Kama kumbukumbu zangu ni sahihi, msimu huu umekuwa mgumu kuliko mingine iliyopita. Kwa hiyo ni vigumu kubashiri timu yenye nafasi ya uhakika kuwa ndio itakayotwaa ubingwa. Kwa kuwa kandanda ni mchezo wa makosa na bahati, basi tusubiri tuone mwishowe.
Mpaka nilipokuwa nawasilisha makala haya kwa mhariri, timu za Simba, Yanga na Azam zilikuwa zikipokezana nafasi.
Mpaka Jumatano ya juzi, timu 10 kati ya 16 zilikuwa zimecheza mechi 23 kila moja. Yanga, Mtibwa Sugar na Azam zilikuwa zimecheza mechi 21 kila moja huku Stand United, Ndanda FC na Toto Africans zikiwa zimecheza michezo 22 kila moja.
Timu tatu za juu, Simba, Yanga na Azam zilikuwa zinatofautiana kwa alama chache. Simba alama 54, Yanga 50 na Azam 47. Hata hivyo, Yanga na Azam zilikuwa nyuma kwa michezo miwili kila moja nyuma ya Simba.
Mpaka Ijumaa iliyopita, Yanga ilikuwa na mabao 51 ya kufunga na kufungwa 11, Simba mabao 41 na kufungwa 13, wakati Azam ikiwa na mabao 36 ya kufunga na kufungwa 13, Mtibwa Sugar ilifungwa mabao 14.
Katika timu hizi nne, mvutano wa kwanza ni ubingwa. Pia nafasi ya pili na ya tatu na ikishindikana, kubaki katika nafasi nne za juu. Mchuano mwingine ni kwa timu zinazopigana kukwepa kushuka daraja zikitambua fika kuwa daraja la kwanza kuna timu korofi sana pengine hata zilizo kwenye Ligi Kuu ya Vodacom.
Kinachozitia kiwewe timu zingine ni zile zilizo chini kati ya 16 ambazo zapigana kufa au kupona ili zisishushwe daraja. Timu hizo ni Coastal Union iliyokuwa na alama 19 baada ya michezo 23, African Sports na Mgambo JKT alama 20 na JKT Ruvu alama 21.
Jana Kagera Sugar iliikaribisha Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa nyumbani, wakati Simba ilikuwa wageni wa Coastal Union Mkwakwani, Tanga. Majimaji walikuwa wenyeji wa Mbeya City na Stand United waliikaribisha Ndanda SC.
Mvutano mwingine wa ligi ya msimu huu ni ushindani mkubwa wa kufunga mabao kati ya wazalendo na wageni. Yaelekea wageni wamewazidi wazalendo kwa uhodari wa ‘kuzisalimu’ nyavu kuliko walivyofanya wenyeji.
Hamis Kiiza wa Simba (Uganda) ndiye anayeongoza kwa kufunga mabao 18 akifuatiwa na Ammis Tambwe wa Yanga (Burundi) mabao 17. Donald Ngoma wa Yanga (Zimbabwe) mabao 13.
Wanafuatia wafungaji wazalendo Jeremiah Juma (Prisons) mabao 11 na Elius Maguli (Stand United) mabao 10. Baada ya hapo anajitokeza mchezaji mgeni Kipre Tcheche wa Azam (Ivory Coast) mwenye mabao 10 wakati mzalendo Ibrahim Ajib wa Simba akifunga mabao tisa.
Hii yaonesha ni jinsi gani miguu na vichwa vya wageni ilivyo na macho ya shabaha kupenyeza gozi la ng’ombe katika kimia cha wapinzani kuliko ilivyo kwa wenyeji.
Kama wachezaji wa kigeni wanaweza, kinachofanya wachezaji wenyeji kutokuwa na uwezo wa kufunga na kuwazidi wageni ni kitu gani? Ni mchecheto au hupata makengeza ya ghafla wanapofika eneo la 18 kuelekea lango la wapinzani?
Mechi za watani wa jadi huvuta hisia kubwa miongoni mwa watazamaji. Kuna matajiri wanaoahidi kuwapa wachezaji hela kama wakishinda, nao wamegawanyika sehemu mbili. Wapo wanaofanya hivyo kujifurahisha ili kuwatambia wapinzani wao mitaani.
Pia wapo matajiri wanaocheza kamari kwa kuwekeana madau makubwa hadi ya milioni kadhaa ya shilingi. Kwa hiyo tajiri anapowapa wachezaji wa timu iliyoshinda Sh. milioni 10 wakati kafutika kibindoni Sh. milioni 100 hupata faida ya Sh. milioni 90 kwa dakika 90 tu. Huenda fedha hizo hazikatwi kodi yoyote!
Ahadi za fedha wakati mwingine huwafanya wachezaji wasisimke na kuwa na matumaini yaliyovuka mpaka. Hata kama hawapo kwenye nafasi nzuri za kufunga hujibidisha vivyo hivyo na matokeo yake huzinyima timu zao ushindi.
Kwa upande mwingine, tabia ya kuwanyang’anya wachezaji simu wakiwa kambini kabla ya mechi za watani wa jadi haizuii wachezaji kurubuniwa na upande wa pili. Mechi hujulikana mapema sana wakati tarehe za michezo ya ligi zinapowekwa hadharani.
Wenye nia mbaya hupangana na wachezaji mapema sana ili siku ya mechi wacheze chini ya viwango. Hukubaliana kiasi fulani cha hela, lakini kwa masharti ya vitisho endapo mchezaji atakiuka makubaliano.
Kinachofanyika ni walinda milango na mabeki wanaoonekana kuwa kikwazo kikubwa kwa washambuliaji wa timu pinzani. Kwa mfano, mlinda mlango aliyepewa mlungula husimama sehemu tofauti ili mpira unapopigwa ajibidishe kuruka ingawa anajua hatoufikia.
Mabeki huweza kucheza rafu kwa kujitia kumzuia mshambuliaji. Huwa hivi: beki aweza ‘kumsindikiza’ mshambuliaji mpaka eneo la hatari, kisha akamchezea rafu ya wazi au akakubali ‘kunawishwa’ (kushikishwa) mpira na kusababisha penelti.
Yapo mengi ya kueleza lakini kwa leo yatosha kutokana na ufinyu wa nafasi.
marobarnabas@yahoo.com
0715/0784 33 40 96


.jpg?itok=nfwjwDzv)








