Msaada huo wenye thamani ya Sh. milioni tano, ulikabidhiwa jana kwa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesera, katika hafla fupi iliyohudhuriwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Maafa ya Mkoa na Wilaya ya Iringa.
Akikabidhi msaada huo, Meneja wa TPB tawi la Iringa, Anthony Kayanda, alisema benki yao ilipokea kwa masikitiko taarifa za madhara ya mafuriko hayo na kuungana na Watanzania wengine kuwasaidia waathirika.
“Leo tunakabidhi mifuko hii 300 ya saruji kama mchango wa benki yetu kwa waathirika hao. Ni imani yetu kwamba msaada huu utasaidia juhudi za serikali zinazolenga kuwarudisha waathirika hao katika maisha yao ya kawaida,” alisema Kayanda.
Kasesera alisema msaada huo utasaidia utekelezaji wa mpango wa serikali unaolenga kuona kaya hizo zinakuwa na nyumba bora zitakazojengwa kwa matofali ya saruji.
“Kwa kupitia mpango huo, hakuna kaya iliyoathirika itakayopewa mifuko ya saruji. Utaratibu uliowekwa na serikali ni wa kufyatua matofali na kuyagawa kwa waathirika hao ili wayatumie kujenga nyumba zao katika viwanja walivyopimiwa,” alisema Kasesera.
Aliongezea kuwa kazi ya kufyatua matofali hayo inaendelea wakati ujenzi wa nyumba hizo ukitarajiwa kuanza wakati wowote kuanzia sasa.
Alisema mpango unalenga kuzinufaisha kaya zote 100 na kila kaya itapata wastani wa matofali 1,500 watakazozitumia kujenga nyumba za vyumba viwili, sebule na choo.