Hatua hiyo imeshitua wadau wengi kutokana na uamuzi huo kuchukuliwa katika kipindi hiki ambacho nchi yetu iko katika ujenzi wa demokrasia.
Kupashana habari ni sehemu muhimu ya demokrasia na wananchi wa Tanzania wana haki ya kupata taarifa na hasa kutoka katika chombo muhimu kama Bunge. Bunge ni moja ya mihimili mitatu ya dola mingine ikiwa ni Serikali na Mahakama.
Uamuzi wa serikali wa kuzuia TBC kurusha matangazo ya moja kwa moja ya Bunge ni pigo kubwa kwa ujenzi wa demokrasia nchini.
Hatua hiyo ni sawa na kurudisha saa nyuma, au kulirudisha taifa hili enzi ya mfumo wa chama kimoja. TBC ni chombo cha umma na ndio maana kinapewa ruzuku inayotokana na kodi za wananchi wote.
Serikali imedai kuwa TBC imeshindwa kurusha matangazo hayo kutokana na gharama kubwa.
Hatua hiyo ni ya kushangaza, kwa sababu pamoja na TBC kupata ruzuku, lakini pia inaruhusiwa kurusha matangazo ya biashara.
Ni tofauti na vyombo vya umma kwenye nchi nyingine, ambavyo hupewa ruzuku, hivyo kutoruhusiwi kurusha matangazo ya biashara.
Mathalani, Shirika la Utangazai la Uingereza (BBC) hupewa ruzuku ya serikali pamoja na kukusanya ada kutoka kwa watu wanaomiliki seti za televisheni.
Mfano mmojawapo wa jinsi TBC inavyonufaika na fedha za matangazo ya biashara ni hivi karibuni ilivyorusha moja kwa moja harusi ya mtu binafsi.
TBC hiyo inayovuna fedha za ruzuku na matangazo ya biashara inashangaza kuona inashindwa kurudha matangazo ya moja kwa moja ya kipindi cha Bunge.
Hata hivyo, jambo linalosikitisha zaidi ni kuwa TBC inajipanga kuandaa vipindi vya Bunge vilivyorekodiwa na kuhaririwa. Kwa maneno mengine, serikali inataka kurudisha taifa hili kwenye enzi za zamani za Redio Tanzania.
Katika kipindi hicho, serikali ilikuwa inamiliki vyombo vya habari na vyombo binafsi vya habari vilikuwa haviruhusiwi.
Ikumbukwe kuwa vyombo vya habari binafsi vilianza kuruhusiwa kufanya kazi nchini baada ya taifa hili kurejesha mfumo wa vyombo vingi vya siasa.
Ni miaka 24, tangu nchi yetu ilipourejesha mfumo huo na wananchi walikuwa wanategemea kuwa taifa hili lingefuata mkondo wa kupanua zaidi demokrasia.
Hatua ya kuminya TBC kurusha matangazo ya Bunge inalitia doa taifa letu ambalo ni miongoni mwa mataifa duniani yanayosifika kwa kuheshimu na kufuata utawala wa kidemokrasia.
Kitendo cha TBC kutorusha moja kwa moja matangazo ya bungeni ni cha kuwanyima wananchi fursa ya kuwasikia michango ya wawakilishi wao.
Bunge katika miaka ya karibuni limegeuka kuwa tumaini la Watanzania kutokana na linavyofanya kazi ya kuisimamia serikali.
Watanzania wameshuhudia jinsi Bunge lilivyoibua vitendo vya ufisadi vinavyowahusika baadhi ya mawaziri na wantendaji waandamizi wa serikali.
Kashfa hizi ni pamoja na ile ya wizi wa fedha kwenye Akaunti ya Malipo ya Nje (EPA) iliyokuwa katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Escrow, Buzwagi, Operesheni Tokomeza na nyinginezo.
Bunge limekuwa likifanya kazi nzuri ya kuisimamia serikali kiasi kwamba wananchi wengi wamejenga imani nalo ikiwamo kuvutika kusikiliza mijadala mbalimbali.
Hatua ya TBC kusitisha matangazo ya moja inazua maswali mengi na hasa kwa wale wanaoamini katika ukweli na uwazi.
Tunaishauri TBC ifipie upya maamuzi hayo na kuyasitisha kwa kuwa yanawaminya wananchi kuwasikia wawakilishi wao.










