Programu ya kupanda miti kuanza mwezi huu

04Jan 2016
Nipashe
Programu ya kupanda miti kuanza mwezi huu

Program ya kitaifa ya kupanda na kutunza mazingira inaanza mwezi huu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba (kulia), akifafanua jambo alipokuwa akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.

Hayo yalitangazwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe, jijini Dar es Salaam jana wakati wa kikao cha pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), January Makamba.

Profesa Maghembe alieleza kuwa Tanzania imetenga maeneo makubwa ya hifadhi ya misitu na mazingira ili kuhifadhi na kuongeza kuwango cha maji nchini.

Aidha, Profesa Maghembe alieleza umuhimu wa miti na misitu katika kuhifadhi maji na umuhimu wa maji kwa viumbe hai.

"Maji katika uasilia wake huvifikishia viumbe hai vyote madini na ili kupata afya na ustawi kwa njia kupitia viiini au seli. Maeneo makubwa haya ya hifadhi ya misitu na mazingira yametengwa ili yasaidie kupata hewa nzuri kwa afya yetu, maji, mvua, kuzuia joto kupanda na kupambana na mabadiliko ya nchi kugeuka jangwa,” alisema.

Alisema kumekuwa na ukataji mkubwa wa miti na uharibifu wa mazingira nchini na kueleza kwamba programu hiyo inalenga kuwa na mazingira bora (ecosystem), upandaji miti na utunzaji wake.

Waziri Profesa Maghembe alisema kikao cha cha mawaziri husika cha kuweka mkakati ya kutekeleza kampeni hiyo ya upandaji miti na utunzazi mazingira cha siku mbili, kitaanza Januari 16, mwaka huu na wataalam wa wizara mbili husika tayari wameagiza kuandaa kwa pamoja mkakati utakaotumika kutekeleza programu hiyo.

Mkutano wa pamoja utazingatia masuala yote ya upatikanaji wa rasilimali zitokanazo na faida ya misitu na mazingira.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Muungano), Makamba alisema suala la mazingira linagusa shughuli za wizara zote na taasisi nyingi na sekta binafsi na kueleza kuwa kuna kila sababu ya vyombo mbalimbali kushirikiana.

Alisema programu hiyo ya kitaifa ni ya aina yake nchini na katika utaratibu huo, Tamisemi itawashirikisha wananchi ili kila mmoja ajivunie kupanda miti katika eneo lake.

Waziri Makamba alisema matarajio ya wizara hizo ni kwamba kwa kutumia progamu hiyo baada ya miaka mitano matokeo yake juu ya uhifadhi wa mazingira na misitu yawe yanaonekana yenyewe pasipo kusemewa na kutetewa na mtu yeyote.

“Tukitekeleza programu hii kwa uangalifu na kufanikiwa, matunda yake yatavutia watu wote wa ndani na nje ya nchi kwa faida ya taifa letu,” alisema Makamba.