Isipokuwasha (pilipili) hujairamba

23Feb 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Tujifunze Kiswahili
Isipokuwasha (pilipili) hujairamba

PILIPILI haiwezi kukuwasha kama hujaionja. Hii ni methali iwezayo kutumiwa kwa mtu anayeelekezwa jambo asilolifahamu vizuri kisha akawa m-bishi.

Ni kama natwanga maji kwenye kinu. Ninayoandika katika safu hii kila Jumanne kuhusu matumizi sahihi ya maneno ya Kiswahili yanapuuzwa na waandishi wabobezi wa maneno ‘mapya’ ya mitaani.

Baadhi ya waandishi hutumia maneno mengi yasiyo muhimu katika sentensi ambazo ama huwachosha wasomaji au hupoteza maana iliyokusudiwa. Hebu tuone sentensi mbili zifuatazo: Moja:

“Mkazi huyo mwenye ujauzito (huo) wa miezi mitano, alifanyiwa unyama (huo) Jumapili iliyopita na kulazwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC.” Maneno niliyoyaweka kwenye mabano ( …) hayakuwa na umuhimu wowote.

Ingeandikwa: “Mkazi huyo mwenye ujauzito wa miezi mitano, alifanyiwa unyama Jumapili iliyopita na kulazwa hospitali ya rufaa ya KCMC.” Mbili: “Kwa mujibu wa baadhi ya wauguzi wa KCMC, mjamzito (huo) alifikishwa hospitalini (hapo) juzi akitokea Hospitali ya Kilema alikokuwa amelazwa tangu Jumanne.

” Nimeondoa maneno ‘huo’ na ‘hapo’ niliyoyaweka kwenye mabano (…). Ingeandikwa: “Kwa mujibu wa baadhi ya wauguzi wa KCMC, mjamzito alifikishwa hospitalini juzi akitokea hospitali ya Kilema alikolazwa tangu Jumanne.”

“Kuelekea mchezo wa Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, Simba itaingia dimbani kumenyana na Yanga ikiwa ni deni la kulipa mabao 14, inayodaiwa na watani (zao) (hao) wa jadi.”

‘Watani’ ni wingi wa ‘mtani.’ Husemwa ‘mtani’ wa- [a- /wa] ni mtu aghalabu wa kabila tofauti au rafiki mkubwa ambaye ameruhusiwa kumdhihaki mwingine kwa mujibu wa mila zao pasi na aliyetaniwa kukasirika. Wingi wao ni ‘watani.’ “Hivyo basi, Simba itaingia katika mchezo huo ikiwa na deni la kupitwa idadi ya mabao 14 na mpinzani wake, Yanga, mwenye mabao hayo 103 dhidi ya 91 kati ya mabao 194 waliyofungana.” (maneno 32).

Sentensi hii imevurugwa kiasi cha kupoteza maudhui (wazo kuu linaloelezwa katika kazi ya fasihi; wazo linaloelezwa katika maandishi au katika kusema). Ingeandikwa: “Simba itaingia mchezoni ikiwa imepitwa na Yanga kwa mabao 14.

Kati ya mabao 194 waliyofungana, Yanga imeifunga Simba mabao 103 ilhali Simba ikiifunga Yanga mabao 91.” (maneno 26).

Maelezo hayo yapo kwenye aya (fungu la maneno lenye maana kamili; paragrafu) ya pili lakini mwandishi ameyarudia tena kwenye aya ya tatu! Kuanza sentensi na neno ‘lakini’ ni tatizo la waandishi wengi. Kadhalika kutojua matumizi ya herufi kubwa kama ilivyo sentensi ifuatayo. “Lakini pia, imemzidi Simba michezo saba ya kushinda katika michezo 35 waliyoshinda Watoto hao wa Jangwani dhidi ya 28 ya Simba.

” Maneno yaliyoharibu sentensi ni ‘lakini’, ‘imemzidi Simba’ na kuandika watoto kwa herufi kubwa – Watoto. ‘Lakini’ ni neno linaloonesha kuwepo upungufu, kasoro au hitilafu; isipokuwa, ila. Badala ya ‘imemzidi Simba’, ingeandikwa ‘imeizidi Simba.’ Neno ‘watoto’ ni la 13 katika sentensi ya maneno 21 lakini mwandishi kalianza kwa herufi kubwa ‘Watoto.’

Haelewi matumizi ya herufi kubwa! “Mvuvi akiandaa nyavu yake kabla ya kuingia majini kuvua samaki katika Bahari ya Hindi eneo la Kunduchi, Dar es Salaam.” ‘Nyavu’ ni wingi wa ‘wavu.’ Inaposemwa ‘nyavu’ (wingi) neno linalofuatia ni zake (wingi).

Ni muhali (lenye ugumu au kutowezekana kuwa) kusema ‘nyavu yake’ kwani kwa Kiswahili fasaha ni ‘nyavu zake.’ Kwa hiyo mvuvi alikuwa akiandaa ‘wavu wake.’ Jambo lililotendeka jana au juzi katika kulieleza ni tofauti na jambo linalotendeka leo au kesho.

Kuna wakati uliopita, uliopo na ujao. Mwandishi wa gazeti makini aliandika: “Mahakama ya rufani jana imeanza…” Isemwapo ‘imeanza’ maana yake ni wakati uliopo; leo.

Wakati uliopita husemwa ‘ilianza’ na wakati ujao ‘itaanza.’ Ingeandikwa: “Mahakama ya rufani jana (wakati uliopita) ‘ilianza…” “Naiagiza wizara kufanya mawasiliano naye hili aanze mara moja,” alisema Majaliwa. Neno ‘hili’ limetumiwa vibaya katika sentensi hii.

‘Hili’ ni kiwakilishi kioneshi cha umoja, ngeli ya li/ya; kivumishi kioneshi kinachoashiria ukaribu wa kinachorejelewa na mzungumzaji. Neno sahihi ni ‘ili’ lenye maana ya ‘kwa lengo la’, ‘kwa sababu ya’, ‘kwa madhumuni ya’ na ‘kwa ajili ya.’ Kwa hiyo ingeandikwa:

“Naiagiza wizara iwasiliane naye ili aanze mara moja.” Methali: “Atangazaye mirimo si mwana wa liwali.”

 

Yawezekana tangazo muhimu likatolewa na mtu asiye na cheo kikubwa lakini hatupaswi kumdharau. marobarnabas@yahoo.com 0715/0784 33 40 96