Dawasa, Dawasco maji yaliyoongezeka yako wapi?

03Apr 2016
Nipashe Jumapili
Nawaza kwa Sauti
Dawasa, Dawasco maji yaliyoongezeka yako wapi?

HIVI karibuni Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasa), ilitangaza ongezeko la maji na kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ikiwamo kutoa taarifa iwapo wataona bomba lilopasuka.

Ongezeko hilo linaelezwa kuwa ni la juu baada ya kukamilika kwa miradi ya upanuzi katika vyanzo vya Ruvu Chini na Ruvu Juu ambavyo vinalisha maji wateja wa jiji la Dar es Salaam na Kibaha.

Naipongeza serikali kwa kuanzisha miradi hiyo ambayo sasa inaelekea kukamilika na kuliwezesha jiji kuwa na maji, kwa sasa katika maeneo yaliyokuwa yakipata kiasi kidogo ambayo hayakuweza kupanda kwenye bomba za ndani sasa wanafungua maji bafuni na jikoni na mengine yanakusanyika kwenye matangi ya akiba.

Hakuna ubishi kuwa ukosefu wa maji jijini umewafanya watu kuwaza kuwa maji ni na anasa kwani yamewagawa wakazi wake katika makundi mawili, lile lenye haki ya kupata huduma hiyo na lisilo na haki na kuishia kutumia maji safi na salama ya bomba na wale wanaokula ya visima vifupi na virefu.

Ukilinganisha idadi ya wateja na huduma ya majisafi inayotolewa ni wachache huku wengi wakitumia maji yasiyofaa ambayo huwasababishia maradhi kama upele, maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), kuhara na kipindupindu.

Wakati hali ikiwa hivyo wapo wanaotajirika kwa kuuza maji ya bomba ambao wamepewa vibali na Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco), huku wananchi ambao walitakiwa kupata huduma hiyo wakitaabika, jambo ambalo linazua maswali mengi.

Yapo maeneo ya jiji suala ya majisafi wanalisikia kwenye vyombo vya habari kwani maisha yao yote wanatumia ya chumvi ikiwa ni kunywa , kuoga , kufua na usafi wa ndani licha ya kwamba walitakiwa kupata majisafi.

Wakati wa kampeni Rais John Magufuli, aliahidi kuwa atahakikisha huduma ya majisafi inapatikana jijini kwa kila kaya kupata huduma hiyo kutokana na ongezeko kubwa la maji.

Suala la majisafi liliwahi kusababisha bajeti ya Wizara ya Maji kukwama bungeni mwaka jana , baada ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, kuwasilisha hoja kueleza jinsi ambavyo serikali imeshindwa kujipanga kutatua tatizo la huduma hiyo jijini, na kutakiwa kuirekebisha ili kuwasilisha bajeti ambayo itaeleza jinsi gani tatizo hilo lingetatuliwa.

Kwa sasa haitoshi Dawasa kutueleza kuwa maji yameongezeka, ni taarifa za matumaini lakini ongezeko hilo halina maana iwapo wanaofaidi huduma hiyo ni wale wale, kwa maana kwa sasa hawayafuati nje ya nyumba zao kwani yameingizwa ndani moja kwa moja.

Tunachotaka kuona ni upanuzi wa miundombinu ya maji ili maji hayo mengi yawafikie wananchi wengi zaidi, watu wamechoka kusikia huduma ya majisafi kuwa ni anasa inayonufaisha wachache ambao ni sehemu ndogo ya wateja wa maji. Lakini pia wanakerwa kusikia matangazo ya Mama Tua Ndoo, huyo mama anaiondoaje kichwani wakati hamjaweza kumletea maji jirani au ndani ya nyumba yake?

Ni vyema sasa tukaona kasi ya kutandaza na kupanua mtandao wa maji kutoka maeneo machache mliyokuwa mnayahudumia hadi kufikia sehemu kubwa ya wakazi, kuna miji mipya kama Goba, Makongo, Mwanagata, Kibeberu na Kitunda kote huko hakuna maji wananchi wanataka kuona mtandao wa usambazaji.

Zipo sehemu nyingi za Mbagala , Mtoni na Temeke ambako walikuwa wanategemea pamp za mtoni nao wanategemea ongezeko liwasaidie.

Licha ya kwamba watategemea maji ya visima vya Kimbiji na Mpera lakini kinachosubiriwa ni kuona kazi ya hiyo ikienda sambamba na kuchunguza wauza maji wanavyoyapata kwani wapo baadhi wanayaiba kiujanja na kuyauza kwa bei kubwa na kibaya hawalipi kodi licha ya kupata faida kubwa.

Isitoshe kutangaza kuwa kuanzia sasa maji yapo ya kutosha au Mama Tua Ndoo wakati mwananchi anayesikia hivyo hayaoni hata kwa jirani ni kitendawili ambacho hakijapata mteguzi.

Ni aibu kwa jiji hili kukosa huduma ya uhakika ya majisafi na wananchi kutumia maji yasiyo safi tena yanayochanganyikana na taka za vyooni (kinyesi) kwani yapo maeneo kisima kifupi cha mita chache kutoka chooni.

Haitoshi kusema maji yameongezeka bali itafaa kusikia yanasambazwa kwa wananchi na inaonekana kweli kwa vitendo yanasambaa na kupatikana kwenye mabomba hiyo ni huduma ya kijamii ambayo inapaswa kumfikia kila mmoja bila ubaguzi na siyo watu fulani wenye kipato kikubwa ambao wanaonekana ndiyo wenye haki ya maji safi na salama.

Tunaiomba serikali kusimamia hili kwa karibu na kwenda na kasi ya Rais John Magufuli ambaye tangu kwenye kampeni alisema hawezi kuwa na Waziri wa Maji halafu wananchi hawana maji, ni wakati sasa wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Greyson Lwenge, kuwajibika kikamilifu na kuonyesha mfano katika hili.

Majisafi yakipatikana ya kutosha yatasaidia kuepusha maradhi ya ngozi, tumbo kama kuhara na kipindupindi kwani watu wataacha kunywa maji machafu na kutumia yaliyo safi na salama.

Kwa sasa kuwe na kasi ya kusambaza na kukarabati miundombinu ya maji ili yanayopatikana yatumike kuhudumia wananchi kwa uhakika zaidi, ili Dawasa na Dawasco wanaposimama mbele ya umma na kueleza ongezeko la maji wateja wawaaelewe kikamilifu.
Mungu ibariki Tanzania
Mungu ibariki Afrika
Kwa maoni salome.kitomari@guardian.co.tz