Elimu pekee haitaondoa kipindupindu

01Mar 2016
Restuta James
Nipashe
Mjadala
Elimu pekee haitaondoa kipindupindu

RIPOTI mbalimbali zinaonyesha kuwa watu milioni 18 nchini hawana uwezo wa kupata maji safi. Ripoti nitakayozirejea hapa leo ni ile ya hali ya haki za wanawake iliyotolewa na Shirika la Wanawake na Maendeleo Afrika (Wildaf), mwaka jana.

Pamoja na mambo mengine, ripoti hiyo ilieleza kuwa karibu nusu ya Watanzania wote yaani watu 18 hawapati maji safi; katika nchi ambayo inautitiri wa vyanzo vya maji.

Ripoti ilifafanua kuwa waathiriwa wakubwa wa tatizo la maji ni wanawake na watoto ambao wamekuwa wakitumia muda mwingi na kutembea umbali mrefu kutafuta maji badala ya kujisomea au kufanya shughuli za maendeleo.

Kwamba katika Tanzania yenye Ziwa Victoria, Tanganyika, Rukwa, Nyasa, milima na mabonde, kuna watu wanaotembea saa nane kutafuta maji ambayo hata hivyo siyo safi.

Mwanamke anayetafuta maji, anatakiwa kufanya shughuli nyingine za nyumbani kama usafi wa nyumba na mazingira yanayomzunguka, atazifanya wakati gani ikiwa saa nane zimeshapotelea kwenye maji?

Je, ndoo moja ya maji aliyoitafuta kwa saa nane, atakunywa, kuogea, kufulia, kuoshea vyombo au kupikia?
Wakati nikijiuliza maswali haya, nimekutana na ripoti nyingine ya shirika la Water Aid ikieleza kuwa chini ya asilimia 50 ya watu hapa nchini hawana vyoo. Kwa hesabu zisizo rasmi ni kwamba takribani watu milioni 20 hawana vyoo; nusu karne baada ya Uhuru.

Hili ni tatizo kubwa kiafya hasa kwa makazi yasiyopimwa na ripoti hiyo inaeleza kuwa athari mojawapo ni kwamba ukosefu wa vyoo unasababisha vifo vya watoto 7,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano kila mwaka kutokana na magonjwa ya kuhara yanayozuilika.

Kwamba tatizo hilo linaathari pana zaidi hadi kwenye elimu ambako watoto hawawezi kufanya vizuri kutokana na maradhi ya mara kwa mara.

Wakati watafiti wakieleza hayo, kila mara kumekuwa na ripoti zinazoonyesha kuwa shule kadha wa kadha hazina vyoo na katika baadhi ya maeneo, wanatafutwa wafadhili wa kusaidia ujenzi wa vyoo ili kuboresha mazingira ya shule!
Nimelazimika kueleza haya kwa kuwa ugonjwa wa kipindupindu umekuwa ukilipuka mara kwa mara kwenye mikoa karibu yote mijini na vijijini.

Kwa ripoti za mashirika nilizotaja hapo juu, elimu ya kunawa mikono na sabuni pamoja na usafi wa mazingira, haitaondoa kipindupindu.

Kinachotakiwa ni maji, siyo elimu wala kuhamasishana. Nasema hivi kwa sababu ikiwa mtu atahamasishwa kufanya usafi, akimaliza atanawa na maji gani wakati hayapo?

Huyu mama ambaye ametumia siku nzima kwenda kusaka maji utamwambia ‘ayachezee’ kwa kunawa kila wakati anapokwenda kujisaidia ‘vichakani’ wakati kinyesi chake kitamfuata hata kama angenawa?

Tatizo la kipindupindu ni zaidi ya linavyotazamwa. Serikali inapaswa kutenga bajeti ya kutosha kuhakikisha maji safi yanapatikana kwa urahisi; hapo ndipo ianze kuhamasisha suala la usafi wa mtu binafsi na wa mazingira yake.

Pia, lazima kila kiongozi kuanzia wa kijiji au mtaa hadi Taifa, wahamasishe ujenzi wa vyoo ili kuzuia uchafunzi wa mazingira.

Uhakika wa upatikanaji wa maji safi na vyoo bora itakuwa tiba mahsusi ya ugonjwa wa kipindupindu.
Mungu Ibariki Tanzania.