TRA kukamata gari za TFF ni uzembe usio na samahani

03Apr 2016
Mhariri
Dar
Lete Raha
TRA kukamata gari za TFF ni uzembe usio na samahani

SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) lipo katika wakati mgumu kwa sasa kufuatia kukamatwa kwa gari zake zote tano, zinazofanya shughuli mbalimbali ikiwemo kubeba wachezaji wa timu za taifa.

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekamata gari tano za TFF kutokana na deni la kodi la Sh. Bilioni 1 Milioni 118 ambazo ni malimbikizo tangu mwaka 2010, wakati shirikisho hilo likiwa chini ya Rais Leodegar Tenga.

Na Rais wa sasa wa TFF, Jamal Malinzi amesema kwamba ana wasiwasi hata Uwanja wa Karume, unaweza kupigwa mnada na TRA kutokana na kwamba gari zilizokamatwa hazifikii thamani ya deni.

Malinzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA), aliyeingia madarakani Oktoba 28, mwaka 2013 ameonakana kabisa kunyong’onyeshwa na hali hiyo kiasi cha kusema hali ni mbaya.

Ofisa wa TRA, Richard Kayombo alikaririwa na vyombo vya Habari akisema kwamba wamekamata gari hizo ili kuwapa shinikizo TFF waweze kulipa madeni hayo yanayotokana na malimbikizo ya kodi mbalimbali kuanzia mwaka 2010 hadi 2015, zikiwemo za VAT na mishahara ya wafanyakazi wake.

Ikumbukwe Desemba mwaka janaTRA ilizifungia akaunti zote za TFF kutokana na na suaa hilo hilo la kodi, wakati huo deni likiwa Sh. Bilioni 1.6, lakini baadaye wakaachiwa baada ya mazongumzo yaliyoihusisha Serikali, kupitia Waziri wa Michezo, Nape Nnauye.

Hata hivyo, katika hali ya kustaajabisha suala hilo linaibuka upya na safari hii gari za TFF zinakamatwa. Lete Raha tunaona kuna uzembe ulifanyika hapa katikati ndiyo maana suala hilo limeibuka tena ghafla.

Tulidhani mazungumzo baina ya viongozi wa TFF na Nape yalipata suluhisho la kudumu la tatizo hilo, lakini kukamatwa kwa gari hizo ni kilelezo kwamba kikao chao hakikuwa na suluhisho wala faida kama miezi mitatu baadaye mambo yanaibuka tena upya.

Tulitarajia kikao cha Nape na viongozi wa TFF kingekuwa na ufumbuzi wa suluhisho la kudumu la deni kubwa, ambalo halilipiki kwa urahisi na kwa haraka.

Hakuna samahani yoyote katika hilo zaidi ya kusema kuna uzembe ulifanyika ndani ya TFF, ndiyo maana suala hilo limeibuka tena baada ya miezi mitatu.

Na Lete Raha tunaona kabisa kama aina hii ya uzembe na upuuzi kwenye mambo mazito kama haya itaendelea siku moja ndoto za Malinzi zitatimia kweli kwa Uwanja wa Karume kupigwa mnada, hususan kipindi hiki cha Serikali isiyo na mzaha ya Rais Dk. John Joseph Pombe Magufuli.

Lete Raha tunaamini Malinzi aligombea TFF kwa ukereketwa wake wa soka, dhamira ikiwa ni kuja kuleta mabadiliko katika soka ya Tanzania, lakini kwa mwenendo huu tunaona anaweza kugeuka kuwa sumu, iwapo ataendelea kuruhusu uzembe wa aina hii ndani ya shirikisho.