Kwa kutomtambua kama mwanachama wao, uongozi huo umesema hauwezi kumsimamisha Matiko kuwania ubunge kupitia chama hicho.
Hivi karibuni, Matiko alizungumza na waandishi wa habari nyumbani kwake na kutangaza nia ya kugombea ubunge kwa tiketi ya CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu wa mwakani ili kuendelea kutumikia wananchi jimboni humo.
"Nimekuwa ninapokea wito kutoka kwa wachungaji na kada mbalimbali; kinamama, vijana, wafanyabiashara na watumishi wa umma wakiniomba nigombee.
"Muda ukifika nitagombea kama ilivyokuwa uchaguzi wa mwaka 2015. Jamii iliniomba kugombea nikafanya hivyo.
"Nikipata wito toka moyoni nitagombea kupitia chama changu cha CHADEMA katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 ili kutumikia wananchi kama vile Mama (Rais Samia Suluhu Hassan) alivyojielekeza katika kutekeleza miradi mingi ya kijamii nchini," amesema .
Matiko amesema kuwa katika kipindi chake akiwa mbunge, alimaliza mgogoro kati ya wananchi wa Bugosi na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kusaidia wananchi kulipwa na kupisha eneo hilo pamoja na mambo mengine mengi, hivyo akirejea kwenye nafasi hiyo atafanya mambo mengi zaidi.
Alipoulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusu kusudio hilo la Matiko ambaye ni miongoni mwa wabunge 19 wa viti maalum ambao wamekuwa katika mgogoro wa kimaadili na chama hicho, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, amesema tayari chama hicho kimetoa miongozo dhidi ya wabunge hao.
Mnyika amesema miongozo hiyo imetolewa kuanzia ngazi za jimbo hadi mikoa yao, hivyo ni vyema uulizwe uongozi wa ngazi husika.
Mwenyekiti wa CHADEMA Mkoa wa Mara, Lucas Ngoto, amesema chama hakimtambui Matiko kama mwanachama wao, na kama anataka kurejea CHADEMA, afuate taratibu za kuomba kuwa mwanachama.
Kuhusu kutia nia kugombea ubunge wa Tarime Mjini, Ngoto amesema kuna mwanachama mmoja tu aliyetangaza nia kwa jimbo hilo ambaye ni Bobu Chacha Wangwe. CHADEMA haina baraka kwa Matiko kugombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho kwa sasa.
Amefafanua kuwa hata kama Matiko ataomba tena kuwa mwanachama wa CHADEMA, kupitishwa kuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho ni ngumu kwa kuwa kwa mujibu wa sheria tayari ameshachelewa.
"Kwa sasa yeye (Matiko) siyo mwanachama wetu, sijajua ni lini ataomba kujiunga na chama pamoja na kufanya mchakato wa kutia nia katika jimbo ambalo tayari lina mtiania na pia vikao vikafanyika kwa ajili ya kujadili na kupitisha.
"Huenda ana hatua zingine ambazo yeye (Matiko) anafahamu. Pengine ana chama kingine atakakogombea, anajua mwenyewe, lakini siyo CHADEMA," amesema Ngoto.
Matiko na wabunge wengine 18 wamekuwa na mgogoro wa kimaadili na CHADEMA, hata kufikia hatua ya kufutwa uanachama wa chama hicho.