Maadhimisho ya siku ya watu wenye ulemavu wa ngozi yanapaswa kuikumbusha jamii yetu kwamba bado watu hao wanakabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo ya kutishiwa maisha yao na watu ambao wamejikita katika imani za kishirikina.
Kwa miaka kadhaa yametokea matukio mengi ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi katika maeneo kadhaa nchini hususan katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Sababu kubwa ambazo zimekuwa zikiongeza kasi ya mauaji ya watu hao ni imani potofu za kishirikina miongoni mwa baadhi ya watu, ambao wanaamini kuwa kupata viungo vya mtu mwenye ulemavu wa ngozi kunamsaidia kutajirika pamoja na kupata nafasi za uongozi wa kisiasa wa kuchaguliwa.
Ni imani hizo potofu ambazo zimekuwa zikiwasukuma watu hao waliokosa maadili ya jamii kutumia fedha kutafuta viungo hivyo kwa gharama zozote kutoka kwa wahalifu ambao huwaua au kuwakata viungo watu wenye ulemavu wa ngozi.
Ni matukio ambayo yamekuwa yakitokea kwa kasi wakati wa uchaguzi na kusababisha hofu kubwa kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kuhusiana na hatima ya usalama wa maisha yao, kiasi kwamba wapo waliolazimika kuomba hifadhi na hadi sasa wanaishi kwa kuhifadhiwa na baadhi ya taasisi pamoja na wasamaria wema.
Watu hawa wanahitaji kulindwa na jamii kwa sababu inaonekana kwamba upo mtandao mpana wa wahalifu wanaojihusisha na kuwaua au kuwakata viungo kutokana na mauaji hayo kuanza kutokea kwa kasi katika nchi kadhaa jirani na Tanzania.
Mbali na jamii nzima kuwa na wajibu wa kuwalinda watu wenye ulemavu wa ngozi, pia watu hawa wana mahitaji mengi maalum na muhimu kwa ajili ya maisha yao hususan ya kiafya.
Kwa maumbile ya miili yao ni rahisi kupata magonjwa kadhaa ikiwamo saratani, hivyo inahitaji dawa, losheni na miwani ili kujikinga na mambo mbalimbali ikiwamo mionzi.
Hivi ni vitu ambavyo jamii inapaswa kuwasaidia wakavipata, lakini kwa upande wake Serikali hainabudi kulifanyia kazi suala hili na ikiwezekana iangalie uwezekano wa kupunguza kodi kwa vifaa maalum na dawa vinavyoingia nchini kwa ajili ya watu hao.
Tunaona kwamba pia ipo haja kwa watu wenye ulemavu wa ngozi kuwekewa utaratibu wa kupata huduma za bure za tiba katika hospitali, zahanati na vituo vya afya vya Serikali.
Tunasema hivyo kwa kuwa watu hawa ni sehemu ya makundi yanayohitaji huduma maalum kama wazee, watoto chini ya miaka mitano na wajawazito na kwa kufanya hivyo watakuwa wamepata ahueni kutokana na kuwapunguzia gharama za kujitibu na kuzuia magonjwa.
Kwa kuwa Sera ya Afya inaelekeza kuwa makundi hayo yapatiwe huduma za afya bila malipo, sio vibaya na kundi hili ambalo linakabiliwa na changamoto nyingi likapatiwa upendeleo huo.
Tunaunga mkono maadhimisho ya kila mwaka ya siku ya watu wenye ulemavu wa ngozi, lakini tunasisitiza kwamba ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha anawajibika kuwapa ulinzi sambamba na serikali pamoja na wadau kuwapatia huduma bora za msingi.










