Wanaoficha sukari tuwafananishe na nani?

22May 2016
Beatrice Bandawe
Nipashe Jumapili
Tuzungumze kidogo
Wanaoficha sukari tuwafananishe na nani?

MWEZI huu nchi imesumbuka na uhaba wa sukari hali inayofanya bei kupanda na wananchi wa kipato cha chini kushindwa kumudu kuinunua na kukosa bidhaa muhimu inayotegemwa na watumiaji wa kila familia.

Licha ya kupanda, sehemu zingine haipatikani kabisa na kufanya watu wengine kutumia chumvi badala ya sukari.

Kinachosikitisha ni kuona baadhi ya wafanyabiashara wakiwa wamerundika sukari hiyo kwenye maghala, wakifurahia wananchi wanavyoteseka kuikosa.

Katika msako uliofanyika takribani sikukadhaa zilizopita, tani kwa tani za sukari zimegundulika kufichwa na baadhi ya wafanyabiashara hao katika mikoa mbalimbali, huku kwenye maduka zikikosekana.

Hali hiyo ilimfanya Rais John Magufuli kuchukua uamuzi wa kuagiza msako wa nchi nzima kwa wote walioficha na ikipatikana ichukuliwe na kuigawa kwa wananchi bure.

Uhaba wa sukari umewapa mwanya wafanyabiashara wenye uroho wa kupata pesa ya harakaharaka, kuingiza sukari toka nje ya nchi isiyo na kiwango na hivyo kuwalisha wananchi bidhaa isiyofaa kwa binadamu.

Baadhi ya wafanyabiashara wamegundulika kununua sukari kwenye viwanda vya hapa nchini na baadaye kuifungasha kwenye makasha yao na kuisafirisha nje ya nchi nyingine wakiuza hapa hapa nchini kwa bei ya juu.

Wanaofanya mchezo huo ni wafanyabiashara tunaoweza kuwaita wenye roho za kinyama na za uuaji.

Wafanyabiashara hao wana ndugu, jamaa na marafiki wanaoteseka kwa kuikosa bidhaa hiyo, lakini wanaochajali wao ni kutunisha mifuko yao.

Bei elekezi ya sukari iliyopangwa na serikali ni Sh. 1,800, lakini wafanyabiashara hao huiza kwa Sh. 2400 hadi Sh. 3,000. Katika baadhi ya maeneo bei imepaa hadi kufikia Sh. 4,000.

Baadhi ya maeneo bidhaa hiyo imepotea kabisa kwenye maduka, hali iliyokuwa inatia hofu kuwarudisha Watanzania miaka kadhaa iliyopita wakati walipokuwa wakipanga foleni kuipata tena wakiuziwa kwa kaya.

Hata hivyo, juhudi za serikali za kudhibiti wafanyabiashara hao wa sukari, zimesaidia kukamata tani nyingi zilizokuwa zimelala kwenye maghala zikisubiri kuuzwa kwa bei ya juu.

Ukitembea kila kona ya nchi hivi sasa kilio kikubwa ni uhaba wa sukari, kwenye mijadala mbalimbali bungeni, mitandao ya kijamii, vijiweni kilio ni hicho.

Kinachofurahisha ni uamuzi wa serikali kuamua sukari inayokamatwa kusambazwa kwa wananchi bure ili iwe fundisho kwa wafanyabiashara wengine wenye tabia ya kuwakomoa Watanzania wenzao.

Katika kukabiliana na uhaba huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amesema mkakati wa serikali ni kuongeza uzalishaji wa sukari na ifikapo mwaka 2019 tatizo hilo litakwisha.

“Wananchi wasiogope, serikali imechukua hatua kwa udhibiti mzuri ili tusije kuporomosha soko letu la ndani,” anasema.

Amesema serikali imetenga maeneo matatu yanayofaa kwa kilimo cha miwa, Bagamoyo, Ngerengere na Kigoma, ambako wanaweza kulima na kujenga viwanda vya sukari na uzalishaji ukawa unapanda mwaka kwa mwaka hadi pengo lililopo litakapomalizwa.

Katika sakata hilo la uhaba wa sukari, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kwa kushirikiana na jeshi la polisi, imekamata tani 1,840 zilizokuwa zimehifadhiwa Bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya miezi mitano.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akizungumzia sakata hilo, amesema tayari wamekamata jumla ya tani 54,860 za sukari, zilizofichwa na wafanyabiashara mbalimbali katika mkoa huo.

Wakati serikali ikipambana na wafanyabiashara wanaoficha sukari, makachero ‘feki’ wameibukia ukaguzi wa bidhaa hiyo mkoani Kilimanjaro, wakijitambulisha kuwa ni maofisa wa Takukuru.

Wanadaiwa kKIDUCHU MEI uomba rushwa kwa wafanyabiashara hao kwa madai ya kuwasafisha kwa Rais.

Hata hivyo, Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, imesema maofisa wake wote wana vitambulisho na kama watatiliwa shaka, wafanyabiashara wameombwa waijulishe ofisi hiyo kwa kutumia simu ya mkononi namba 0784 998 804 au 0786 089 805.

Kama sukari iliyokamatwa itasambazwa kwa wakati kama serikali ilivyoahidi, hawa matapeli walioanza kujitokeza wataumbuka na wananchi wataendelea kupata bidhaa hiyo kama kawaida tena kwa bei elekezi iliyopangwa na serikali.

Vita hivi vya kupambana na walanguzi wa sukari ni vya wote, hivyo wananchi hatuna budi kutoa ushirikiano popote pale tutakapoiona sukari imefichwa tutoe taarifa ili kuepuka uhaba huu.

Tushirikiane kuikomboa nchi yetu katika janga hili.
bbandawe@hotmail.com; Simu: 0774 466571