Kujitolea ndiko kusogeza karibu huduma za afya

22Aug 2019
Sabato Kasika
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kujitolea ndiko kusogeza karibu huduma za afya

KUTEMBEA umbali mrefu kufuata huduma za afya ni moja ya changamoto, ambayo inazikumbuka baadhi ya wananchi wa mikoa mbalimbali.

Hata hivyo, baada ya serikali kuanzisha mkakati wa kujenga zahanati kila kijiji, baadhi ya vijiji vimeanza kunufaika nao, huku wananchi wakiunga mkono mkakati huo kwa kujitolea kujenga zahanati kwenye maeneo yao.

Miongoni mwa wananchi waliofanikiwa kutimiza azma hiyo ni wakazi wa vijiji vya Wilaya ya Musoma Vijijini mkoani Mara, ambao wamekuwa wakijitolea kwa hali na mali kujenga zahanati ambazo sasa zimefikia 20 na zinaelezwa kuwa zinatoa huduma.

Dokta Vincent Anney ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma, ambaye anasema mbali na hizo, zipo nyingine mpya zinazoendelea kujengwa katika vijiji mbalimbali ili kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati.

Anasema mbali na ujenzi wa zahanati, wananchi hao pia wamekubali kuchangia ujenzi wa hospitali ya wilaya, ambao unaendelea sasa kwenye kitongoji cha Kwikonera katika kijiji cha Suguti.

"Musoma Vijijini ina kata 21, na kwenye kuchangia ujenzi wa hospitali ya wilaya, kila kata imekubali kuchangia Sh. milioni 7.5 na matarajio  yetu ni kupata Sh. milioni 157.5," anasema Dk. Anney.

Kadhalika anasema kuwa mchango huo wa wananchi ni kuunga mkono juhudi za serikali kuu, ambayo imetoa Sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo, ambayo tayari majengo yake manane yameezekwa.

Suala la wananchi kuchangia ujenzi wa zahanati, vituo vya afya na hospitali ni la muhimu kwani wao ndiyo wanaotarajia kupata huduma pale ujenzi unapokamilika.

Kwa mfano wakazi wa Musoma Vijijini, baadhi ya wananchi wamekuwa wakiuza mifugo yao ikiwamo ng'ombe ili kupata fedha za kuchangia ujenzi wa zahanati, kituo cha afya au hospotali.

Wengine wanasomba, mawe, mchanga, maji na kokoto, lengo likiwa ni kufanikisha ujenzi huo ili kusogeza karibu huduma za afya karibu yao na kuondoka na changamoto ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma hiyo.

Hii inatokana na ukweli kwamba haiwezekani viongozi kwenda kuomba msaada kwa watu wa nje kwa ajili ya kuwajengea zahanati au hospitali wakati wananchi wenyewe wapo na ndio wanufaika wakubwa.

Kwa kawaida, serikali imekuwa ikiunga mkono pale wananchi wanapoonyesha jitihada katika jambo fulani la maendeleo, hivyo ni muhimu wananchi waendelee kuonyesha mfano kama hao wa Musoma Vijijini.

Inawezekana wakawapo baadhi ya wananchi, ambao hawataki kusikia habari za kuchangia maendeleo, lakini ninaamini kwamba wanaojitolea wanaweza kuwa chachu kwa watu wa aina hiyo.

Kimsingi ni kwamba utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa zahanati kila kijiji, vituo vya afya kila kata na hospitali kila wilaya ili kusogeza huduma ya afya karibu na wananchi, hivyo juhudi hizo hazina budi kuungwa mkono.

Hivyo kama kuna baadhi ya wananachi ambao hawajatambua umuhimu wa kuchangia ujenzi huo, basi waendelee kuelekezwa vizuri wataelewa na mwisho wa siku wanaweza kuwa mstari wa mbele kushiriki kikamilifu.

Ikumbukwe kuwa afya maana yake ni hali ya ukamilifu kimwili, kiakili, kijamii na kutokuwapo  kwa  maradhi na pia afya bora ni nguzo na raslimali muhimu  katika  kuchangia  mtu na taifa.

Kwa mantiki hii afya inalenga kuwa na ustawi endelevu wa jamii, kwa kuzingatia mchango wa mtu binafsi kulingana na nafasi, uwezo na fursa zilizopo katika kuleta maisha bora.