Mabadiliko Halmashauri Jiji Dar yaje na ubunifu

26Feb 2021
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Mabadiliko Halmashauri Jiji Dar yaje na ubunifu

RAIS John Magufuli juzi alitangaza kuivunja Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi Manispaa ya Ilala kuwa Halmashauri mpya ya Jiji la Dar es Salaam.

Tunaipongeza Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji, na hiyo ni hatua nzuri ambayo hata viongozi wenyewe na wakazi wa halmashauri hiyo watakuwa wameifurahia, lakini sasa hawanabudi kuongeza kasi katika utendaji wao.

Pamoja na kufurahia kupata hadhi hiyo adhimu, tuwakumbushe kuwa halmashuari ndiyo kitovu cha maendeleo ya wananchi, hivyo suala la ukusanyaji wa mapato kwa ajili ya huduma za jamii ikiwamo afya, elimu na nyingine ni la muhimu na kipaumbele.

Kwa maana hiyo, ukusanyaji mapato pia unahitaji kuchukukuliwa kwa umakini kwa kutumia sheria zilizopo na ndogondogo za halmashauri ili kuepuka kusababisha madhara kwa watu. Angalizo letu kwa madiwani ni kusimamia utekelezaji likiwamo suala la ukusanyaji wa mapato badala ya kujikita kwenye vikao tu na kugawana posho na kusahau maendeleo.

Dar es Salaam iilikuwa na manispaa tano, lakini Ilala imechaguliwa kuwa jiji, hiyo ni heshima ambayo Ilala yenyewe inatakiwa kuilinda, kwa kuongeza kasi, ubunifu wa miradi ya maendeleo, ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma kwa wananchi kwa tija na ufanisi.

Halmashauri hiyo ijipange kuweka mipango madhubuti na endelevu ambayo itaiwezesha kuendelea kukusanya mapato mengi zaidi ili kuiwezesha kutoa huduma mbalimbali zikiwamo za kijamii.

Tunaamini kwamba Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji si kwa bahati mbaya, bali imekidhi vigezo vyote hususani makusanyo ya mapato kama Rais John Magufuli alivyoeleza jana katika siku ya pili ya ziara yake ya siku tatu mkoani Dar es Salaam.

Tunawakumbusha viongozi (madiwani na watendaji) kwamba jukumu kubwa lililoko mbele yao ni kuboresha jiji na kuliwezesha kufanya mambo makubwa hasa kwa kuzingatia kwamba, Dar es Salaam kwa sasa ni jiji la kibiashara.

Hivyo sasa ni wakati wa viongozi wa jiji hilo hilo kuongeza ubunifu katika kuibua miradi mipya na kutekeleza iliyopo pamoja na ukusanyaji wa mapato, ili liweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Kabla ya kuwa jiji, Ilala ilikuwa inatajwa kuwa miongoni mwa manispaa ambazo zinakusanya vizuri mapato, hivyo kwa uzoefu huo, ni wazi kwamba viongozi wakiongeza ubunifu, itakuwa rahisi jiji kupaa zaidi na kuwa mfano nchini.

Vilevile, tunaamini kwamba kuwapo kwa mabadiliko hayo, kuna faida nyingi, kwani hakutakuwa na Baraza la Madiwani la Jiji la Dar es Salaam, ambao wanateuliwa kuwakilisha manispaa.

Hii ina maana kwamba, madiwani wa Ilala, wataunda baraza lao, hivyo kupunguza gharama za uendeshaji ikiwamo mishahara, posho na pia kuondoa mgongano wa mamlaka katika usimamizi wa vyanzo wa mapato kati ya jiji na manispaa uliokuwapo kabla ya uamuzi wa juzi.

Kwa kuwa Ilala imekuwa jiji, ni wakati sasa kuwaandalia wamachinga mazingira mazuri ya biashara ili iweze kukusanya mapato bila migongano kutokana na awali kuwapo mkanganyiko kuhusu nani akusanye mapato hayo kati ya lililokuwa jiji na iliyokuwa Manispaa ya Ilala.

Tinaona pia kwamba kundi hilo litatengewa maeneo rasmi ya kufanya biashara katika mazingira rafiki, tofauti na ilivyo sasa.

Wakijengewa masoko ya kutosha na yenye miundombinu yote muhimu, itakuwa ni rahisi wao kwenda kufanya biashara na kuchangia kwa uhakika pato la jiji na hata taifa kwa ujumla.

Tunambua kuwa halmashauri hujiendesha kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ambavyo hukusanywa, ndiyo maana tunasisitiza ubunifu ikiwamo kubuni vyanzo zaidi vya mapato, ambavyo hata hivyo, havitawaumiza wananchi.

Ni matarajio yetu kwamba Rais kama kiongozi mwenye dhamana na TAMISEMI, ataendelea kufanya maamuzi ya kuzipandisha hadhi halmashauri ambazo zitaonekana kupiga kasi katika suala zima la ukusanyaji mapato, badala ya kuzipandisha hadhi kwa sababu za kisiasa.