Malinzi ameshindwa, awapishe wengine

02Apr 2016
Barnabas Maro
Nipashe
Muungwana Lazima Nilonge
Malinzi ameshindwa, awapishe wengine

“ASIYEONYWA huona kwa macho yake.” Maana yake mtu anayekanywa kisha akayapuuza maonyo yale huishia kufikwa na madhara.

Hii ni methali iwezayo kutumiwa kumwelezea mtu anayepuuza ushauri anaopewa, kuwa atakuja kupatwa na madhara mbele ya safari. Yatufunza umuhimu wa kuzingatia ushauri tupewao na wenzetu.

Pia twaambiwa: “Asiyesikia hujionea mwenyewe.” Ni methali itumiwayo kutunasihi kuthamini mashauri mazuri tupewayo na wanaotuzidi maarifa.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Kandanda Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, haambiliki wala hashauriki. Utendaji wake katika shirikisho hilo tangu aingie mdarakani wanifanya nikumbuke utendaji wa aliyemtangulia, Leodgar Tenga.

Tangu Malinzi aingie madarakani baada ya kutoa ahadi kemkem ya kuboresha mchezo wa kandanda nchini, amekuwa akifanya kinyume chake takriban kwa kila jambo.

Upangaji wa ratiba za Ligi Kuu hauna utaratibu maalumu, kwani misimu yote hukumbwa na matatizo na malalamiko kwa timu zinazoshiriki. Ratiba za TFF huingiliana na michezo ya kimataifa inayopangwa na CAF na Fifa, hivyo kufanyiwa marekebisho ya hapa na pale mara kwa mara.

Ratiba za mechi za kimataifa hupangwa mapema kabla ya TFF. Pamoja na kupewa ratiba hizo mapema, bado shirikisho hilo hushindwa kabisa kuendana nazo. Matokeo yake ligi yetu husimamishwa mara kwa mara au ratiba kurekebishwa kupisha michezo ya kimataifa. Mbona Ulaya mechi huchezwa kwa utaratibu mzuri na timu hutofautiana kwa mechi moja tu kuliko sisi?

Tanzania kuna timu zinazocheza mechi nyingi zaidi na zingine kucheza chache. Kama hiyo haitoshi, timu moja yaweza kupangiwa mechi nne mfululizo za ugenini.

Wakati mwingine mchezo huahirishwa wakati timu ngeni ikiwa imeshafika kituoni! Hakuna fidia inayolipwa timu ngeni bali hujigharimia yenyewe wakati ilitegemea mapato ya mechi.

TFF ya Malinzi haijali gharama zinazoigharimu timu. Hakuna msaada wowote unaotolewa na TFF kufidia gharama za timu husika. Ni katika kile kisemwacho na vijana wa mjini kuwa “imekula kwao!”

Kinachoshangaza ni TFF kuruhusu timu inayoshiriki Ligi Kuu kwenda kucheza mechi za kirafiki n-nje ya nchi wakati ligi ikiendelea badala ya kufuata ratiba yake. Matokeo yake timu zilizopangwa kucheza na timu husika hulazimika kutocheza au kupangiwa timu zingine baada ya ratiba kurekebishwa. Ni vurugu tupu!

Azam na Yanga zinaiwakilisha Tanzania kimataifa lakini zimepangiwa kucheza mechi tatu mfululizo ili kuwa sawa na timu zingine. Na hii ni baada ya Simba kulilalamikia shirikisho hilo kwa kucheza mechi tatu zaidi ya Azam na Yanga.

Wakati Azam ikiwa na mchezo wa kimataifa dhidi ya Esparance ya Tunisia na Yanga ikiisubiri Al Ahly ya Misri, zatakiwa kucheza mechi tatu za viporo, huku zikikabiliwa na mechi za kimataifa.

Shirikisho halijali uchovu wa wachezaji kucheza mechi mfululizo kinyume cha kanuni za Fifa. Wala halifikirii uwezekano wa wachezaji wetu kuumia katika mechi za nyumbani na kupoteza zile za kimataifa.

Malalamiko kuhusu uchezeshaji wa waamuzi ni mengi, lakini hakuna adhabu ya maana wapewayo ingawa makosa hayo huonekana wazi uwanjani.

Ni kama shirikisho hilo lina ajenda ya siri dhidi ya timu za mikoani ili kuzinufaisha Azam, Simba na Yanga za Dar es Salaam!
Wachezaji hufanya vituko uwanjani kwa kushikana sehemu za siri na kupigana viwiko, lakini wanaoadhibiwa ni wa timu za mikoani ila za Dar es Salaam zafumbiwa macho!

Runinga ya Azam huonesha kila tukio uwanjani, lakini TFF eti hutafuta ushahidi kwa kukaa mezani. Kwanini hawaombi mikanda ya Azam TV kuangalia mechi zinazolalamikiwa ili waone ukweli wenyewe? Shirikisho halitaki kwa sababu ‘wakubwa’ ambao ndio chanzo cha kuliingizia fedha, wataumbuka.

Kuna malalamiko ya kupanga matokeo katika mechi za kupata bingwa wa mkoa wa Katavi. Nyundo iliyokuwa ikiongoza kwa alama 21 na mabao 24 kabla ya mchezo wa mwisho, Stand United ilihitaji mabao 13 kuwa bingwa. Kilichotokea ni Stand United kuigonga Nyundo mabao 16-0!

Timu zingine za Ligi Daraja la Kwanza zinazotuhumiwa kupanga matokeo ni Geita Gold iliyoifunga JKT Kanembwa mabao 8-0 na Oljoro JKT iliyochapwa na Polisi Tabora mabao 7-0.

Mpaka nilipokuwa naandaa makala haya, hakukuwa na taarifa zozote zilizotolewa na TFF kuhusu tuhuma hizo. Labda limechukuliwa kama tukio la kawaida!

Wapenda kandanda wanataka Shirikisho lenye viongozi wasio wanachama wa vilabu, hasa Simba na Yanga. Historia yaonesha kwamba viongozi walio wanachama wa vilabu hivyo ndio chanzo cha Shirikisho hilo kushindwa kuamua haki itokeapo migogoro hasa inayozihusisha timu za Dar es Salaam dhidi ya zile za mikoani.

Mara hii upangaji wa matokeo kwa timu nilizozitaja, hapana shaka vyama husika vya mikoa hiyo vina mkono katika upangaji wa matokeo.

Ili kukomesha hali hii, timu zilizohusika kushinda na kushindwa zishushwe daraja.
Kwa jumla, Jamal Malinzi ameshindwa kuiongoza TFF. Badala ya soka letu kwenda mbele ndio lazidi kudorora. Ajiuzulu ili kuwapisha wengine. Kinachomkawiza Malinzi kujiuzulu ni nini?
marobarnabas@yahoo.com
0715/0784 33 40 96