Hivi karibuni, mathalan, kumekuwapo na taarifa za kukithiri kwa vitendo hivyo katika baadhi ya vyuo, hatua ambayo iliwafanya wanaharakati kuingilia kati na kutaka uchunguzi ufanyike na wale wanaobainika kujihusisha na vitendo hivyo wachukuliwe hatua.
Miongoni mwa vyuo ambavyo vilitajwa hivi karibuni kuwa vinara wa vitendo hivyo ni Mtakatifu Augustino (Saut), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE). Katika taasisi hizi na nyinginezo, ilidaiwa kuwa baadhi ya wanataaluma wamekuwa wakiwataka wanafunzi wa kike kufanya nao mapenzi ili wawasaidie kufaulu mitihani ya vyuo.
Kutokana na kuwapo kwa tuhuma hizo, serikali iliingilia kati na kukemea kwa juhudi zote huku ikionya kuwa haitakuwa na msalie mtume na watu wote watakaobainika kujihusisha na aina hiyo ya rushwa ambayo ni sehemu ya ukatili wa kijinsia. Tunasema ni ukatili wa kijinsia kwa sababu mhusika (mwanafunzi) analazimishwa kufanya tendo la ndoa bila ridhaa yake na matokeo yake ni kumwondolea utu wake.
Hivi karibuni, wakati wa mkutano wa wakuu wa taasisi za elimu ya juu uliofanyika jijini Dodoma, serikali ilikunjua tena makucha yake na kukemea kwa nguvu zote kuandelea kukithiri kwa vitendo hivyo.
Katika ufunguzi wa mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Dk. John Jingu, aliwapasha bayana wakuu hao juu ya vitendo hivyo vya aibu.
Bila kuuma maneno, Dk. Jingu ambaye kabla ya kushika wadhifa huo alikuwa mhadhiri UDSM, alisema vitendo hivyo vimeitia nchi doa baya na kuifanya sekta ya elimu hasa ngazi ya elimu ya juu kudharauliwa na kuchafuliwa.
Licha ya taasisi hizo hadhi yake kuporomoka, alisema rushwa ya ngono inasababisha kushuka kwa elimu kwa sababu ya kuzalisha wasomi ambao hawana sifa wala uwezo wa kushindana katika soko la ajira.
Sambamba na hilo, kiongozi huyo alisisitiza kwamba rushwa hiyo inasababisha hata kuporomoka kwa uchumi, hivyo kwa kuzingatia hayo, vitendo hivyo vya aibu havina budi kukomeshwa.
Hata hivyo, akifunga mkutano huo juzi, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Francis Michael, alitoa sehemu ya suluhisho la kumaliza kashfa hiyo kwenye ngazi hiyo ya juu ya elimu nchini. Katika hotuba yake, Dk. Michael alisema njia mojawapo ya kukabiliana na vitendo hivyo ni kuanzishwa madawati ya jinsia katika taasisi hizo.
Wazo hilo ni mwafaka kwa sababu litasaidia kwa kiasi kikubwa kupambana na vitendo hivyo kwa sababu wale watakaonyanyaswa, watakuwa na nafasi ya kuripoti matukio hayo ya aibu na hatimaye hatua kuchukuliwa.
Suala hilo halina budi kutekelezwa kwa haraka kwani ni imani yetu kwamba licha ya kupunguza vitendo hivyo, litasaidia kuwafichua wale wote wanaoendeleza uovu huo na kuchukuliwa hatua stahiki.