Singida Utd yaitishia 'nyau' Simba

21Feb 2016
Faustine Feliciane
Dar
Nipashe Jumapili
Singida Utd yaitishia 'nyau' Simba

BAADA ya kufanikiwa kutua hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), timu ya Singida United imesema inajiandaa kuishangaza Simba katika mechi yao baadaye mwezi huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Singida Utd.

Mshambuliaji Songa Rajed aliyefunga goli moja katika ushindi wa magoli 2-0 dhidi ya Mvuvuma FC na kutinga hatua ya 16 bora, alisema kuwa mchezo utakuwa mgumu lakini wamejipanga kuishangaza Simba.

"Simba timu kubwa, hilo halina ubishi, lakini kwenye mpira kuna maajabu, tumejipanga kuwashangaza, " alisema Rajed.

Aidha, kiungo Kitoba Mhoja alisema watacheza kwa nidhamu kubwa kwenye mchezo kwa vile wanaamini Simba ni timu kubwa na yenye uwezo.

Wakati Singida United wakitinga hatua hiyo kwa kuiondoa Mvuvuma FC, Simba wenyewe walitinga hatua hiyo baada ya kuipa kipigo cha magoli 3-0 Burkinafaso FC ya Morogoro.