Adhabu hizi TFF zinafunza, zinabomoa?

04Apr 2016
Mhariri
Dar
Nipashe
Adhabu hizi TFF zinafunza, zinabomoa?

SOKA la Tanzania limetumbukia katika aibu kubwa ya upangaji matokeo. Katika mchezo wa soka unaoongozwa kwa kupendwa ukiwa na mashabiki zaidi ya bilioni 3.5 duniani kote ni kosa kubwa kushawishi matokeo ya uwanjani kuamriwa kwa kupangwa.

Lakini kwa Tanzania, sasa ni mchezo wa kawaida. Kuna mechi nyingi matokeo yake yamekuwa yakipangwa na kuitia aibu nchi.

Upangaji mwingine wa matokeo umevuka mipata ya aibu kiasi cha kukosa neno moja la kuielezea hali hiyo. Lakini kweli inasikitisha.

Mfano wa matokeo mabaya ya kupangwa ni mechi za ligi daraja la kwanza.

Timu zilizohusika katika sakata hilo zilikuwa ni Geita Gold Sport ya Shinyanga, JKT Kanembwa ya mkoani Kigoma, JKT Oljoro kutoka jijini Arusha na Polisi Tabora ya Tabora.

Katika mechi za mwisho za kundi hilo na matokeo yake kushtua wengi kiasi cha kuwafanya kutoamini walichosikia, Geita Gold walishinda mabao 8-0 dhidi ya Polisi, huku Polisi Tabora ikipata ushindi wa magoli 7-0 dhidi ya JKT Oljoro.

Kumbukumbu za kundi hilo zinaonyesha kwamba hakuna timu iliyowahi kupata ushindi wa kuanzia mabao 3-0 katika mechi zilizopita, kuanzia JKT Kanembwa ambao ilikuwa inaburuza mkia kwenye kundi hilo, wakati JKT Oljoro aliweka mpira kwapani dakika ya 68 baada ya kufungwa bao la pili wakati anacheza na Geita Gold Sport.

Juzi Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ilitangaza uamuzi waliouchukua baada ya kufanya uchunguzi wake kuhusiana na mechi hizo mbili.

Uamuzi uliotolewa na kamati hiyo uliosomwa na Makamu Mwenyekiti, Jerome Msemwa na uliishusha daraja Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Kanembwa na JKT Oljoro baada ya kuzikuta na hatia ya kupanga matokeo.

JKT Kanembwa imeshushwa hadi Ligi ya Mkoa, wakati Geita Gold, Polisi Tabora na JKT Oljoro zimeshushwa hadi Daraja la Pili, huku pia refa, viongozi wa Chama cha Soka Tabora (Tarefa), kocha msaidizi Polisi Tabora na Mwenyekiti Oljoro wakifungiwa kujihusisha na mchezo huo kwa miaka 10 na kutozwa faini ya Sh. milioni 10.

Kamati hiyo pia 'imemhukumu' kipa wa Geita Gold, Denis Richard ambaye aliazimwa kutoka kikosi cha Simba B kucheza soka kwa muda wa miaka 10 na kulipa faini ya Sh. milioni 10 kutokana na kuhusika na sakata hilo.

Ni kweli mechi hizo mbili wazi zina harufu ya upangaji wa matokeo, lakini kwa faida ya soka la Tanzania, adhabu kwa kipa Richard ambaye umri wake ni chini ya miaka 20, tunadhani haiko sahihi.

Siyo kwamba tunaunga mkono vitendo vilivyofanyika, lakini tunajiuliza kwa mchezaji mwenye ndoto ya kusonga mbele, adhabu kama hiyo inamsaidia au inampoteza?

Kamati ilipaswa kuangalia uzito wa adhabu kwa mchezaji huyo, huku ikizingatia TFF sasa inatumia kiasi kikubwa cha fedha kuwekeza kwa wachezaji chipukizi ili icheze Dunia 2026.

Simba ambayo ndiyo ina mkataba na mchezaji huyo, mna nafasi ya kukata rufaa kupinga adhabu hiyo iliyotolewa kwa kuzingatia kanuni ya 69 ya mechi za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza ya 2015.

Mbali na hili la kupanga matokeo, TFF na kamati zake pia inatakiwa kukutana na kutoa uamuzi wa malalamiko na rufaa mbalimbali zilizowasilishwa badala ya kusubiri 'kelele' kutoka kwa wadau wa mchezo huo.

Kwa kukaa kimya na kutoa uamuzi kwa kuchagua baadhi ya malalamiko, TFF itaendelea kuelemewa na lawama za kufanya kazi kwa kubabaisha.