Baadhi ya watu wametumia mwanya wa kutopita magari ya taka kwenye maeneo yao, kwa kuamua kuzikusanya na huzitupa barabarani, wakiamini kufanya hivyo ndiyo suluhisho la kuwaamsha wenye wajibu wa kuzitoa.
Tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli, alipotangaza usafi wa mazingira, Desemba 9, mwaka jana, wananchi wengi wamehamasika na baadhi kutangaza kila mwisho wa wiki, na mwisho wa mwezi kuwa ni siku ya kufanya usafi.
Hata hivyo, changamoto inayojitokeza katika hamasa hiyo ni uzoaji wa taka baada ya kusokesana kwa vifaa vya kutosha vya kuondoa uchafu huo.
Yalitolewa pia maagizo na viongozi ya kukamatwa kwa watu wanatakaobainika kuchafua mazingira kwa kutupa uchafu hovyo, ambayo faini yake ni Sh. 50,000 au kwenda jela.
Hata hivyo utekelezaji wa amri hizo unaonekana kugonga mwamba kwa sababu hata hivyo vifaa vya kutupia taka havionekani kuwekwa barabarani.
Magari ya abiria yanayofanya safari za mjini yaliagizwa pia kuwekwa vikapu vya kutupia taka ili abiria wasitupe uchafu hovyo, lakini ni machache yaliyotekeleza agizo hilo. Agizo hilo limeonekana kutekelezwa zaidi na mabasi yanayofanya safari za mikoani.
Kuna baadhi ya maeneo yameelemewa na taka za tangu Desemba 9, mwaka jana, zikiwa bado hazijazolewa kwa sababu mpaka leo hakuna magari yanayopita kuziondoa.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi sasa wameamua kuondoa mrundikano wa taka hizo kwenye maeneo yao na kwenda kuzirundika katikati ya barabara.
Taka hizo zinatupwa eneo la barabara ambalo limetengwa kwa ajili ya kupanda miti au majani na sasa kugeuzwa dampo la viroba vya uchafu.
Wameona hiyo ndiyo njia itakayowafanya wahusika kushituka. Ingawa njia hiyo inayotumiwa si sahihi kwa sababu licha ya kuchafua mazingira, lakini pia inaharibu mandhari ya barabara.
Katika baadhi ya barabara mrundikano wa viroba vya uchafu unaweza kuachwa muda mrefu bila kuzolewa, lakini wahusika hufanya juhudi ya kutafuta magari haraka ya kuziondoa ili kuondoa aibu hiyo.
Mpaka wananchi wanaamua kutumia njia hiyo, inaonyesha jinsi gani juhudi zinazofanywa na wananchi kuhakikisha maeneo yao yanakuwa safi, zinavyo vunjwa moyo.
Hata hivyo, mitaa inayoonekana kupitiwa na magari yanayozoa taka ni ile wanayoishi watu wenye kipato fulani, huku wananchi wenye kipato cha chini wakiendelea kuishi na marundo ya uchafu kwenye maeneo yao.
Katika baadhi ya mitaa, viongozi walijaribu kuweka utaratibu wa wananchi wao kuchangia fedha kila mwezi ili kupata huduma ya kuzolewa taka, lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda.
Ingawa katika baadhi ya mitaa, magari hayo yalianza kazi hiyo, lakini kutokana uchakavu wa magari yenyewe, hayakuweza kumudu kazi hiyo na matokeo yake hali ikabaki vile vile.
Hakuna mtu anayependa kuishi na uchafu nyumbani kwake au kwenye mazingira yanayomzunguka, hata hivyo, ukosefu wa vitendea kazi vya kuondokana na mazingira hayo, unasababisha maeneo mengi kuendelea kubaki na uchafu.
Kuna umuhimu wa utekelezaji wa sheria zilizowekwa ili kudhibiti watu wenye tabia zinazoenda kinyume na sheria hizo. Hili linawezekana kama kutakuwa na ufuataliaji makini.
Kwa wale wanaopita barabara ya Bagamoyo, eneo la jeshini, wanaweza kuona tofuati kubwa na barabara zingine.
Kipande cha barabara hiyo kinachoanzia Mwenge hadi njiapanda ya Kawe ni mfano mzuri wa kuigwa, kutokana na mandhari nzuri iliyotengenezwa na wanajeshi wanaotunza bustani ya kipande hicho.
Katika bustani hiyo ya barabara, mtu yeyote anayethubutu kutupa hata kipisi cha sigara, atakiona kilichomtoa kanga manyoa. Mtu anaweza akapewa adhabu ya kumwagilia maua kwa kutumia kijiko cha kulia chakula.
Kwa kuwa watu wanaelewa adhabu yake, bustani ya kipande hicho cha barabara huheshimiwa kama vile mtu anavyomheshimu mkwe wake. Watu wamekuwa makini kwa kutotupa hata karatasi ya pipi.
Abiria wa daladala wanapopita eneo hilo, hasa wale wanaopenda kutafuna mahindi ya kuchoma, hukumbushwa na abiria wenzao kutotupa maganda kwa sababu wameshajua, kosa la mtu mmoja wanaweza kuadhibiwa abiria wote.
Kama barabara zote za miji yetu zingepandwa maua kama kipande hicho cha Lugalo badala ya kugeuza dampo, tungekuwa mbali katika suala la usafi.
Hata hivyo, bila kujijengea utaratibu wa kufuata sheria na kuzitekeleza, tutaendelea kuona barabara nyingi kwenye miji yetu ikigeuzwa dampo.
bbandawe@hotmail.com, Simu: 0774 466571
mwisho



.jpg?itok=nfwjwDzv)








