Samatta ajeruhiwa pua Ulaya

27Apr 2016
Somoe Ng'itu
Dar es Salaam
Lete Raha
Samatta ajeruhiwa pua Ulaya

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jana alitarajiwa kufanyiwa vipimo vya pua baada ya kuumia Jumapili katika mchezo wa mchujo wa kuwania kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.

Mbwana Ally Samatta.

Samatta alicheza kwa dakika 45 tu za kwanza Jumapili usiku, wakati timu yake, KRC Genk ikifungwa 2-1 na Gent katika mchezo wa mchujo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji kuwania kucheza michuano ya Ulaya, tena Uwanja wa nyumbani, Cristal Arena mjini Genk.

Samatta alitolewa baada ya kumalizika kipindi cha kwanza, akimpisha mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis ambaye wamekuwa wakipokezana siku zote.

Na baadaye Genk ikasema Samatta aliumia pua ndiyo maana akashindwa kuendelea na mchezo. Samatta mwenyewe jana asubuhi alisema kwamba alisikia maumivu makali na kizunguzungu baada ya kugongana na mchezaji wa Genk, hivyo akaona apumzike na alitarajiwa kufanyiwa vipimo jioni.

Samatta alitoka timu hizo zilikuwa zimefungana bao 1-1, Genk wakitangulia kwa bao la Leon Bailey dakika ya 16, kabla ya Laurent Depoitre kuwasawazishia wageni dakika ya 23.

Renato Neto akaifungia Gent bao la ushindi kwa penalti dakika ya pili ya muda wa nyongeza baada ya kutimu kwa dakika 90 za kawaida za mchezo.

Huo ulikuwa mchezo wa 11 tangu ajiunge na Genk Januari mwaka huu akitokea TP Mazembe ya DRC, akiwa amefunga mabao nne.

Samatta alifunga bao moja katika ushindi wa 2-1 ugenini dhidi ya wenyeji SV Zulte-Waregem mwishoni mwa wiki baada ya awali kufunga katika ushindi wa 4-0 na 4-1 dhidi ya KV Oostende na 3-2 dhidi ya Club Brugge.