Kuengua wagombea sio afya kwenye demokrasia

22Sep 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Kuengua wagombea sio afya kwenye demokrasia

AGOSTI 23, mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan, wakati akipokea taarifa ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka jana, aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuangalia sheria za uchaguzi ili zisitumike kuwanyima wagombea haki wakati wa uchaguzi.

Alisema masuala ya kiufundi, mathalani pale mtu anapokosea kuandika herufu za jina lake au za chama chake yasitumike kumnyima haki ya kushiriki uchaguzi.

Agizo hilo lilionekana kushusha pumzi kwa upinzani kwa kuwa walishangilia sana kama namna ya kufikisha ujumbe wa kilio chao cha muda mrefu, kwa kuwa katika uchaguzi huo na uchaguzi mbalimbali kabla ya hapo ukiwamo wa serikali za mitaa mwaka 2019 wengi walienguliwa kwa sababu hizo hizo, hivyo kuwaacha wa chama tawala (CCM) pekee wakipita bila kupingwa.

Umepita mwezi mmoja, wagombea 10 wa vyama vya upinzani walioomba ridhaa ya kugombea udiwani Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga, wameenguliwa kwa madai ya kukosa sifa kwa kuwa kwenye fomu zao zilikuwa na kasoro.

Imeelezwa kuwa mgombea pekee wa CCM ndiye aliyepitishwa kwa kuwa fomu yake haikuwa na kasoro yoyote na alitimiza vigezo vyote muhimu.

Tunafahamu kuwa maagizo ya Rais ni sheria na watendaji wa taasisi zote wanapaswa kuitekeleza. Hata hivyo, inashangaza kusikia katika hili bado mamlaka husika hususani NEC yenye jukumu la kusimamia uchaguzi kutochukua hatua za utekelezaji wa agizo la Rais la kuacha kuengua wagombea wa upinzani kwa sababu zile zile, huku mgombea wa chama kimoja akiachwa kwa sababu zile zile zilizotumika kwenye chaguzi nyingine.

Kimsingi, jambo hili halina taswira nzuri kwa jamii ndani na kimataifa kwa kuwa linazuia ushindani ulio sawa kwenye demokrasia, kwamba siku zote wanaokosea ni wa vyama vya upinzani ila wasiokosea ni wagombea wa chama tawala!

Matukio haya yanaweza kuendeleza malalamiko yasiyo ya lazima ya baadhi ya watu kwenye jamii kuwa NEC haiko huru, kwa kuwa wasimamizi wa uchaguzi ambao ni wateule wa Rais, wanaegemea upande mmoja na kusahau wajibu wao wa kutengeneza mazingira ya ushindani kwa vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa kwa mujibu wa sheria.

Malalamiko ya wagombea wa upinzani kuenguliwa ni ya muda mrefu na hutokea kwao kwa kuelezwa na wasimamizi wa uchaguzi kwamba  fomu zao zimechelewa au zina kasoro mbalimbali  zinazowafanya wakose sifa ya kuruhusiwa kugombea nafasi husika.

Jambo hili likitazamwa na sura tofauti tofauti linaweza kuonyesha kuwa huenda vyama haviwaandai wagombea wake na kuwaelekeza namna ya kujaza fomu, lakini kwanini kila wakati ni upinzani tu?

Tunaona kwamba makamishna na watendaji wa NEC wanawajibika sasa kuhakikisha kwamba maagizo ya Rais Samia yanatekelezwa ipasavyo, vinginevyo hali hiyo inaweza kutafsiriwa vibaya na umma.

Kuacha hivi kunaweza kusababisha wadau wa uchaguzi na umma kwa ujumla kupoteza imani kwa NEC na matokeo yake kupunguza idadi ya wapigakura, kuongeza malalamiko ya wapinzani na kutengeneza mazingira kuwa wao hawatendewi haki.

Ni muhimu sana wasimamizi wa uchaguzi wakatambua kuwa wanapaswa kufanyakazi kwa mazingira yenye uwanja sawa wa ushindani kuliko kumtengenezea mmojawapo mazingira ya ushindi kabla ya uchaguzi kufanyika, kwa kuwa ikiwa wote wameenguliwa maana yake aliyebaki anatangazwa kuwa mshindi.

Ni muhimu maswali magumu yawe na majibu sahihi na kusiwe na majibu rahisi kwa maswali magumu, kwa kuwa jamii ya sasa siyo ya miaka ya 60, bali inauelewa wa kuchanganua, kupima na kufanya maamuzi sahihi kwa kile wanachoona ni sahihi.

Ni muhimu NEC ikafanyia kazi maagizo ya Rais kwa kuwa kama mwanasiasa na mkuu wa nchi ameona kasoro ilipo na inapaswa kurekebishwa ili kutenda haki kwa wote, na vyama kutimiza wajibu wao kuondoa malalamiko yasiyo ya lazima.