Mvutano uliopo unahusu uundwaji wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ambazo hazina wenyeviti tangu kufanyika kwa uchaguzi wa Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge Januri 21, mwaka huu.
Kamati hizo kwa mujibu wa kanuni za Bunge na utamaduni wa mabunge ya Jumuiya ya Madola, zinapaswa kuongozwa na wabunge wa upinzani. Hata hivyo, upinzani ulisusia kuteua wenyeviti wa kamati hizo ambazo hufuatilia kwa karibu matumizi ya fedha za umma kutokana na kubaini kuwa kuna mambo hayakwenda sawa.
Hoja zilizotolewa na wabunge wa Ukawa ni kwamba kamati hizo ni zao, hivyo walitakiwa kushirikishwa katika uteuzi wa wajumbe kwa kuwa miongoni mwao watapatikana wenyeviti wa kamati hizo badala ya Spika kuwateua bila mashauriano.
Kimsingi, kutoteuliwa kwa wenyeviti kutakuwa kumeathiri shughuli nzima za kamati hizo vikiwamo vikao vilivyokuwa vinafanyika takribani wiki mbili zilizopita kabla ya kuanza kwa mkutano wa Bunge jana.
Kwa mfano, miongoni mwa mambo yaliyoibuka wakati wa vikao hivyo ni suala la mkataba tata wa ufungaji wa vifaa vya kutambua alama za vidole katika vituo vya Polisi nchini ambao zabuni hiyo ya Sh. bilioni 37 ilitolewa na Jeshi la Polisi kwa Kampuni ya Lugumi.
Ingawa PAC chini ya Makamu Mwenyekiti kutoka CCM, Aeshi Khalfan Hilaly, ilionyesha ujasiri kwa kudai mkataba huo kutoka Polisi, lakini kukosekana kwa mwenyekiti kutoka upinzani kulionekana dhahiri.
Ni dhahiri kamati hizo muhimu zimekaa muda mrefu bila wenyeviti, hivyo kuna haja kwa Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani na Spika kuketi mezani mapema iwezekanavyo katika mkutano unaoendelea ili kufikia muafaka kwa kuwa hakuna anayenufaika na mvutano huo.
Kwa bahati nzuri wabunge wa Ukawa kupitia kwa Mwenyekiti Mwenza wa umoja huo, James Mbatia, ambaye pia ni Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), alisema juzi kwamba waliingia bungeni leo jana wakiwa na ushauri wa kutaka kuitishwa meza ya mazungumzo kwa ajili ya maridhiano.
Tunaishauri ofisi ya Spika kuona umuhimu wa kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa kukubali kukutana na wabunge wa upinzani kulijadili suala hilo na kulipatia ufumbuzi kwa kuwa ni la kikanuni.
Itakuwa vizuri kama Spika Ndugai atashauriwa vizuri na wasaidizi wake akawashirikisha wabunge wa upinzani katika uteuzi wa wajumbe wake wa kuingia katika PAC na LAAC ili iwe rahisi kwao kuchagua wenyeviti ambao wataona kuwa wana sifa zinazotakiwa.
Hakuna ubishi kwamba kamati hizo zinahitaji wenyeviti wenye uwezo mkubwa na uzoefu wa kuibua mambo yanayohusiana na matumizi mabaya ya fedha za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa, kujenga hoja na kuzitetea.
Uzoefu unaonyesha kuwa wenyeviti wote walioziongoza kamati hizo tangu utaratibu wa kuongozwa na upinzani wakati wa Bunge la Tisa, walikuwa watu wenye sifa hizo na ndiyo maana utendaji wao ulikuwa wa tija na ufanisi mkubwa.
Tunaamini kuwa wakipatikana wenyeviti wenye sifa hizo, Bunge letu litaendelea kuwa na 'meno' katika kufuatilia utendaji wa serikali hususan matumizi ya fedha za umma.










