa?
Kabla ya tukio hilo, Ibrahim Ajib wa Simba alifunga bao, lakini mwamuzi wa pembeni akanyoosha kibendera kuashiria alikuwa ‘kazidi’ (offside). Hapana bwana. Ajib alikuwa mbele ya mabeki wawili wa Yanga. Aliotea vipi? Lilikuwa bao halali.
Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika, Simba ingekuwa mbele kwa bao la Ajib kama si kibendera cha mwamuzi wa pembeni kunyanyuliwa juu kuashiria Ajib ‘aliotea!’
Kipindi cha pili Simba walibadilika katika uchezaji huku Yanga wakidhani wamekwisha shinda. Wakawa wanacheza kwa kutega na kuwapa mwanya Simba watulie.
Jonas Mkude, nahodha wa Simba alipotolewa n-nje ya uwanja, wachezaji wenzie hawakukata tamaa bali walicheza kwa ari ingawa walikuwa pungufu. Yanga walishindwa kuitumia nafasi hiyo. Wakidhani wameshinda, kijana Shiza Kichuya akaifungia Simba bao.
Mpira wa kona ulijaa kimiani bila kuguswa na mabeki wawili wa Yanga waliokuwa nyuma ya kipa wao, Ally Mustafa. Ni uzembe wa kipa na mabeki wake wawili waliokuwa wamejipanga golini!
Kwa maoni yangu, Simba walikuwa washindi kwa mabao 2-0 kulipiza kisasi cha msimu uliopita. Tukubali tunaposhindwa badala ya kulalama!
[email protected]
0715/0784 33 40 96