Kila taasisi ielewe mwelekeo wa Rais

01May 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Kila taasisi ielewe mwelekeo wa Rais

Akifungua kikao cha kazi cha Makamanda wa Polisi wa Mikoa, Mawakili wafawidhi wa serikali wa Mikoa na Wakuu wa upelelezi wa Mikoa na Vikosi mjini Dodoma juzi, Rais John Magufuli alilitaka jeshi hilo kuelewa mwelekeo wake wakati akiongoza serikali ya awamu ya tano.

Rais Magufuli alisema si tu kuna taarifa za matumizi mabaya ya fedha zinazotolewa na serikali kwa ajili ya kununulia vifaa na sare za askari Polisi:

Lakini pia mikataba yenye mashaka inayotiwa saini kati ya Polisi na wawekezaji, ni baadhi ya mambo yanayoongeza hali ngumu ya utendaji kazi kwa jeshi hilo.

Rais Magufuli alitoa mfano wa uwekezaji unaofanyika kwenye eneo la kituo kikuu cha mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, cha Oysterbay jijini Dar es Salaam ambako alishangaa kuona licha ya kwamba ni eneo lenye thamani kubwa, jeshi hilo limeingia kwenye mikataba inayoijua lenyewe.

Rais Magufuli akaonyesha kama yeye ndiye angekuwa mwenye sahihi ya mwisho katika mradi wa uendelezaji wa eneo hilo, mipango yake kwa eneo la Oysterbay ingekuwa kutafuta hati, kisha akaitumia hati hiyo kukopa benki na kujenga nyumba hata za ghorofa 20 mahali hapo.

Majengo hayo, alisema Rais, yangekuwa kitega uchumi na nyumba zilizobaki zikawa makazi bora ya Polisi.

Rais Magufuli pia alilitaka Jeshi la Polisi kujiepusha na kashfa ambazo zimekuwa zikisemwa dhidi yake, ikiwemo maafisa wa Polisi kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na kuazimisha silaha kwa majambazi.

Tuchukue fursa hii, Nipashe, kwanza kumpongeza Rais kwa kuwa na maono ya mbali, kwa sababu uwekezaji ambao amependekeza ungekuwa si tu endelevu bali pia wenye tija ZAIDI kwa Jeshi la Polisi na uchumi wa nchi kwa ujumla, kwa kupunguza bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kwa ujumla.

Lakini pili tuchukue fursa hii pia, Nipashe, kumpongeza Magufuli kwa kuwa kwake muwazi na kulitaka jeshi hilo kuelewa muelekeo wa Rais wa Tano huyo ambaye wananchi wamemkubali kwa moyo wake wa dhati wa kutaka kuinua maisha ya watanzania, hasa wa kipato cha chini.

Kwamba kauli ya Rais ya juzi imekuja wakati sakata la mkataba wa Kampuni ya Lugumi Enterprises na Polisi likiwa halijapoa, ni dalili kuwa jeshi hilo lina mengi ya kujitathmini, linapokuja suala la mikataba.

Mkataba kati ya Polisi na kampuni ya Lugumi umezua mjadala mkali nchini kiasi cha Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuunda kamati ndogo kufanya uchunguzi kama ulitekeleza kama ilivyokuwa kwenye makubaliano na kama haukuwa wa kifisadi.

Rais Magufuli aliliambia jeshi la polisi na ni matarajio yetu Nipashe, kuwa atazungumzia tena uelekeo wa serikali ya awamu ya tano ya uongozi wa nchi, katika hotuba yake kwenye kilele cha sherehe za Mei mosi leo mjini Dodoma.

Lakini tuchukue fursa hii pia, Nipashe, kuwataka wakuu wa taasisi, wakala na idara za serikali, majeshi na vikosi vyake yakiwamo, kusoma alama za nyakati na kuelewa kwa pamoja muelekeo wa Rais wa Tano, kama mwenyewe alivyoiomba Polisi.

Ni rahisi, kwa hulka ya binadamu, kwa mtumishi wa umma kushawishika na kujikuta ameweka nyuma maslahi ya nchi pindi anapokuwa katika nafasi nyeti ya kutoa maamuzi yanayohusu watu wengi.

Lakini uzalendo, ambo unaelekea kuwa ndiyo msingi wa maamuzi katika utumishi wa serikali ya awamu ya tano, unatulazimisha kuweka maslahi ya taifa mbele kabla ya ubinafsi.

Kila taasisi, basi, ijifunze na kuelewa kwanza, mwelekeo wa Rais Magufuli.