Jamii isikubali makaburi kugeuzwa pango la wezi

19Jun 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Jamii isikubali makaburi kugeuzwa pango la wezi

KUNA taarifa kuwa makaburi mengi jijini Dar es Salaam hugeuzwa kuwa makiazi ya watu walio hai nyakati za usiku.

Katika taarifa hiyo iliyotokana na uchunguzi uliozaa ripoti maalum kwenye gazeti hili jana, ilibainika kuwa baadhi ya watu, bila woga wala aibu, wamekuwa wakitandika maboksi, magunia na hata magodoro kwa minajili ya kulala.

Ilibainika kuwa ugumu wa maisha ni miongoni mwa sababu zinazotajwa kuwavutia watu hao kwenye maeneo ya makaburi nyakati za usiku, hasa kutokana na ukosefu wa maeneo rasmi ya makazi kwa ajili yao.

Aidha, imebainika kuwa wapo pia wanaolala makaburini kwa minajili ya kukidhi masharti ya waganga wenye kuagua kwa taratibu za kishirikina. Wapo pia wanaodaiwa kulala kwenye makaburi kwa sababu ya kile kinachotajwa kuwa ni matokeo ya athari mbaya za matumizi ya dawa za kulevya.

Kwamba, wapo waliokataliwa katika nyumba za familia zao kutokana na kujihusisha kwao na utumiaji wa vilevi haramu na kuona kuwa mahala pekee panapowafaa ni makaburini.
Kundi jingine la watu hao walalao makaburini linatajwa kuwa ni lile la wezi na vibaka.

Inadaiwa kuwa hawa, hutumia makaburi kuwa sehemu yao ya kujificha baada ya kufanya maovu. Kwao, makaburi ni pango la kufichia mali za wizi na pia kujificha wenyewe pia. Sababu zinazotajwa ni nyingi.

Sisi tunaamini kwamba hili la kulala makaburini ni jipya. Ni kiwango cha juu cha ukiukaji wa maadili na utu wa Mtanzania. Tunaamini hilo kutokana na ukweli kuwa hapo kabla, haikuwahi kusikika kuwa kuna watu hulala makaburini au kujificha huko kwa sababu yoyote ile.

Bali, mara zote, maeneo hayo huchukuliwa kuwa ni mahala pa kuheshimiwa sana. Ni mahala palipoheshimiwa na wema na waovu kutokana na ukweli kuwa binadamu wote wangali katika safari ya pumziko la milele katika maeneo hayo.

Cha kusikitisha, katika taarifa hiyo, imebainika kuwa wanaolala ni wengi na baadhi yao hutundika hadi vyandarua ili kujiepusha na mashambulizi ya mbu ili wapate usingizi mnono. Wengi kati ya wale waliobainika kuyageuza makaburi kuwa sehemu zao za malazi hufanya hivyo usiku na kuondoka asubuhi kwenda kwenye mihangaiko yao ya kimaisha.

Kwa mfano, katika makaburi ya Sinza, kwenye Manispaa ya Kinodnoni, imebainika kuwa kwa wastani hulala watu 30, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na mwenyekiti wa Mtaa wa Sinza A ambako makaburi hayo ndiko yalipo.

Jitihada kadhaa zimekuwa zikichukuliwa na serikali za mitaa bila ya mafanikio kutokana na kile kilichobainika kuwa mara zote, hata baada ya kufanyika kwa operesheni za kuwaondoa, watu walalao makaburini hurejea tena katika siku chache zijazo na kuendelea na utaratibu huo.

Ni kwa sababu hiyo, ndipo Nipashe tunaona kwamba sasa kuna kila sababu kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam na kwingineko nchini kupiga vita vitendo hivi. Kamwe, kusiwe na fursa hata kidogo kwa mtu yeyote yule kugeuza maeneo ya makaburi kuwa ‘pango’ la kujificha wahalifu na mali za kihalifu.

Wananchi wote kwa pamoja washirikiane na uongozi wa serikali zao za mitaa kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayelala makaburini kwa kisingizio chochote kile. Wasaidiane kuwatimua watu hao mchana na usiku. Wasipewe nafasi ya kuendelea kulala makaburini kwa sababu kufanya hivyo ni kukiuka mila na tamaduni za jamii nyingi za Kitanzania.

Isitoshe, kuwaachia watu walale makaburini ni sawa pia na kubariki wezi na vibaka kupata maficho maeneo hayo na kuendelea kuhatarisha usalama wa raia wema na mali zao.