Viongozi wa Yanga wamefanya la maana

29Aug 2016
Mhariri
Dar es Salaam
Nipashe
Viongozi wa Yanga wamefanya la maana

WIKI iliyopita wachezaji wa Yanga waligomea mazoezi ya mwisho kujiandaa na machezo wao dhidi ya TP Mazembe wa kombe la shirikisho Afrika kwa kile kilichoelezwa ni kushinikiza viongozi wao kuwalipa posho zao na stahiki zingine walizoahidiwa kabla hata awajachukua ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara.

Ahadi hizo zilitolewa wakati ligi ikiendelea kwa kuahidiwa kupewa fedha endapo wangetwaa ubingwa wa ligi kuu pamoja na kombe la FA vitu ambavyo walifanikiwa kuvipata.

Mgomo huo ulianza kuibua hofu na mashabiki na wanachama wa klabu hiyo wakifikiria kuwa huenda ukaathiri mwenendo wa timu hiyo kwenye ligi kuu msimu huu iliyoanza Agosti 20.

Katika hali ya kawaida mfanyakazi yeyote asipolipwa stahiki zake utendaji wake wa kazi unapungua.

Baada ya vyombo vya habari kuanza kuripoti hali ya mambo ndani ya kikosi cha klabu hiyo, kuelezea kutolipwa kwa posho za wachezaji hao, haraka uongozi wa klabu hiyo umechukua hatua na kuweka mambo sawa.

Nipashe, inawapongeza viongozi wa Yanga kwa kuamua kulimaliza suala hilo kabla alijaenda mbali zaidi.

Jana imeripotiwa kuwa wachezaji wote wa Yanga wamelipwa stahiki zao zote walizokuwa wakidai ikiwa ni pamoja na posho na ahadi walizokuwa wakipewa na viongozi wao katika kuhakikisha timu inafanya vizuri.

Kimsingi, ilikuwa ni lazima kwa viongozi kufanya hivyo ili kuendeleza ari ya kujituma na kujitolea kwa wachezaji wao kwenye mechi dhidi yao.

Jambo hilo litaendeleza umoja na ari ya kupambana kwa wachezaji hao ambao jana walianza mikikimikiki ya ligi kuu kwa kuchuana dhidi ya African Lyon kwenye mchezo wao wa kwanza.

Tunawakumbusha viongozi wa klabu hata vyama vya michezo nchini kuwa na utaratibu wa kutimiza ahadi mnazozitoa kwa wachezaji ili kuweka mahusiano mazuri baina ya wachezaji na viongozi.

Kabla ya kutoa ahadi kunakuwa hakuna deni kati ya pande mbili, lakini pindi ahadi inapotolewa kwa makubaliano, hiyo inabaki kuwa deni ambalo ni lazima lilipwe.

Na kwa kuwa wachezaji wanafanya kazi ambayo wanalipwa mshahara kila mwisho wa mwezi kama hakuna uhakika wa kutimiza ahadi hizo, ni bora viongozi wakaacha kutoa ahadi kwa wachezaji kwa kuwa wanawafanya waamini kuna kitu cha ziada watakachokipata.

Si jambo jema kusubiri vyombo vya habari vianze kuandika malalamiko ya wachezaji ndipo hatua zichukuliwe, uwe utaratibu kwa viongozi kutimiza kile wanachokiahidi kwa wachezaji wao.

Kutekeleza ahadi kwa wachezaji kunasaidia kuwaongezea morali na kujituma zaidi pale wanapokuwa wakishiriki katika mashindano.

Vile vile, hatua hiyo inasaidia kuweka mazingira ya kuaminiana na kujenga mshikamano kati ya uongozi na wachezaji.

Tunatumia fursa hii kuupongeza uongozi wa Yanga kwa kulimaliza suala hili la posho na madai ya wachezaji wao, hatua hiyo ya Yanga iakisi kwa uongozi wa timu nyingine wenye utaratibu wa kutoa ahadi kwa wachezaji wake kukumbuka kuzitimiza.

Kazi imebaki kwa wachezaji wa Yanga, kuhakikisha kwamba wanaipa matokeo mazuri klabu yao kwa kuwa viongozi nao wameshatimiza wajibu wao wa kuhakikisha wachezaji wamelipwa madai yao ya muda mrefu.