Hatua ya vyuo hivyo ni mchango wao katika harakati za wilaya hiyo kutatua upungufu wa madawati na kuwafanya wanafunzi kukaa chini.
Vyuo vilivyokubali kutengeneza madawati kwa bei ya chini ni Kyela Polytecnic College (KPC), Moravian na Chuo cha Upendo.
Kwa pamoja, vyuo hivyo vimekubali kutengeza madawati kwa bei ya Sh. 13,000 badala ya Sh. 40,000.
Serikali wilayani humo imetimiza agizo la Rais John Magufuli, la kutaka kila wilaya ihakikishe inamaliza tatizo la madawati shuleni baada ya kuitisha harambee mwishoni mwa wiki ya kutafuta fedha kwa ajili ya kutengeneza madawati.
Katika harambee hiyo, yalipatikana madawati 3,406 huku kukiwa na upungufu wa madawati 1,594 ili kufikia 5,000 yanayohitajika.
Wadau mbalimbali wilayani humu wakiwamo waishio jijini Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange, Mkurugenzi wa Majengo nchini, Elius Mwakalinga na Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Akson, walifanikisha upatikanaji wa madawati hayo.
Aidha, kampuni mbalimbali na taasisi za kifedha wilayani humu, pia zilijitokeza katika harambee hiyo.
Mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza meli Songoro Marini, Salehe Songoro, aliwaongoza wenzake kwa kampuni yake pekee kutoa Sh. milioni nane kuhakikisha shughuli hiyo inakamilika.
Madiwani kwa umoja wao na wakuu wa idara kwa nafasi zao ikiwa ni pamoja na waandishi wa habari, pia walitoa michango yao ambapo kupitia harambee hiyo, walitoa fedha kuunga mkono jitihada za serikali kuhakikisha madawati yanapatikana.
Baada ya kumalizika kwa harambee hiyo, ndipo Umoja wa Mafundi Seremara wilayani humo walipojitokeza wakisema wanaungana na vyuo hivyo kutengeneza madawati kwa bei hiyo ili iwe sehemu ya mchango wao kuhakikisha wanafunzi suala la kukaa chini kwa wilaya hiyo inabaki kuwa historia.
Mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Thea Ntara, alisema tayari amefanikiwa kutimiza agizo la Rais Magufuli kwa kumaliza tatizo la madawati.
Dk. Ntara alisema mbali na upatikanaji wa madawati hayo, pia amehakikisha ugonjwa wa kipindupindu unamalizika licha ya kuwapo kwa changamoto lukuki.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Clement Kasongo na Mwenyekiti wa Halmashauri, Dk. Hunter Mwakifuna, kwa nyakati tofauti, waliwapongeza wadau waliojitokeza katika harambee hiyo licha ya kuwapo na hali mbaya ya hewa kutokana na mvua za mafuriko zinazoendelea kunyesha wilayani humu.
Walisema watahakikisha shughuli hiyo ya madawati inasimamaiwa na kufanyika kama lilivyopangwa ili kusiwapo na lawama.










