Walimu wapewa suluhisho la mikopo kausha damu

07Dec 2023
Daniel Limbe
Chato
Nipashe
Walimu wapewa suluhisho la mikopo kausha damu

IMEELEZWA kuwa njia pekee ya kuepukana na mikopo ya kinyonyaji kwa walimu nchini maarufu mikopo kausha damu ni kujiunga na huduma za Mwalimu Saccos ili kukidhi mahitaji yao badala ya kwenda kwenye taasisi binafsi za kifedha.

Hii ni kutokana na baadhi ya walimu kukopeshwa fedha kwa riba kubwa huku baadhi yao wakiporwa kadi za benki na wamiliki wa makampuni ya kifedha, hali ambayo imekuwa ikiwasababishi maisha magumu na kushindwa kutimiza majukumu yao kikamilifu.

Akiongea na Nipashe Digital Katibu wa Chama cha ushirika cha Walimu wilaya ya Chato mkoani Geita, Mwl. Pius Katani, amesema njia pekee ya kuepukana na mikopo ya kinyonyaji ni walimu kutumia chombo chao ambacho ni rahisi kuwasikiliza na kushauriana kwa lengo la kuboresha ufanisi wa maisha tofauti na taasisi zingine ambazo hulenga kujipatia faida pekee.

"Huu ni wakati wa walimu wote wilaya ya Chato kuungana pamoja kutumia chombo chetu cha Mwalimu Saccos ili kuepukana na changamoto ya mikopo kausha damu...maana mikopo hiyo imesababisha baadhi yao kubaki na pesa kiduchu kwenye mishahara yao na hivyo kushindwa kumudu gharaama za maisha na kusababisha msongo wa mawazo" amesema Katani.